LUGAZIYA ANA HOJA JUU YA KURUDISHWA KWA WAMBURA, LAKINI WANACHAMA WA SIMBA NA VIONGOZI WAO WATAJILAUMU KWA UZEMBE
https://samchardtz.blogspot.com/2014/06/lugaziya-ana-hoja-juu-ya-kurudishwa-kwa.html
Mwenyekiti
wa kamati ya Rufani ya TFF, Wakili Julius Mutabazi Lugaziya (kushoto)
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jana kutangaza kutengua
maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya Simba kuliengua jina la Wambura.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Juni 12, 2014, saa 11:14 jioni
BAADA ya kamati ya rufani kutengua maamuzi ya
kamati ya uchaguzi wa Simba sc kuhusu kuliengua jina la Mgombea Urais, Michael
Richard Wambura na kumrudisha katika kinyang`anyiro hicho mengi yanazungumzwa
juu ya uhalali wa maamuzi hayo.
Ulikuwa mlolongo mrefu mpaka kufikia maamuzi.
Kamati ya rufani ilikaa kwa siku mbili, lakini ngoma ilikuwa nzito mpaka
walipoamua kupiga kura ambapo Wambura alipata kura 3 kati ya 5 za wajumbe wa
kamati.
Baadhi ya watu wanaeleza kuwa kamati ya Rufani ya
TFF imembeba Wambura na wengine wanahoji kwanini maamuzi hayo yamefikiwa kwa
njia ya kura wakati kanuni na sheria zipo wazi.
Mwenyekiti wa kamati ya Rufani, Wakili Julius
Mutabazi Lugaziya alifafanua jana kuwa kwa kawaida maamuzi ya vikao vya rufani,
inapofikia wajumbe wanashindwa kufikia muafa, maamuzi yanaamuriwa kwa kura.
Jana wakati Wakili Lugaziya akiongea na waandishi
wa habari kutangaza maamuzi ya kamati yake, alizungumza mambo mengi ambayo
baadhi yake niliyaandika kwa kirefu.
Michael Richard Wambura anaungwa mkono na wanachama wengi wa Simba sc
Ikumbukwe sheria za mpira wa miguu ziko wazi
kabisa. Ni dhambi kubwa kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za
kawaida. Jambo hili lilifanywa na Wambura miaka ya nyuma. Kwa sheria ilivyo,
mtu anayefanya haya anajiondoa katika masuala ya mpira wa miguu.
Moja ya mapingamizi aliyowekewa Wambura, suala la kuipeleka
Simba Sports Club mahakamani katika kesi Namba 100/2010 iliyofunguliwa katika
mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam, Kinyume na Ibara ya 11 (1) (e),
(2), 12(3), na 55 ya Katiba ya Simba Sports Club ya Mwaka 2010 lilikuwa na
nguvu na wengi waliokuwa wanaamini ataondolewa moja kwa moja katika uchaguzi wa
Simba waliegemea sehemu hii.
Pia kamati ya uchaguzi ya Simba sc, chini ya
mwanasheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ilieleza kuwa sababu nyingine ya kumuengua
Wambura ni kwamba, mwekewa Pingamizi (Wambura) alisimamishwa Uanachama na
Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club iliyokutana tarehe 5 Mei 2010 na barua
ya tarehe 6 Mei 2010, (Kumb. Na. SSC/MMKT/163/VOL.40/11) na hivyo basi
anapoteza haki za kuwa mwanachama wa Simba Sports Club.
Sababu hizi mbili ndio zilikuwa na nguvu katika
maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya Simba sc kuliengua jina la Wambura.
Baada ya maamuzi hayo, Wambura alikata rufani
kupinga maamuzi akiweka sababu 14 na hapo jana ndipo majibu ya rufani yake
yalitoka na kushinda.
Wambura aliipekea Simba mahakamani, hilo halina
ubishi. Wambura alisimamishwa uanachama, hilo pia linafahamika. Lakini je,
baada ya kusimamishwa, utekelezaji wa adhabu hiyo ulikuwaje?, hapo ndipo tatizo
lilipoanzia.
