Ubalozi wa Tanzania nchini Oman unastahili pongezi
Naibu Balozi wa Tanzania nchini Oman Juma Othaman (mwenye Kaunda suti) akipokea Tunzo ya ushiriki iliyotolewa na Mwakilishi kutok...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/02/ubalozi-wa-tanzania-nchini-oman.html
Naibu
Balozi wa Tanzania nchini Oman Juma Othaman (mwenye Kaunda suti)
akipokea Tunzo ya ushiriki iliyotolewa na Mwakilishi kutoka Manispaa ya
Mji wa Muscat ambao ni Waandaaji wa Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa,
Ubunifu na Utamaduni. Tanzania imepeleka zaidi ya Watu 40 kuonesha kazi
wanazoifanya za sanaa ikiwemo,Uchongaji,uchoraji na ufumaji wa nguo.
Kulia ni Kiongozi wa Msafara huo Khadija Battashy na kushoto ni Msaidizi
kiongozi Masha Hussein. Picha na Faki Mjaka, Muscat Oman
Naibu
Balozi wa Tanzania nchini Oman Juma Othman (katikati) akiwa kashika
Tunzo ya ushiriki wa Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa, Ubunifu na
Utamaduni nchini Oman waliyopewa kutoka Manispaa ya Mji wa Muscat ambao
ndio waandaaji wa Maonesho hayo. Kulia kwake ni Kiongozi wa Msafara wa
Washiriki kutoka Tanzania Khadija Battashy na kushoto ni Msaidizi
kiongozi Masha Hussein na Mkuu wa mambo ya kiufundi wa Msafara Moza
Habib.
Na Faki Mjaka, Muscat Oman
Msemo
wa Kiswahili usemao ‘aisifiaye Mvua huwa imemnyeshea’ unafanana kwa
mbali na ule usemao ‘adhabu ya Kaburi aijuaye Maiti’. Misemo hii
huonesha jinsi ambavyo muhusika kwenye tukio husika ndiye mwenye uelewa
mpana zaidi wa kufahamu umuhimu au madhara ya jambo fulani.
Hata
kunapotokea tatizo la kihalifu na kutakiwa ushahidi mara nyingi Polisi
huanzia kuwakamata wale waliokuwa katika tukio hilo ili kusaidia kutoa
ushahidi wa awali.
Mantiki
ya utangulizo huo ni kusifia namna gani Ofisi ya Balozi wa Tanzania
nchini Oman ilivyofanikisha Maonesho ya kimataifa ya Sanaa,Ubunifu na
Utamaduni yanayofanyika nchini Omani na namna Maonesho hayo yanavyoweza
kuisaidia Tanzania kupiga hatua mbele katika Sekta ya Kiutalii.
Sifa
hizo za Ubalozi hazitakuwa lolote bila kuisifia Manispaa ya Muscat na
Serikali ya Omani kwa ujumla kwa kuialika nchi ya Tanzania kushiriki
katika Maonesho hayo yanayofanyika kwa muda wa mwezi mmoja. Ushiriki huo
unaonesha namna gani Tanzania ilivyokuwa na mahusinao mema na nchi
hiyo. Katika maonesho hayo ni nchi chache Rafiki wa Omani zilizoalikwa
kuonesha bidhaa na vivutio vyake ikiwemo China, Ufaransa, Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran, India, Thailand, Morocco, Uzbekistan, Misri na
Tanzania.
Kwa
hakika kuna faida nyingi zilizopatikana katika Maonesho hayo lakini
kubwa kuliko ni namna ambavyo Tanzania ilivyotumia nafasi hiyo
kikamilifu kujitangaza kwa Wanachi wa Omani na Wageni lukuki ambao
walifanikiwa kufika katika Banda la Tanzania au kupata taarifa kupitia
Vyombo vya habari vinavyoripoti Maonesho hayo.
