WANAOMKOSOA JK KUHUSU KATIBA HAWAKO SAHIHI...( IMEANDIKWA KWENYE MWANANCHI)
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/ofisi-ya-rais-imesema-kuwa-wanaomkosoa.html
Ofisi ya Rais imesema kuwa wanaomkosoa Rais Jakaya Kikwete kuhusu msimamo wake katika mchakato wa Katiba Mpya hawako sahihi kwa kuwa ni mlezi na ana haki ya kutoa maoni yake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa.
Pia,
imewataka wasiokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba waiache kazi hiyo
mikononi mwa Bunge hilo kwa sasa hadi hapo rasimu itakapowasilishwa kwa
wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya kuikubali au kuikataa.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva
Rweyemamu ikiwa ni siku moja baada ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), kutoa tamko zito kwa Rais Jakaya Kikwete ikiishangaa kauli yake
ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na
maoni ya Watanzania.
Rais
Kikwete amekuwa akilaumiwa na taasisi na watu binafsi baada ya
kulieleza Bunge la Katiba kuwa kuna baadhi ya mambo kwenye Rasimu ya
Katiba ambayo hayawezekani kutekelezeka, akitoa mfano wa muundo wa
Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo CCT ilisema jana kuwa alitakiwa
alifanye wakati Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikimfuata
kumweleza maendeleo ya kazi yao.
Hata hivyo jana, Rweyemamu aliliambia
gazeti hili kuwa: "Kinachoendelea
kwa sasa kwa baadhi ya makundi ya kidini kutoa matamko dhidi ya Rais si
sahihi, kwa kuwa Rais ni mlezi na ana haki ya kutoa mtazamo wake kama
mkuu wa nchi na kama mwanasiasa."
Alisema
kimsingi mchakato huo ni wa kisiasa na Rais ni mwanasiasa, pia ni mkuu
wa nchi hivyo ndiye mwenye uwezo wa kutoa ushauri na kutoa angalizo pale
inapohitajika, hasa anapoona kuna jambo lisilokuwa sawa, hivyo hakuna
haja ya kuendelea kusimama kupinga kile alichokielekeza nje ya Bunge.
"Tulioko
nje ya Bunge la Katiba hebu tuwaachie wajumbe. Rais kama msimamizi mkuu
atakoseaje kwa kutoa ushauri? Alichokifanya ni sahihi na kama kuna
tatizo, walioko nje ya Bunge warudi ndani ili wajadiliane kwa kina na
kumaliza tatizo," alisema.
Kauli ya CCM
Wakati
Rweyemamu akisema kazi hiyo ya mjadala wa katiba iachwe kwa wajumbe wa
chombo hicho cha kuandika Katiba, CCM ilisema jana kuwa kila mtu ana
haki ya kutoa maoni yake kuhusu mchakato huo na akaisifu CCT kwa kutumia
haki hiyo ya kikatiba.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema katika mchakato wa
kupatikana kwa katiba iliyo bora, kila mtu na kila kundi lina fursa ya
kutumia uhuru wa kikatiba kueleza na kutoa maoni yao, hivyo viongozi hao
wa CCT wametumia vyema uhuru huo.
Alisema
kwamba anaamini CCT haikufanya hivyo kimakosa kama ambavyo makundi
mengine, wakiwamo majaji, chama chake na hata watu binafsi wamekuwa
wakifanya, kwa kutoa mitazamo yao kuhusu aina ya muundo wa Serikali
wanayohitaji.
"Siyo hao tu, tunatarajia na wengine zaidi watatoa. Hiyo ni haki ya kimsingi iliyowekwa na Katiba.
Hatupo hapa kwa ajili ya
kushindanishwa, tunaamini Bunge lipo kwa mujibu wa sheria nalo
litaendelea kusimamia taratibu zake, hatuna sababu ya kumziba mtu
mdomo."
Chanzo: Mwananchi