Katiba ya Simba iko wazi na inaeleza kuwa mtu
ambaye amepoteza uanachama, hatakiwa kushiriki shughuli yoyote ya klabu. Haya
yameandikwa kwenye katiba ambayo wanasimba wanayo na wanaisoma kila siku.
Walimsimamisha uanachama, lakini wakamuacha
aendelee kushiriki kazi za Simba ikiwemo mikutano mikuu na ya dharuta, pamoja na vikao vya maamuzi ya klabu ya Simba.
Kamati ya rufani ilieleza kuwa Wambura tangu
asimamishwe, amekuwa akishiriki shughuli za Simba kama mwanachama halali.
Wakili Lugaziya alisema katika mikutano minne
iliyofanyika nyuma Wambura alishiriki akiwa mwanachama halali na kubwa zaidi mpaka
leo ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu ya Simba.
Wambura alishiriki katika mkutano wa mabadiliko ya
katiba, pia alihusika kuiteua kamati ya uchaguzi ambayo baadaye ilimuengua.
Lugaziya alifafanua kuwa kinachoonekana hapa ni
kwamba, baada ya Simba kumsimamisha Wambura, haikuwahi kumchukulia kama
amesimamishwa kwasababu amekuwa akishiriki shughuli za Simba.
“Katiba inasema mtu anayepoteza uanachama,
anapoteza haki ya kulipa ada, kushiriki mikutano na vikao vya maamuzi na
kupoteza haki ya kuteuliwa katika vyombo mbalimbali vya Simba sc”.
“Wambura tangu atangazwe kusimamishwa amekuwa
akilipa ada na michango yote ya uanachama na michango ya mawazo kwa kipindi
chote, isipokuwa kunapokuwa na uchaguzi”. Alisema Wakili Lugaziya.
Aliendelea kwa kusema kuwa pili; Wambura ameshiriki mikutano yote mikuu na
ya dharura kwa kipindi chote. Ikumbukwe kuwa ni sharti la msingi la katiba kuwa
mwanachama halali yaani ambaye ni hai kwa maana ya yule aliyelipa ada yake na
hajasimamishwa ndiyo anatakiwa kushiriki tu.
“Uongozi wa klabu ya Simba ulikuwa na mamlaka ya
kuhoji mahudhurio ya mwanachama asiye halali, hilo halijawahi kufanyika kwa
Wambura”.
“Tatu; Mrufani amewahi kuteuliwa na kushiriki kuandaa mpango mkakati wa Simba sc
ulioshirikisha chuo kikuu huria. Kamati hiyo ilishirikisha wajumbe ambao sio
wanachama wa Simba sc, hata hivyo kamati haikushawishika kuwa mrufani aliitwa
kama mtu `baki`, bali aliona kuwa bwana Wambura aliitwa kwa kuzingatia nafasi
yake ndani ya samba sc.”
“Kubwa zaidi Mrufani mpaka hivi sasa ni mjumbe wa
kamati ya utendaji. Ameshiriki kufanya maamuzi mengi ikiwemo kuchagua kamati ya
uchaguzi yenyewe pamoja na mkutano wa katiba. Mwanachama asiye na haki
anawezaje kufanya mambo haya yote na wenzake wanaangalia?”. Alihoji Wakili
Lugaziya.
“Suala la uanachama wa mrufani (Wambura) halijawahi
kuhojiwa ama kwa mujibu wa mrufani mwenyewe au mwanachama mwingine yeyote wa
Simba sc. Jambo alilosimamishia mrufani lilikuwa la dharura. Kwa mujibu wa
katiba ibara ya 12, suala hilo lilitakiwa kuletwa katika mkutano mkuu unaofuata”.
