Flatnews

Serikali mbili dhahiri Bunge la Katiba


Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samuel Sitta. PICHA |MAKTABA 
  • Jana, baadhi ya kamati hizo zilianza kujadili sura namba 7, 8, 11, 14 na 15 ambazo zinagusa masuala kadhaa yanayohusu muundo wa muungano, huku zikigawa baadhi ya majukumu kwa serikali za nchi washirika – Tanganyika na Zanzibar.


Dodoma. Wakati kamati za Bunge Maalumu zikiendelea na uchambuzi wa Rasimu ya Katiba, mwelekeo wa kuzika muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba umejidhihirisha huku mabishano yakitawala katika baadhi ya kamati kuhusu suala hilo.
Jana, baadhi ya kamati hizo zilianza kujadili sura namba 7, 8, 11, 14 na 15 ambazo zinagusa masuala kadhaa yanayohusu muundo wa muungano, huku zikigawa baadhi ya majukumu kwa serikali za nchi washirika – Tanganyika na Zanzibar.
Habari kutoka katika baadhi ya kamati zinasema baadhi ya maneno kama vile ‘serikali za nchi washirika na Rais wa Tanganyika yamependekezwa kufutwa, huku baadhi ya wenyeviti wakisema wanajadili sura hizo kwa kuzingatia mapendekezo yao ya awali.
Tayari kamati zote zilishajadili sura namba moja na sita zinazohusu muundo wa muungano na nyingi zilipendekeza kuendelea kwa muundo wa serikali mbili, lakini uamuzi wa mwisho haujafanyika katika Bunge hadi sasa kutokana na mvutano ulioligawa kuhusu suala hilo.
Kamati namba moja inayoongozwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais, Ummy Mwalimu imependekeza kuundwa kwa sura maalumu ya ardhi na rasilimali ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Sura hiyo haimo kwenye Rasimu ya Katiba kwani Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipendekeza suala hilo kuwa chini ya serikali za nchi washirika.
“Kamati iliona kwamba kuna changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji, tukaamua tuwe na sura mpya ya ardhi ambayo itazungumzia masuala ya ardhi,” alisema Mwalimu.
Kuhusu hoja kwamba kufanya hivyo ni kwenda nje ya Rasimu ya Katiba iliyoacha suala hilo mikononi mwa nchi washirika, Mwalimu alisema kamati yake inachambua sehemu za rasimu zilizobaki kwa kuzingatia mapendekezo yake ya awali ya muundo wa muungano wa serikali mbili.
Juzi, kamati ya wajumbe wanaowakilisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji wadogo wa madini waliwasilisha kwa Katibu wa Bunge Maalumu mapendekezo ya sura mpya inayohusu masuala ya ardhi, maliasili na mazingira.
Mmoja wa wajumbe hao kutoka kundi la wakulima, Hamis Dambaya alisema walichukua hatua hiyo kutokana na makundi hayo kutokutajwa kwa kina katika Rasimu ya Katiba.
“Tuliwasilisha mapendekezo yetu kwa Katibu jana (juzi) na leo (jana) tumeambiwa kwamba kuna Kamati ya Uongozi, hatujui pengine huenda yakajadiliwa na kuruhusiwa kupelekwa kwenye kamati zote kwa ajili ya kujadiliwa,” alisema Dambaya.

Post a Comment

emo-but-icon

item