Obama aikosoa hotuba ya Netanyahu
Rais Barack Obama amemkosoa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusiana na hotuba yake katika bunge la Marekani, kuhusu makubalia...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/03/obama-aikosoa-hotuba-ya-netanyahu.html
Rais Barack Obama amemkosoa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
kuhusiana na hotuba yake katika bunge la Marekani, kuhusu makubaliano
yanayotarajiwa kufikiwa kati ya Marekani na Iran ya mpango wa nyuklia
Baada ya Netanyahu kutoa hotuba hiyo katika bunge la Marekani hapo jana, Obama alijibu kwa kusema kuwa kiongozi huyo wa Israel hana mpango wowote mbadala unaoweza kukikabili kitisho hicho cha Iran. Na, wakati Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry akifany amazungumzo na mwenzake wa Iran nchini Uswisi, mataifa yenye nguvu duniani yanashinikiza kupatikana muafaka ambao utapunguza uwezo wa Iran wa nishati ya nyuklia, kwa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.
Katika hotuba yake, Netanyahu hakuficha msimamo wake huku akiyapinga makubaliano anayotarajia kuwa Iran itasaini na Marekani kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Obama hakutazama hotuba hiyo, kwa sababu alikuwa kwenye kikao alichoandaa kwa njia ya video na viongozi wa Ulaya kuhusu mzozo wa Ukraine, lakini baadaye alitoa hisia zake kuhusu hotuba hiyo.
Wakati wabunge kadhaa wa chama cha Obama cha Democratic wakisusia hotuba hiyo ya Congress, wabunge wengine wengi kutoka pande zote mbili walihudhuria na kumpigia makofi Netanyahu.
Lakini licha ya hayo, baadhi ya Wademocrats walimkosoa kwa kile walichokiita kuwa ni “kuzusha hofu”. Kiongozi wa wabunge wa upinzani wa chama cha Democratic katika baraza la wawakilishi Nancy Pelosi alisema “amehuzunishwa na kile alitaja kuwa ni matusi kwa busara ya taifa la Marekani”.
Wiki mbili kabla ya uchaguzi nchini Israel ambako anawania kuchaguliwa tena, Netanyahu amesema kwamba makubaliano yoyote na Iran yanatishia uhai wa taifa lake. Pia amesema kwamba kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameandika katika ukurasa wa Twitter kwamba Israel ni lazima iangamizwe. Iran imezipinga kauli za Netanyahu, huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje Marzieh Afkhan akimshtumu Netanyahu kwa kueneza uwongo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambao serikali ya Iran inasisitiza ni wa amani.