Mkuu
wa Utawala katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Oman Abdallah
Kilima anasema walitakiwa kualika Wanasanaa na Wajasiriamali wa
kitanzania watakaoonesha kazi zao wanazozitengeneza kwa mikono, hivyo
likaja wazo la kutafuta Kampuni ya Utalii ambayo itakuja kutoa huduma ya
kutangaza Vivutio vya Tanzania kwa vile uwepo wa bidhaa hizo huambatana
na uwepo wa Wageni(Watalii).
“Kwanza
Banda tuliliweka strategically, wenyeji wetu walitaka tuepeleke watu wa
bidhaa za Mikono, moja kwa moja tukajua tu kuwa bidhaa hizi
zinaambatana na ujio wa wageni wengi kwani ni kivutio cha Watalii hapo
ndio ikawa bahati ya kuwaalika Pongo Safaris&Tours”Alisema Kilima.
Kweli
banda liliwekwa Kimkakati maana Unapoingia katika Banda hilo la Tanzania
unakutana na Bango kubwa lenye Mlima Kilimanjaro linalosomeka “Welcome
Tanzania, The Land of Kilimanjaro, Zanzibar and The Serengeti” ambapo
harufu ya viuongo kama vile Karafuu inahanikiza uzuri na upekee wa Banda
hilo.
Screen
kubwa inayoonesha vivutio mbalimbali kama vile Mbuga za Wanyama, Maziwa
,Fukwe nzuri za Zanzibar na Hoteli zake huku Mavazi ya kimasai na
Vinyago katika Banda hilo vikiwa ni vivutio tosha kwa wageni kuingia.
Kwa
vile Ubalozi ulidhamiria haukumuacha mkono Mwakilishi kutoka Kampuni ya
Pongo Safaris&Tours na hivyo kumsaidia kwa kumkutanisha na Wadau
wakubwa wa Kampuni za Omani zinazojishughulisha kusafirisha Watalii ili
kubadilishana uzoefu na kupanga namna ya kufanya kazi kwa pamoja.
Kampuni hizo nipamoja na Marmul Travels, Khimji Travel House na National
Travel and Tourism (NIG).
Kilima
anasema Ofisi zingine na Wadau wengine wa Utalii wafahamu kuwa Soko la
Utalii ni kubwa nchini Oman na halijaharibiwa hivyo kuna haja Watu
kuchangamkia fursa hiyo ili Watalii badala ya kwenda kutembea nchi za
Mashariki ya Mbali na Magharibi waje nchini Tanzania.
Kwa hakika kama watahamasishwa vilivyo kuna uwezekano mkubwa wa kubadili mwelekeo na hilo linawezekana.
Katika
kuonesha namna ambavyo Tanzania imejitangaza zaidi ya Makundi ya watu
150 wamejisajili kuja Tanzania kwa ajili ya kufanya shughuli ya Utalii
kupitia Kampuni ya Kusafirisha Watalii maarufu kama Pongo
Safaris&Tours.
Bi
Annah Shangvi Mwakilishi kutoka Pongo Safari&Tours anasema katika
Watu waliojisajili kuja Tanzania wapo pia Wanafunzi wa Vyuo Vikuu, Shule
za kawaida na watu mbalimbali wenye hadhi tofauti baada ya kuvutiwa na
Tanzania.
Anasema
wapo pia Wenyeji wa Oman na wageni mbalimbali kutoka nchi za Asia kama
Wahindi, Wairani, Wachina na Wazungu kutoka nchi mbalimbali ambao zaidi
wamevutiwa na kupanda Mlima Kilimanjaro, Kuwinda na kutembelea Zanzibar.
Bi
Anna Shangvi amedai kuwa katika kuchunguza kwake amebaini kuwa Makampuni
kutoka Kenya yanayojishughulisha kusafirisha Watalii huwa wanaongopa
kwa kusema kuwa Mbuga ya Masai Mara ndio Manyara na Mlima Kilimanjaro
haupo Tanzania bali upo Kenya.
