Maoni: Sisi sote ndiyo Jamhuri ya Ufaransa!
Hayakuwa tu maandamano ya maombolezo, bali pia ya kuonyesha mshikamano mjini Paris. Lakini pamoja na furaha yote juu ya mshikamano huo, ni...
https://samchardtz.blogspot.com/2015/01/maoni-sisi-sote-ndiyo-jamhuri-ya.html
Hayakuwa tu maandamano ya maombolezo, bali pia ya kuonyesha mshikamano
mjini Paris. Lakini pamoja na furaha yote juu ya mshikamano huo, ni
wakati tu unaoweza kuonyesha iwapo umoja huo utadumu, anasema Barbara
Wesel
Mtu angeweza kuwahusudu Wafaransa kwa siku hii, kwa sababu yalikuwa
maandamano yenye nguvu isiyo kifani. Baada ya matukio ya umwagaji damu ya wiki iliyopita, wameonyesha dhamira ya kuvutia kwa historia na maadili ya taifa lao na misingi yake. Maandamano hayo ya watu zaidi ya milioni 1.5 mjini Paris, na karibu milioni mbili katika maeneo mengine ya nchi, yalionyesha dhamira ya nguvu kwa demokrasia, na kutotishwa na vitendo vya kigaidi. Juu ya yote, walionyesha kuwa hawako tayari kuacha kile wanachokiona kuwa ni muhimu kwao: uhuru wa maoni. Ni sehemu ya mila za Ufaransa, hata maoni yaliyopitiliza yanaweza kutolewa, na yanayokinzana na demokrasia.
Mshikamano mkubwa - wakati mwingine kama kejeli!
Viongozi kutoka mataifa zaidi ya 40 walikwenda mjini Paris kuonyesha mshikamano wao kwa kushiriki maandamano hayo. Uwepo wa waziri mkuu wa Israel Benjamin Nenyatahu akiwa bega kwa bega na rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas, haukukosa vituko. Kwa mara ya kwanza wawili hao walishiriki maandamano pamoja, lakini Netanyahu hakutumia wasaa huo maalumu kama ishara ya amani. Badala yake aliwatolea mwito Wayahudi wa Ufaransa kuhamia nchini Israel kufuatia matukio ya wiki iliyopita. Na kipi alikuwa akiwaza waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov wakati akiwa safu moja na rais wa Ukraine Petro Poroshenko kwa ajili ya uhuru na demokrasia? Mtu anaweza kutoa tafsiri ya kusikitisha au kejeli kulingana na hali aliyoiona.
"Dunia inasimama" yaliandika magazeti ya Jumapili nchini Ufaransa kwa namna ya kujifaharisha kuona kwamba nchi yao imevutia usikivu wa ulimwengu kwa siku hiyo. Kwa sababu Wafaransa wanatafuta uthibitisho na uungwaji mkono kutoka nje. Wanajiona katika msitari wa mbele kutetea maadili ya demokrasia na bado wana hofu kwa sababu wanajua kitisho kinachotokana na ugaidi wa ndani bado kinaendelea. Sawa na nchi jirani ya Uingereza, itikadi kali za dini ya Kiislamu zimekita mizizi katika vitongoji vya mjini Paris, ambazo zinaelekea kuwa ngumu kudhibitiwa.
Jamhuri kama utambulisho wa pamoja
Kulikuwa na ishara nyingi za ubinaadamu na raia katika siku hizi- waandamanaji walibeba mabango yenye ujumbe wa "mimi ni Charlie Hebdo, mimi ni askari polisi, mimi myahudi," ili kuikumbusha jamii kuwa wahanga wote walikuwa binaadamu. Na kila mahala kila mmoja alikuwa akijitambulisha na Jamhuri ya Ufaransa.
Lakini baada ya muda huu mfupi wa mshikamano, nchi hiyo inarejea kwenye matatizo yake yaliyoigawa kwa muda sasa. Malumbano ya kisiasa yalikuwa yamesimama hadi Jumapili - na sasa yanarejea. Wanasiasa wataanza kutupiana lawama kuhusiana na matukio ya mji mkuu. Lakini kinachopaswa kuanza kwa ukweli ni mjadala juu ya hali za maisha ya wahamiaji kutoka Afrika Kaskazini. Ufaransa imelipuuza tatizo hilo kwa miongo kadhaa. Hali mbaya katika vitongoji, shule duni, vijana wasiyo na fursa na matumaini, ambao hawajioni hata kama sehemu ya Jamhuri hii na magereza yasiyo ya kibinaadamu vimeyafanya maeneo yao kuwa kitovu cha itikadi kali.
Ufaransa itahitaji mpango endelevu wa mageuzi ili kuboresha maisha ya mamilioni ya Wafaransa wenye asili ya uhamiaji. Pamoja na hayo inapaswa kuhakikisha kwamba mkakati huo hauyanufaishi makundi yenye siasa kali za mrengo wa kulia. Mwisho wa maneno mazito ya siku zilizopita, yaonekana nafasi nyingine yakusawazisha inapotea.