Flatnews

MSAADA UNAHITAJIKA AOKOTWA NA MUUZA MBOGAMBOGA. MADAKTARI: MATIBABU YAKE NI INDIA.



Joseph Hamis Mruma akiwa na msamaria mwema anayemuuguza
Mwanafunzi (denti) wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya J.K.Nyerere, mkoani Kilimanjaro, Joseph Hamis Mruma (17), ameshindwa kuendelea na masomo tangu Januari, mwaka huu kutokana na maunivu makali ya donda la ajabu lililotokeza katika kisigino cha mguu wake wa kushoto.
Donda hilo amedumu nalo kwa miaka mitatu sasa na limemfanya akose raha.NI YATIMA
Joseph ni mtoto yatima, aliokotwa na msamaria mwema eneo la Himo mkoani Kilimanjaro akiwa anaokota vitu katika mapipa na mashimo ya takataka akidai hana mahala pa kuishi wala kupatia chakula baada ya wazazi wake kufariki.

MUUGUZAJI WAKE ANASEMAJE?
Muuguzaji wake anayemtunza aitwaye Conjesta Joseph Masawe anasema hivi:
“Mtoto huyu nilimuokota mtaani akiwa akitafuta chakula katika jalala maeneo ya Himo, mkoani Kilimanjaro. Wakati huo alikuwa na miaka kumi, alinieleza kuwa yupo katika mazingira hayo kutokana na tabu anayopata baada ya kufiwa na wazazi wake.
“Nilimuuliza kama ana ndugu yake alisema kwamba anaye mjomba wake ambaye alikuwa akimlea baada ya wazazi wake kufariki na aliamua kumtimua bila sababu za msingi.
“Alieleza kuwa awali alikuwa akiishi na wazazi wake jijini Dar es Saalaam maisha ya furaha.
Joseph Hamis Mruma akisumbuliwa na donda la ajabu mguuni kwake
VIFO VYA WAZAZI WAKE
“Mtoto huyo alinieleza kuwa wa kwanza kufariki ni baba yake na wakati huo alikuwa na umri wa miaka miwili na baada ya mwaka mmoja mama yake naye akafariki dunia, ndipo mjomba wake akamchukua na kuishi naye Himo, Moshi Vijijini.
“Mjomba wake huyo alimpeleka shule lakini anadai alikuwa akisoma kwa mateso makubwa kwani kuna wakati hata chakula alikuwa hapewi.
“Ingawa maisha yangu ni duni kwani nimekuwa nikiishi kwa kuuza mbogamboga lakini niliamua kumchukua na kukaa naye, nilimpeleka shule darasa la tatu alifanya vizuri katika masomo yake akawa amefaulu darasa la saba kwa maksi za juu na kujiunga na elimu ya sekondari Shule ya J.K  Nyerere lakini alizidiwa na maumivu makali ya mguu kutokana na kidonda alichonacho na kwa sasa yupo nyumbani.
“Joseph ameshindwa kwenda shule kutokana na maumivu kwani shule ipo mbali na tunakoishi naye anashindwa kutembea, anaelekea kukata tamaa kimasomo, ingawa wanafunzi wenzake na walimu wanapomtembelea anaumia sana kimawazo, nami napata naye taabu sana kwani nashindwa kwenda kufanya shughuli zangu kwa ajili yake.
Donda la ajabu linalomsumbua kijana Joseph
DONDA LILIVYOANZA
“Joseph alinieleza kuwa akiwa mdogo aliwahi kuungua moto lakini alipona, alishangaa kuona vijipele vikijitokeza sehemu aliyoungua hatimaye kikawa kidonda.
“Nimeshahangaika naye kimatibabu katika hospitali mbalimbali ikiwemo ya Mawenzi na KCMC bila mafanikio na kwa sasa nampa dawa ya kutuliza maumivu aina ya panadol lakini donda linazidi kuvimba na kutoa harufu kali kiasi kwamba kama siyo mtu mwenye moyo unaweza kumfukuza.
“Mimi hapa nina watoto wanne, nashindwa hata jinsi ya kuwahudumia, mume wangu naye hana kazi anategemea kilimo cha mkono ambacho hakina msaada mkubwa, madaktari walisema kwamba huenda ugonjwa huu unaweza ukawa kansa lakini unaweza kutibiwa Hospitali ya Ocean Road Dar au nchini India lakini sina uwezo wa kumpeleka huko.
WATU WAMSUSA
“Kutokana na kidonda kuzidi kukua na kutoa harufu kali baadhi ya watu wameanza kutususa kwa kutofika hapa nyumbani, lakini mimi Joseph nitamuuguza hadi Mungu atakavyoamua.
“Naamini Mungu aliamua kunipa mtoto huyu. Watanzania nawaombeni mnisaidie matibabu yake na fedha za matumizi kwa kupitia namba za simu 0767 604113 au 0754 853146.”

Post a Comment

emo-but-icon

item