“Kwa
kweli Maonesho haya yamesaidia sana kuweka ukweli hadharani, Wageni
wanaokuja hapa Wanalazimika kuamini kuwa Kilimanjaro ipo Tanzania na
Mbuga ya Manyara ni tofauti na Masai Mara..CD na Ramani zinasaidia sana
tunapowaonesha kutufahamu kwa haraka” Bi Annah alisema.
Vipeperushi
na Machapisho mbalimbali zaidi ya 1,000 kutoka Mamlaka ya Mbuga Taifa
(TANAPA) na vile vilivyotoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na
Michezo Zanzibar viligawiwa kwa Wageni mbalimbali waliokuwa na shauku ya
kuijua Tanzania.
Ukweli
nikwamba Wananchi wa Oman wanapenda kuzuru nchi mbalimbali duniani
kiutalii mfano mdogo ni nchi ya Thailand ambapo kwa mujibu wa Gazeti la
Oman ‘Times of Oman’ toleo la jana Februari 14, amekaririwa Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Utalii nchini Thailand Bw. Chalermsak Suranant akisema
makadirio yao ni kupata Watalii 90,000 kwa mwaka 2015 kutoka nchi ya
Oman.
Suranant
anasema kupitia Kampeni mpya waliyoipa jina la “2015 Discover Thainess”
wanatarajia hamasa itaongezeka zaidi kwa Wananchi wa Oman kwenda
kutalii Thailand mwaka huu ambapo kwa mwaka jana Jumla ya Watalii 75,000
walitembelea nchi hiyo.
Katika
hali ya kawaida mtu hawezi kwenda sehemu anayotarajia kwenda kupumzika
au kustarehe huku akiwa na kasumba au upofu wa taarifa ya huko
anakokwenda. Uwingi wa Watalii hao kutoka Oman bila shaka umechangiwa na
Waoman wenyewe kuwa na Taarifa sahihi zinazoshawishi vivutio vya huko.
Maonesho
haya kwa hakika imekuwa ni Mwanzo mzuri kwa Tanzania maana Vyombo vya
habari vya Oman havikuwa na ubinafsi katika kuyatangaza maonesho hayo
kupitia mtangazo ya moja kwa moja kwa moja au ya kurikodiwa.
Taarifa
mbalimbali na Makala maalum za kuisifia Tanzania na Vivutio vyake
katika Magazeti na Majarida yao yanayoandikwa kwa Kiarabu na yale
yanayoandikwa kwa Lugha ya Kingereza zimehanikiza sifa ya Tanzania
kuzidi kujulikana kwa Wenyeji na Wageni wa Oman.
Kwa
vyovyote iwavyo ni wakati sasa wa kukaa Mkao wa kula na kuzidi kuandaa
mazingira rafiki ya kupokea Watalii wapya kutoka nchi Tofauti ambao ni
Matokeo ya Ushawishi unaotokana na nafasi waliyoipata Tanzania ya
kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa, Ubunifu na Utamaduni
nchini Oman.
Mkuu
wa Msafara wa Watanzania hao Bi Khadija Battashy anasema imefika wakati
wa kubadilika na kuepuka kutegemea soko la nchi za Ulaya na Marekani kwa
ajili ya Utalii nchini Tanzania. Vivutio vingi na vyaupekee na hali ya
Usalama iliyopo Zanzibar na Bara haiendani sawa na Idadi ndogo ya
Watalii wanaukuja Tanzania.
Bado
kuna kazi kubwa ya kufanya kuitangaza Tanzania na Vivutio vyake. Kazi
iliyofanywa na Ofisi ya Balozi wa Tanzania Nchini Oman chini ya Bw. Ali
Ahmed Saleh ya kufanikisha Ushiriki wa zaidi ya Watanzania 40 walioenda
kuonesha vipaji vyao katika Maonesho hayo inafaa kuigwa na Ofisi zingine
za Kibalozi pale fursa zinapotokea.
.jpg)
.jpg)