MKUTANO WA MALINZI NA KLABU ZA VPL WAAMUA WACHEZAJI WATANO WA KIGENI
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/mkutano-wa-malinzi-na-klabu-za-vpl.html
Na Boniface Wambura, Dar es saalam
Mkutano wa Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenyeviti wa klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) kupata maoni yao juu ya changamoto zilizojitokeza katika ligi
hiyo umefanyika juzi (Mei 11 mwaka huu).
Klabu za VPL zilizohudhuria mkutano
huo ni Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa
Sugar, Polisi Morogoro, Ndanda FC, Ruvu Shooting, Stand United na Tanzania
Prisons.
Simba na Yanga hazikuhudhuria
mkutano huo, na wala klabu hizo hazikutoa udhuru wowote wa kutokuwepo.
Maazimio ya mkutano huo ni kuwa kwa
misimu mitatu ijayo kuanzia msimu wa 2014/2015 klabu zimekubaliana ziruhusiwe
kusajili wachezaji watano wa kigeni. Kamati ya Utendaji ya TFF itatoa uamuzi wa
mwisho juu ya suala hilo katika kikao chake kijacho.
Pia klabu hizo zimekubali timu zao
za U20 kuanzia msimu ujao zicheze ligi ya mkondo mmoja. Hata hivyo, utekelezaji
wa hilo utategemea na upatikanaji wa mdhamini wa ligi hiyo ambapo TFF inafanya
jitihada za kumpata mdhamini huyo.
Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya
Mpira wa Miguu wa Wanawake, Lina Kessy amezishauri klabu za VPL kuanzisha timu
za wanawake, ambapo klabu hizo zimesema zitaufanyia kazi ushauri huo.