ALEJANDRO SABELLA KUAMUA HATIMA YA KUIFUNDISHA ARGENTINA YA LIONEL MESSI KABLA YA WIKI IJAYO!
https://samchardtz.blogspot.com/2014/07/alejandro-sabella-kuamua-hatima-ya.html
KOCHA wa Argentina, Alejandro Sabella amesema atafanya maamuzi ya hatima yake ya baadaye ndani ya wikiendi hii.
Kocha
huyo mwenye miaka 59 aliiongoza Argentina katika fainali ya kwanza
baada ya kupita miaka 24 nchini Brazil na kufungwa bao 1-0 dhidi ya
mabingwa Ujerumani.
Sabella
ameweka wazi kuwa atafikiria juu ya kazi yake na siku zijazo ataeleza
kila kitu, na kama anataka kuendelea na majukumu yake ataangailia kama
ataweza kuhimili mikikimikiki.
“Awali
ya yote, sijui mawazo ya AFA (chama cha soka cha Argentina) juu ya
hatima yangu, nahitaji kupumzika kwa siku chache. Sitapenda kushikilia
sana mambo kwasababu mimi ni mtu wa kuwajibika. Nitalitafakari hili
mwishoni mwa wiki hii na nitampigia simu (Rais wa AFA) Julio Grondona
ili tuonane,” aliviambia vituo vya luninga vya C5N na TyC Sports.
“Nitaendelea kuwa kocha kama nitaweza kutoa asilimia 100 ya nguvu zangu, kama ninavyowaomba wachezaji wangu”.

Sabella alisifu mchango wa Lionel Messi katika kampeni za kombe la dunia, akidai kuwa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano aliyoipata ilitokana na kiwango chake, na anadhani alijitolea kadiri awezavyo kuisaidia timu.
“Messi
ni mfano wa kile timu ilichofanya. Aliwaza mengi na sio moja, timu
ilikuwa juu yake, alitoa kabla ya kupokea”. Alisema Sabella.
“Alijitoa
mhanga na kuwa mchezaji bora wa dunia. Alikuwa msaada mkubwa kwetu
kufuzu hatua ya kwanza, na alielewa kuwa katika hatua nyingine za
mashindano tulitakiwa kubadili mfumo wetu wa uchezaji”.
“Tunajivunia
kuwa naye, tunamponggeza Messi kwasababu alijitolea kwa ajili ya timu.
Asante kwa kuwa Muargentina, asante kwa kuchagua kuichezea Argentina na
asante kwa kuwa tayari kucheza muda wote”.
Sabella
aliongeza kuwa bado hajatazama mechi ya fainali aliyofungwa na
Ujerumani kwa bao la dakika ya 113 la Mario Gotze, na amekiri kuwa timu
yake ilikuwa na nafasi ya kushinda.
“Sijaitazama tena mechi dhidi ya Ujerumani. Nahitaji kupumzika, tungeshinda mechi,” alisema.
“Nawapongeza Ujerumani kwasababu walikuwa ndio timu bora”.