Mjumbe afuatwa wodini kupiga kura
https://samchardtz.blogspot.com/2014/08/mjumbe-afuatwa-wodini-kupiga-kura.html
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Kundi la 201, Thomas Mgoli
akiwa amelazwa katika Hospital ya Mkoa wa Dodoma, jana. Picha na
Emmanuel Herman
- Tukio hilo limekuja kukiwa na taarifa kuwa baadhi ya kamati zinashindwa kupiga kura kuamua au kuchelewa kuanza vikao vyake kutokana na tatizo la akidi.
Dodoma. Mbunge aliyelazwa
katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Thomas Mgilo baada ya kupigwa na
watu wasiojulikana amefuatwa hospitalini ili apige kura kupitisha baadhi
ya sura za rasimu.
Tukio hilo limekuja kukiwa na taarifa kuwa baadhi
ya kamati zinashindwa kupiga kura kuamua au kuchelewa kuanza vikao vyake
kutokana na tatizo la akidi.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalumu, idadi ya
wajumbe wanaotakiwa ili kuruhusu kikao kuanza ni nusu ya wajumbe wote,
wakati theluthi mbili inatakiwa wakati wa kupiga kura.
Jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati namba 12,
Thuwayba Kisasi akiwa ameongozana na polisi walimpelekea karatasi za
kupiga kura Mgilo na alipiga kura ya wazi kuamua kuhusu Ibara ya 39 ya
Sura ya Nne ambayo pamoja na mambo mengine, inazungumzia haki za
mtuhumiwa au mfungwa.
Ibara hiyo inataka kutoa ruhusa kwa wafungwa wenye
ulemavu kuingia na magongo yao kifungoni, jambo ambalo Mgilo
alilipinga. Alisema hawezi kuunga mkono wafungwa wenye ulemavu kwenda na
magongo gerezani kwani wanaweza kuyatumia kuwadhuru wengine.
Mwenyekiti wa Kamati namba 12, Paul Kimiti alisema Mgoli aliomba kushiriki katika upigaji huo wa kura.
“Nilimtembelea mgonjwa (Mgoli) asubuhi akasema
hali yake ni ahueni na akaomba kwa mwenyekiti ashiriki kupiga kura
katika kamati,” alisema Kimiti.
“Kwa hiyo nilimtuma Makamu Mwenyekiti akaenda huko
hospitali na kweli mgonjwa wetu amepiga kura na leo tulipigia kura Sura
namba 2, 3, 4 na tano na tayari kamati yangu ilipata kura za kutosha
kwa pande zote za muungano.”
Changamoto ya akidi
Kumekuwa na taarifa za ama kuchelewa kuanza kwa
vikao vya kamati au kamati kuahirisha kufanya uamuzi kutokana na idadi
ya wajumbe kutokidhi matakwa ya kikanuni, huku kamati nyingine zikiamua
kutozingatia suala hilo.