HATIMA YA MICHAEL WAMBURA KUWANIA KUMRITHI ADEN RAGE SIMBA SC NI JUNI 9
https://samchardtz.blogspot.com/2014/06/hatima-ya-michael-wambura-kuwania.html
Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
inakaa Jumatatu (Juni 9 mwaka huu) kusikiliza rufani moja inayopinga
uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba.
Michael
Wambura amewasilisha rufani yake TFF akipinga uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi ya Simba iliyomwengua katika kinyang’anyiro cha kuwania urais
katika uchaguzi wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi
huu.
Kamati
hiyo inayoongozwa na Wakili Julius Lugaziya itakutana saa 5 asubuhi
kwenye hoteli ya Courtyard iliyopo Upanga, jijini Dar es Salaam.
WAKATI HUO HUO NYOTA WAWILI COPA WAENDA BRAZIL
Wachezaji
wawili waliochaguliwa kwenda kwenye kambi ya Copa Coca-Cola ya Dunia
nchini Brazil wamekabidhiwa bendera tayari kwa safari hiyo inayofanyika
leo (Juni 4 mwaka huu).
Hafla
ya kukabidhi bendera hiyo kwa Ali Shabani Mabuyu na Juma Yusuf
imefanyika leo katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yassoda ndiye alikabidhi bendera.
Wakati
Mabuyu kutoka Ilala alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Copa Coca-Cola
kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 kwa mwaka 2013/2014, Yusuf
kutoka Zanzibar ndiye aliyeibuka mfungaji bora katika michuano hiyo.
Wachezaji
hao watakuwa katika kambi hiyo itakayokuwa katika Jiji la Sao Paulo kwa
siku kumi ambapo watafundishwa masuala mbalimbali ya mpira wa miguu.
Pia watashuhudia mechi ya ufunguzi ya Fainali za Kombe la Dunia katika
ya wenyeji Brazil na Croatia itakayochezwa Juni 12 mwaka huu.