Tofauti bado zipo kati ya Iran na mataifa makubwa duniani
Marekani na washirika wake watatu barani Ulaya Wameapa Jumamosi (21.03.2015)kuendelea na mazungumzo na Iran kuhusiana na mpango wa nchi ...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/03/tofauti-bado-zipo-kati-ya-iran-na.html
Marekani na washirika wake watatu barani Ulaya Wameapa Jumamosi
(21.03.2015)kuendelea na mazungumzo na Iran kuhusiana na mpango wa nchi
hiyo wa kinyuklia licha ya tofauti zilizopo wakati muda wa mwisho
ukikaribia.
Marekani na mataifa matatu washirika wake barani Ulaya Wameapa Jumamosi
(21.03.2015) kusonga mbele na mazungumzo pamoja na Iran kuhusiana na
mpango wa nchi hiyo wa kinyuklia licha ya tofauti zilizopo wakati muda
wa mwisho wa makubaliano ukikaribia."Tuko katika hatua muhimu katika majadiliano," waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na wenzake kutoka Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Ulaya wamesema katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo katika uwanja wa ndege wa heathrow mjini London.
"Iwapo tutaweza kutatua masuala yote makubwa, kazi ya kiufundi itafuatia kubadilisha mpango elekezi kuwa waraka wenye maelekezo."
Kerry amesema mazungumzo mjini London yalikuwa "yenye matunda" na yanaonesha kuwa mawaziri wako pamoja katika haja ya kupatikana makubaliano sahihi, na sio tu makubaliano yoyote."
Iran yatakiwa kuchukua uamuzi mgumu
Iwapo makubaliano yatapatikana , maelezo kamili ya makubaliano yanatarajiwa kufikiwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni.
Kerry na mawaziri wengine wa mambo ya kigeni mjini London wamesema Iran inahitajika "kuchukua uamuzi mgumu" kabla ya kupatikana makubaliano kamili. "Suluhisho lololote linapaswa kuwa pana, la muda mrefu na linaloweza kuthibitika," wamesema.
"Tumekubaliana kwamba kumekuwa na hatua zilizopigwa katika maeneo muhimu licha ya kuwa bado kuna masuala muhimu ambayo hayajafikiwa makubaliano." Akizungumza mapema jana Jumamosi (21.03.2015) katika mji wa Lausanne nchini Uswisi, Kerry amesema licha ya kwamba "tofauti muhimu bado zipo" na iran pande hizo mbili zina "fursa ya kujaribu kufikia makubaliano" katika muda wa siku kumi zijazo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius, wakati huo huo, amesisitiza kwamba makubaliano kamili ni lazima yafikiwe pamoja na Iran. Ni muhimu kufikia makubaliano ambayo mataifa yote ya kimkoa kama vile Uturuki na Saudi Arabia , yanaweza kuyaamini, ameiambia radio ya Ufaransa Europe 1, na kuongeza kwamba Iran yenye silaha za kinyuklia itaanzisha mashindano yenye mwelekeo mbaya ya kinyuklia katika mashariki ya kati.
Gerard Araud , balozi wa Ufaransa nchini Marekani, amesema siku ya Ijumaa (20.03.2015) kwamba msisitizo wa Marekani juu ya muda wa mwisho wa tarehe 31 Machi ni , "mbinu mbovu" ambayo inaweka "mbinyo kwetu kufikia makubaliano ya aina yoyote kwa gharama yoyote.
Iran yasema Marekani inaonesha "ubabe"
Iran imeonesha hali mchanganyiko jana Jumamosi (21.03.2015) wakati kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei alipoishutumu Marekani kwa kufanya "ubabe" na amesisitiza kwamba vikwazo ni lazima viondolewe kabla ya kufikia makubaliano.
Amesema kuwa , Marekani inasema "tutie saini makubaliano na watafanya uchunguzi kuhusu tabia yetu katika makubaliano hayo na baadaye wataondoa vikwazo, " televisheni ya Iran ya Press imemnukuu Khamenei akisema.
"Haya ni makosa na haikubaliki na Iran haitakubali hilo," Khamenei amenukuliwa akisema. Wakati Marekani iko tayari kuondoa sehemu ya vikwazo vya kiuchumi haraka, hakuna nia ya kuondoa haraka vikwazo vilivyowekwa na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vinavyopiga marufuku mauzo yanayohusiano na nyuklia nchini Iran, wamesema maafisa wa Marekani.
Rais Hassan Rowhani amesema Iran ina nia thabiti katika mazungumzo hayo na "kufikia makubaliano ya mwisho ni jambo linalowezekana," wakati waziri wa mambo ya kigeni Javad Zarif amenukuliwa akisema majadiliano yamepiga hatua muhimu" wiki hii.