Siku Wambura alipochukua fomu ya kugombea Urais Simba sc
“Mrufani alisimamishwa tarehe 5 mei mwaka 2010,
mkutano mkuu wa Simba sc uliofuata ulifanyika siku nne baadaye, yaani tarehe 9,
5, 2010. Hoja ya kusimamishwa ikiwa bado inatokota wakati ule mkutano
ulipofanyika, hata hivyo hoja hiyo haikuwasilishwa kwenye mkutano ule na mikutano
mingine mingi iliyofuata. Kwa kushindwa kufanya hivyo, kamati ya utendaji na si
mrufani, ilishindwa kutekeleza matakwa ya katiba na mbaya zaidi badala ya
kuchukua hatua zilioainishwa ikawa inampa fursa mbalimbali kutoa michango yake
Simba sc”.
“Kwa mujibu wa katiba ya Simba, kamati ya utendaji
inakutana mara moja kila baada ya miezi mitatu, kwa maana hiyo kwa mujibu wa
katiba ya Simba ibara ya 31 kifungu cha kwanza, kamati ya utendaji inakutana
mara nne kwa mwaka”.
“Tangu mei 2010 ukitoa miezi mitatu iliyokuwa
imepita, kamati ya utendaji ya Simba inatakiwa kuwa imekaa vikao vya kikatiba
20. Kwa mujibu wa katiba hiyo ibara ya 20, mkutano mkuu unafanyika mara moja
kwa kila mwaka, tangu wakati huo imefanyika mikutano mikuu ya kawaida minne,
mrufani (Wambura) ameshiriki mikutano yote hiyo”.
“Kwahiyo kamati ya rufani imejielekeza kwenye
kanuni zinazozuia mtu au chombo kukanusha mambo iliyoyafanya kwa maana ya
kwamba kwa kutangaza kuondoa haki za mwanachama, lakini hapo hapo ikawa inampa
haki na kushiriki kama mwanachama, ni kama vile yenyewe iliondoa zuizi lake na
haina nafasi ya kumkanusha mwomba rufani”
“Kamati ilijielekeza katika athari ya kuutunza
uamuzi wa kamati ya uchaguzi wa Simba. Endapo chombo au kikao chochote
kimefanya maamuzi na baadhi ya wajumbe walioshiriki katika chombo kile
hawakupaswa kushiriki katika uamuzi, uamuzi uliopitishwa unakosa nguvu za
kisheria. Kama ndivyo kamati ikajiuliza, je, vikao vilivyoandaa katiba ya Simba
na kuipitisha ambayo mrufani (Wambura)alishiriki vina athari zipi kuhusu
uhalali wa katiba yenyewe ya Simba.
“Pili; Je, vikao vilivyoteua kamati ya uchaguzi ya
Simba ambavyo mrufani alishiriki huku akiwa hana hadhi ya kushiriki vina
maanisha nini katika uhalali wa kamati wenyewe.”
“Kama mtu batili ameshiriki kupitisha maamuzi,
yale maamuzi nayo yanakuwa batili. Kwa maana hiyo kama tutaendelea kutunza
uamuzi wa kamati ya uchaguzi ambayo na yenyewe ni batili. kwa maana hii, katiba ya Simba haipo kihalali,
Je, athari hizo zingeleta matokeo gani?”.
“Lakini kamati ilishasema huko nyuma kuwa Simba
leo hii haiwezi kukataa kwamba ilimchukuliwa Wambura kama mwanachama wa kawaida
wa Simba. Kwahiyo suala la ubatilifu linakuwa halipo”.
“Kamati inapenda ieleweke kwamba uamuzi huu hauna
maana na wala usichukuliwe kwa maana yoyote ile kwamba una nia ya kufungua njia
kwa wanachama wa klabu kupeleka masuala ya mpira kwenye mahakama hizi za
kawaida”.
“Maana ya maamuzi haya ni kwamba, uamuzi huu unalenga kuzihimiza klabu
mwanachama wa TFF kuzingatia taratibu walijiwekea kwa uweledi badala ya kutumia
taratibu hizo kwa manufaa hasi na kwa manufaa ya wachache kwenye mpira wa miguu”.
