Washukiwa kadhaa wa ugaidi wakamatwa barani Ulaya
Mataifa ya Ulaya yamewakamata washukiwa kadhaa wa Uislamu wa itikadi kali jana Ijumaa(16.01.2015)wakati Ubelgiji imesema imesambaratisha...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/01/washukiwa-kadhaa-wa-ugaidi-wakamatwa.html
Mataifa ya Ulaya yamewakamata washukiwa kadhaa wa Uislamu wa itikadi
kali jana Ijumaa(16.01.2015)wakati Ubelgiji imesema imesambaratisha,
kikundi cha "magaidi" waliokuwa wakipanga kuwauwa maafisa wa polisi.
Na Ufaransa ikifuatilia taarifa mpya kuhusiana na mashambulio ya wiki iliyopita mjini Paris.Misako hiyo imeleta hofu mpya juu ya maelfu ya vijana wa mataifa ya Ulaya wanaoaminika kuwa wamekwenda katika mataifa ya mashariki ya kati kupigana pamoja na kundi linalojiita Dola la Kiislamu na makundi mengine yenye mafungamano na al-Qaeda kabla ya kurejea nyumbani na kufanya mashambulio.
Washukiwa wawili wa jihadi wamepigwa risasi na kuuwawa katika mapambano makali ya silaha wakati wa msako dhidi ya ugaidi katika mji wa mashariki mwa Ubelgiji wa Verviers, karibu na mpaka na Ujerumani, usiku wa Alhamisi, wamesema waendesha mashtaka.
Washukiwa wakamatwa
Polisi imewakamata watu 13 wakati wa msako huo nchini Ubelgiji, watano kati yao wamefunguliwa mashitaka baadaye kwa "kushiriki katika shughuli za kundi la kigaidi", msemaji wa idara ya waendesha mashitaka Eric Van der Sijpt ameliambia shirika la habari la AFP.
Hapo kabla ameuambia mkutano na waandishi habari kuwa kundi hilo, baadhi yao wamerejea hivi karibuni kutoka Syria, lilikuwa ukingoni mwa kufanya mashambulizi ya kigaidi kuwauwa maafisa wa polisi mitaani na katika vituo vya polisi.
Polisi wamepata bunduki nne chapa Kalashnikov, miripuko, risasi na vifaa vya mawasiliano katika msako huo, pamoja na sare za polisi.
Kurasa za Twitter za makundi ya jihadi baadaye zimewatambua watu hao wawili waliouwawa kuwa ni Radwan Haqawi na Tareq Jadoun na kuchapisha kile ilichosema ni picha zao wakiwa nchini Syria. Maafisa wa Ubelgiji hawakuthibitisha majina yao.
Wabelgiji wengine wawili wamekamatwa nchini Ufaransa baada ya kudaiwa walikuwa wanakimbia msako huo na walikuwa wanaelekea nchini Italia, chanzo cha polisi kimesema. Ubelgiji imeomba watu hao warejeshwe nchini humo.
Polisi ya Ufaransa imewakamata watu 12 usiku na kuwahoji juu ya uwezekano kwamba huenda walitoa msaada kwa washambuliaji waliokuwa na silaha mjini Paris, ndugu wawili Said na Cherif Kouachi na Amedy Coulibaly, chanzo cha polisi kimesema.
Nchini Ujerumani anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi la Waturuki na Warusi linalopanga kufanya shambulio nchini Syria na mtu ambaye anahusika na kutoa fedha za kugharamia shughuli za kigaidi wamekamatwa katika msako dhidi ya maeneo ya washukiwa wa kundi la Waislamu wenye itikadi kali ndani na kuzunguka mji wa Berlin ambapo zaidi ya polisi 200 walihusika, wamesema maafisa.
Maandamano ya kupinga Charlie Hebdo
Maelfu ya watu wameandamana duniani na ghasia zimezuka nchini Niger na Pakistan wakati Waislamu wakionesha hasira zao kuhusiana na kuchapishwa kwa katuni mpya za Mtume Muhammad na gazeti la Charlie Hebdo.
Watu wanne wameuwawa na 45 wamejeruhiwa katika mji wa pili nchini Niger wa Zinder katika maandamano ambayo yaligeuka kuwa ya ghasia ambapo waandamanaji waliingia na kuharibu makanisa matatu na kuchoma moto kituo cha utamaduni cha Ufaransa.
Kiasi watu watatu wamejeruhiwa wakati waandamanaji wakipambana na polisi nje ya ubalozi wa Ufaransa mjini Karachi, Pakistan. Miongoni mwao ni mpiga picha wa shirika la habari la AFP, ambaye alipigwa risasi mgongoni.
Marekani imeshutumu ghasia hizo, ikisema kuna haki za msingi kwa vyombo vya habari kuchapisha kwa uhuru aina yoyote ya taarifa , ikiwa ni pamoja na vikatuni.
Mjini Washington , rais Barack Obama na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron wameapa kuisaidia Ufaransa na nchi nyingine kuushinda ugaidi duniani kwa ushirikiano mkubwa na uchunguzi.
"Tutaendelea kufanya kila lililo katika uwezo wetu kuisaidia Ufaransa kutafuta haki inayohitajika .. kuweza kuishinda mitandao hii ya kigaidi," Obama amesema.
Hata hivyo , Obama ameongeza kwamba kuijumuisha jamii ya Waislamu inawezekana kufanywa kwa ubora zaidi katika bara la Ulaya na kusema " ni muhimu kwa Ulaya kutojibu kwa kutumia nyundo na sheria pamoja na jeshi kwa matatizo haya.
Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel amesema yuko tayari kuliweka jeshi mitaani kuhakikisha usalama baada ya misako hiyo. Ameongeza kiwango cha tahadhari ya ugaidi nchini humo kuwa katika kiwango cha juu katika nafasi ya nne.
Shule za Wayahudi mjini Brussels na mji wa bandari wa Antwerp zimefungwa jana Ijumaa(16.01.2015). Misako hiyo inakuja chini ya mwaka mmoja baada ya watu wanne kupigwa risasi na kuuwawa katika shambulio dhidi ya nyumba ya makumbusho ya Wayahudi mjini Brussels.