Flatnews

Kiir na Machar wajadili mpango wa amani

Mazungumzo ya kupata suluhu ya kudumu ya mzozo wa Sudan Kusini yamerefushwa kwa siku moja. Rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar w...


Mazungumzo ya kupata suluhu ya kudumu ya mzozo wa Sudan Kusini yamerefushwa kwa siku moja. Rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar wanaokutana Addis Ababa bado hawajafikia makubaliano ya amani.
Riek Machar na Salva Kiir
Jumuiya ya Ushirikiano ya nchi za Mashariki na pembe ya Afrika IGAD ilikuwa imewapa Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar muda hadi Alhamisi saa sita usiku kufikia makubaliano mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mpatanishi mkuu wa IGAD, Seyoum Mesfin, alionekana kuwa mwenye
matumaini wakati mkutano ulipokuwa ukiendelea: "Leo ni siku ya mwisho ya mazungumzo. Ni siku ya mwisho lakini bado wanajadiliana wakiwa na matumaini kuwa wataafikiana. Sisi tutaendelea kuwatia moyo ili waweze kufikia makubaliano."
Hata hivyo matarajio ya kupatikana muafaka yalififia baada ya Kiir na Machar kuondoka ghafla. Waliahidi kurejea kwenye meza ya mazungumzo lakini hawakufanya hivyo. Wanadiplomasia wa IGAD hivyo walilazimika kurefusha muda wa mkutano hadi Ijumaa jioni. Mpaka hapo Kiir na Machar wanatakiwa wasaini makubaliano ya amani. Hii ni mara ya nane kwa mazungumzo kama hayo kufanyika lakini kila wakati yameshindwa kuzaa matunda. Akiuzungumzia mgogogro wa Sudan Kusini Seyoum Mesfin wa IGAD alisema: "Suala la ulinzi, suala la kugawana madaraka. Hayo yote ni mambo ya muhimu yanayowafanya wazozane na kwa sasa ndio wanayajadili."
Nia ya kweli ipo?
Vita vimewafanya wananchi milioni 1.5 wayakimbie makazi yao Vita vimewafanya wananchi milioni 1.5 wayakimbie makazi yao
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini Sudan Kusini mwezi Desemba mwaka 2013 baada ya Kiir kudai kuwa Machar, aliyekuwa makamu wake kwa wakati huo, alikuwa amepanga njama za kumpindua. Baada ya shutuma hizo wafuasi wa viongozi hao wawili wakaanza kushambuliana. Miezi 15 baadaye bado hakuna amani Sudan Kusini. Watu 10,000 wameuliwa na wengine milioni 1.5 kulazimika kuyakimbia makazi yao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amewataka Kiir na Machar wafikie makubaliano haraka. Umoja wa Mataifa mapema wiki hii ulipitisha azimio litakalouruhusu kuwawekea vikwazo wale wote watakaozuia juhudi za kuleta amani.
Iwapo makubaliano ya amani yatafikiwa basi mpango uliopo utaitaka Sudan Kusini iunde serikali ya mpito ifikapo katikati ya mwezi Aprili. Wachambuzi wanashuku kama kweli Kiir na Machar wana nia ya kupata suluhu. Duru hii ya mazungumzo ilipoanza Februari 23, hakuna hata mmoja wao aliyeona umuhimu wa kuhudhuria.

Related

NEWS 4112707195503689128

Post a Comment

emo-but-icon

item