“Kwasababu tulizozitaja na tutakazofafanua zaidi
kwenye waraka tutakaoutoa, kamati ya rufani ya uchaguzi ya TFF inabatilisha uamuzi
wa kamati ya uchaguzi ya Simba sc. Michael Richard Wambura anastahili kuwa
mgombea na kuondolewa kwake kunatenguliwa”.
Haya ndiyo yalikuwa maelezo ya mwenyekiti wa
kamati ya rufani ya TFF, Wakili Julius Mutabazi Lugaziya hapo jana.
Ismail Aden Rage (kulia), uongozi wake ulishindwa kusimamia taratibu za katiba kuhusu suala la Michael Wambura
Ukiyafuatilia kwa umakini maelezo na sababu walizotumia
kumrudisha Wambura, unagundua kuwa kuna usahihi na hoja ndani yake.
Wambura alikuwa na makosa, lakini kuna upande
mmoja ulishindwa kufanya kazi yake kwa maana ya uongozi wa klabu ya Simba.
Miaka ya nyuma, baadhi ya wanachama walipiga
kelele kwe mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage juu ya uhalali wa Wambura na
wengine walikuja juu zaidi alipoteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji.
Baadhi yao walihitaji ufafanuzi juu ya uteuzi ule,
lakini wakati anateuliwa, tayari alikuwa ameifanyia Simba mambo mengi kwa
nafasi ya uanachama.
Nadhani hata wale waliokuwa wanafuatilia suala
hilo ilifika wakati wakalipotezea kwasababu ni utamaduni wa watanzania wengi
kuwaka kwa muda na kuachana na jambo muhimu.
Mambo mengi yanatokea katika jamii ya watanzania,
watu wanaongea, lakini inafika muda wanaacha na kuendelea na maisha mengine.
Hivi ndivyo suala la Wambura lilivyoshughulikiwa katika klabu ya Simba.
Wambura ni mtu maarufu, anafahamika na watu wengi,
hivyo akienda kwenye mkutano ni rahisi kutambulika. Angekuwa mtu wa kawaida,
labda tungesema hakuonekana, lakini bado kulikuwa na daftari la mahudhurio.
Wanachama wa Simba walikuwa wanamuona Wambura
kwenye mikutano yao na akifanya kazi muhimu za klabu, lakini hawakuwahi kuhoji
kwa umakini na kuhakikisha wanapata majibu.
Kwa bahati mbaya baada ya uongozi wa Rage
kushindwa kuwajibu kwa wakati, inawezekana wakaona sio `ishu`. Lakini madhara
yake yamekuwa makubwa.
Kama kweli kamati ya Lugaziya ingetunza maamuzi ya
kamati ya uchaguzi ya Simba, hakika mambo yangekuwa mengine. Maana yake uhalali
wa katiba ungehojiwa na kamati ya uchaguzi yenyewe.
Fikiria kama wangebatilisha kila kitu, nini
kingetokea kwa wakati huu. Ingeleta athari kubwa mno. Binafsi naomba uamuzi wa
kamati ya rufani uheshimike.
Yanazungumzwa mengi kwasababu ni haki ya mtu
kueleza mawazo yake, lakini tuwe wepesi wa kukubali makosa na kuanza upya.
Simba tayari walishafanya makosa siku za nyuma,
Wambura amekuwa mjanja zaidi yao.. Lazima wanachama wakubaliane na hilo.
Hakuna jinsi kwa sababu zilizoelezwa, cha msingi
muacheni Wambura aende kwenye uchaguzi kupambana na Evans Aveva na Andrew Tupa.
Kama akishindwa basi, kama atashinda isiwe kigezo
cha kugombana. Kura ndio mwamuzi wa yote. Wingi wa kura utampa urais Wambura au
uchache wa kura utamnyima Urais.
Wanachama wa Simba, tulieni na achaneni na maneno
yasiyokuwa na msingi kwa muda huu, nendeni mkafanye maamuzi juni 29 mwaka huu.
Nawatakia amani wanasimba wote wakati huu muhimu
wa uchaguzi.