Flatnews

Shilole, Nina Shaka na Uanamke Wako!

Nirahisi zaidi kumpata kama utatumia jina la Shilole, kwa sababu mashabiki wake wengi kila kona wanamtambua...


Shilole, Nina Shaka na Uanamke Wako!
Nirahisi zaidi kumpata kama utatumia jina la Shilole, kwa sababu mashabiki wake wengi kila kona wanamtambua kwa jina hilo la kisanii, ingawa alipozaliwa, wazazi wake walimpa jina la Zuwena Mohamed.

Nitakuwa sijakosea nikimuita Shilole kama mjasiriamali, kwa sababu ni mwanamke mtafutaji, siyo kama wale akina dada wanaouza sura mijini, kipato chao kikubwa wakitarajia kutoka kwa wanaume.
Huyu mdada ni shoka, anajichanganya kila sehemu ili mradi ‘chapaa’ iingie kibindoni, ndiyo maana leo utamuona kwenye filamu, kesho unakutana naye jukwaani anazungusha kiuno kama hana akili sawasawa, hiyo yote ni katika kuwapa mashabiki kile wao wanapenda, ili mwisho wa siku mkono wake uende kinywani.
Shilole anavuma zaidi kimuziki kwa sababu amefanya kazi nyingi na nzuri, kiasi kwamba amewahi kupata mialiko sehemu mbalimbali, ndani na nje ya nchi. Kibao chake kilichompa heshima kubwa kinaitwa Malele, ingawa pia aliwahi kuimba Bata Batani aliomshirikisha Abdul Kiba na Nakomaa na Jiji kuzitaja chache.
Binti huyu mwenyeji wa Mkoa wa Tabora anafanya vizuri kwa sababu aina ya muziki alioamua kuufanya, uko na watu wachache kwa hiyo upinzani si mkubwa. Wapinzani wake ni kama akina IT, Snura na wengine wachache.
Nje ya muziki, Shilole ni binadamu kama binadamu wengine, akifanya yale ambayo mimi na wewe tunafanya. Hata hivyo, uhusiano wake wa kimapenzi na Nuh Mziwanda umekuwa ukikosolewa na wapinzani wake, kwa madai kwamba yeye ni mkubwa kiumri kuliko mwenzake.
Binafsi nimewahi kumuuliza swali hilo, kama ni kweli wanavyosema kuwa ‘anambembenda’ bwana mdogo, lakini jibu lake kama inavyokuwa mara zote, ni kwamba Nuh ni mtu mzima na kwa maana hiyo, waachwe waendelee na maisha yao.
Ni kweli, Nuh anaweza kuwa ana umri mdogo kuliko Shilole, lakini ni mtu mzima anayejitambua, kwa hiyo kama ameamua kuwa na mwenza anayemzidi umri, ni uamuzi wake ambao ni makosa kumkosoa, mbona wababu wengi tu wanawaoa ‘wajukuu’ zao?
Lakini katikati ya kelele hizi, yapo madai ya mara kwa mara juu ya kuwepo kwa mizozo inayosababisha wawili hao kupigana, ingawa habari zinasema inapotokea hivyo, binti huyo ndiye anaibuka kidedea kwa kushinda pambano.
Kwetu sisi waandishi, ugomvi kati yao siyo kitu kigeni. Kinachosikitisha, mara zote Shilole ndiye anatajwa kuwa chanzo na mshindi wa kila tukio. Ninajua maisha ya ndoa yalivyo na hivyo ninaelewa ni kwa kiwango gani haipendezi habari za uhusiano wao zinapotapakaa nje. Ninafahamu juu ya uwepo wa kutokuelewana ndani ya uhusiano wa watu wengi, lakini ni wengi pia hatusikii habari zao zikitoka nje.
Kwa Shilole na Nuh, watu wanamsema vibaya mwanamke, wakisema anamuonea mwenzake kwa vile tu, yeye mambo yake ni mazuri kuliko mwenzake. Nuh ambaye pia ni msanii, hana fedha kama Shishi Baby.
Kiukweli, hatuwezi kujua nini hasa kinatokea ndani mwao, lakini maneno ya aina ileile yanapoendelea kutolewa juu ya watu walewale, yanatosha kutuma ujumbe kuwa lisemwalo lipo na kama halipo laja.
Kama mwanamke, kama staa, hatoi picha nzuri kwa jamii inayomzunguka, ambayo inaamini katika mila na desturi za Kitanzania. Asiilazimishe jamii yake kuelewa kwamba anakuwa mgomvi kwa sababu tu anaringia uwezo wake kifedha.
Sina uhakika wa wingi wa fedha alizonazo, lakini ninachoamini ni kwamba mwanamke wa kiafrika siku zote anapaswa kuwa na heshima kwa mume au bwana aliyeamua kuwa naye. Hela haina mwenyewe, leo unayo kesho hauna, kama unaamini katika uwezo kifedha, maana yake ni utumwa.
Kesho na keshokutwa hela ikiondoka, utakuwa tayari kunyanyasika kwa vile unaamini katika mkwanja, kitu ambacho siyo kweli. Utu na heshima kwanza!
Chanzo: Za Chembe Lazima  Ukae by Ujuku Abraham, GPL

Related

Shilole 885415176879177435

Post a Comment

emo-but-icon

item