MAMA SALMA KIKWETE AHIMIZA WANAFUNZI WA KIKE WA VYUO VYA UALIMU KUVAA MAVAZI YA HESHIMA
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/mama-salma-kikwete-ahimiza-wanafunzi-wa.html
Wanafunzi wa kike wa vyuo
vya ualimu nchini wametakiwa kuvaa mavazi nadhifu yanayoendana na
maadili ya kazi yao ili wanafunzi na jamii inayowazunguka ijifunze
kutoka kwao kwani wao ni kioo cha jamii.
Mwito
huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akiongea na baadhi ya wanafunzi wa kike wa chuo cha Ualimu Nachingwea
mara baada ya kumalizika kwa futari aliyoiandaa kwa ajili ya viongozi wa
wilaya iliyofanyika chuoni hapo.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa kupitia wilaya ya
Lindi mjini alisema siyo jambo jema kwa mwalimu kuvaa mavazi
yanayoonyesha sehemu za miili yao ikiwemo kata mikono, nguo zinazobana
na sketi fupi kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haiba ya ualimu.
Alisema,
“Sikuhizi kuna baadhi ya watu wanavaa mavazi yasiyoendana na utamaduni
wa mtanzania, nyinyi kama walimu ambao ni kioo cha jamii na
mnawafundisha wanafunzi madarasani msifanye hivyo kwa kufanya hivyo
watoto wataiga na kufikiria kuwa kuvaa mavazi hayo ni sawa”.
Mama
Kikwete pia aliwataka wanafunzi hao kutokuchagua maeneo ya kwenda
kufanya kazi pindi wamalizapo masomo yao na kupangiwa vituo vipya vya
kazi kwani kazi ya ualimu ni wito na kama mtu hakuipenda kazi hiyo basi
angechagua fani nyingine za kusoma.
“Baadhi
ya walimu wamekuwa wakikataa kwenda kufanya kazi katika maeneo ya
vijijini, na wengine wakipangiwa vituo vya mbali na mjini wanaogopa na
kudiriki hata kuacha kazi, kama ni hivyo kwa nini ulipoteza fedha na
muda wako kusomea ualimu?” , aliuliza Mama Kikwete.
MNEC
huyo alimalizia kwa kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na
kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi wawapo masomoni kitendo ambacho
kitawasaidia kumaliza masomo yao salama na kurudi nyumbani bila ya
kufukuzwa chuo kwa ajili ya kupata ujauzito.
Mama
Kikwete ambaye kitaaluma ni mwalimu miaka ya nyuma alisoma chuo cha
ualimu Nachingwea na juzi akiwa chuoni hapo alitembelea Bweni la
wasichana la Kawawa ambalo ndilo alilokuwa analala wakati akiwa
mwanafunzi wa chuo hicho.
CHANZO NI MATUKIO NA VIJANA