HII NDIO TAARIFA KAMILI KUHUSU YULE KIJANA ALIYECHOMWA NA SHOKA...IPITIE HAPA
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/hii-ndio-taarifa-kamili-kuhusu-yule.html
NI tukio la kutisha! Tukio hilo linadaiwa kutokea jijini Mwanza
ambapo mwanaume mmoja (jina halikupatikana mara moja) amepigwa shoka la
upande wa kushoto wa kchwa na kuzama ndani ikidaiwa ni sababu ya
kufumaniwa.
Picha za tukio hilo zilitumbukizwa mitandaoni na mtu anayedaiwa ni daktari aliyekuwa akimfanyia upasuaji mtuhumiwa huyo.
TAARIFA FUPI
Kwenye mitandao ya kijamii, picha hizo ziliambatana na maelezo mafupi sana kwa chini yakisomeka hivi:
“Baada ya madoctor (madaktari) wa Bugando kupambana kuokoa maisha ya
jamaa aliyefumaniwa huko Mwanza hatimaye wamefanikiwa kumtoa shoka
kichwani na hali yake bado mbaya, yuko ICU (chumba cha wagonjwa
mahututi) kwa uangalizi zaidi. Mke wa mtu sumu!”
MAZINGIRA YA PICHA
Kwenye baadhi ya picha, mwanaume huyo anaonekana ana nywele ndefu
kidogo na mustachi ulionona. Picha nyingine zinamuonea akiwa na kipara
nusu kichwa baada ya kunyolewa nywele ili madaktari waweze kumfanyia
upasuaji wa kulitoa shoka hilo lililozama ndani sana.
MAZINGIRA YA HOSPITALI
Baadhi ya watu waliochangia kwenye mitandao ya kijamii walisema tukio
hilo lilitokea nje ya Tanzania. Walisema ingekuwa Bongo lazima vyombo
vya habari vingeandika lakini hata hivyo, mazingira ya chumba cha
upasuaji alicholazwa mwanaume huyo yalionesha ni Tanzania.
Shoka likiwa limetolewa na madaktari wa upasuaji.
KWA NINI NI TANZANIA?
Ni Tanzania kwa sababu, picha zinamuonesha mwanaume huyo akiwa kwenye
kitanda cha chumba cha upasuaji akiwa amefunikwa shuka yenye maandishi
yanayosomeka kwa kifupi MSD.
MSD ni kifupi cha maneno Medical Stores Department (Bohari Kuu ya
Dawa). Mbali na kugawa dawa katika hospitali za serikali nchini, pia MSD
inatoa mashuka yenye nembo hiyo kwa ajli ya kujifunika wagonjwa
mahospitalini.
RPC ASHTUKA
Ili kupata ukweli wa madai hayo kwamba mwanaume huyo alikutwa na
mkasa huo mkoani Mwanza na kulazwa katika Hospitali ya Bugando, Risasi
Jumamosi liliingia kazini kufuatilia tukio hilo kwa kuzungumza na Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime na kumuuliza kama
ana ishu hiyo mezani kwake.
“Mh! Hivi nyiye mnajua kama mitandao siku hizi imezua balaa kubwa
sana? Hivi tukio kama hilo, mwanaume apigwe shoka mpaka kuzama kichwani,
alazwe Bugando Hospital mimi nisijue? “Hakuna kitu kama hicho. Hayo ni
mambo ya mitandao tu, sijui wametoa wapi? Halafu si umeona hata maelezo
hayajitoshelezi? Mimi mkoa wangu upo shwari kabisa mpaka hivi
ninavyoongea na wewe,” alisema Afande Fuime kwa sauti iliyoashiria
kushtuka.
DAKTARI BUGANDO AONGEA
Ili kuchimba zaidi, Risasi Jumamosi lilimtuma paparazi wake aliye
Mwanza, Mashaka Bartazal ambaye alikwenda hadi Hospitali ya Rufaa,
Bugando na kuzungumza na daktari mmoja anayefanya kazi kwenye kitengo
cha upasuaji ambapo alisema:
“Ni kweli tunapokea watu wenye matukio ya kutisha lakini mwanaume
aliyepigwa shoka mpaka likazama kichwani hatujampokea,” alisema daktari
huyo akiomba asitajwe jina gazetini kwani si msemaji wa hospitali hiyo.
TUKIO LAHAMISHIWA KAHAMA
Katika hali iliyozidi kuibua maswali, baadhi ya watu waliozungumza na
mwandishi wetu wa Mwanza walisema wamesikia mwanaume huyo alikumbwa na
balaa hilo wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
RISASI JUMAMOSI KAHAMA
Kwa sababu Kampuni ya Global Publishers inayochapisha magazeti pendwa
Bongo ina waandishi nchi nzima, ilimwagiza mwandishi wake aishiye
Kahama kulisaka tukio hilo na kutoa ripoti Makao Makuu, Bamaga-Mwenge
jijini Dar ambapo alifanya hivyo kwa kuomba apewe saa mbili tu
kufuatilia.
Baada ya saa mbili kupita, mwandishi wetu alitoa ripoti makao makuu
kwamba, hakuna mwanaume aliyelazwa kwenye hospitali yoyote ya wilayani
Kahama wala mkoa huo kwa kupigwa shoka la kichwani.
MASWALI YA MSINGI
Bado jamii imebaki na maswali kadhaa ya kujiuliza. Kwamba, kama ni
tukio la Tanzania, hiyo sehemu aliyolazwa mtu huyo hakuna jeshi la
polisi? Kwa sababu polisi ndiyo wanahusika na kupewa taarifa za matukio
kama hayo na kuyatangaza.