Mbowe: Mrema,Cheyo nje Baraza la Mawaziri
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/mbowe-mremacheyo-nje-baraza-la-mawaziri.html
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, amesema ni vyama vitatu pekee vya upinzani ndivyo
atakavyoviingiza kuunda baraza jipya la mawaziri kivuli.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana alipozungumza
na NIPASHE lililotaka kujua muda wa kuunda baraza hilo na idadi ya vyama
atakavyoviingiza baada ya kulivunja baraza la sasa wiki hii.
Alivitaja vyama hivyo kuwa ni Chadema, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Kwa mujibu wa Mbowe, sababu kubwa ya
kuviingiza vyama hivyo kwenye baraza hilo ni kutokana na msimamo wao wa
kushiriki vyema katika mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya na
kujadili Rasimu ya Katiba sura ya kwanza na ya sita ya kwenye Mkutano wa
Bunge Maalum la Katiba ulioahirishwa Aprili 25, mwaka huu hadi ngwe ya
pili kuanzia Agosti 5, mwaka huu.
“Ni vyama vitatu tu ambavyo vipo kikamilifu
katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), yaani Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi. Mrema (Augustine- TLP) yupo CCM na Cheyo (John-UDP) yupo
nusu nusu, hivyo ni vyama hivyo vitatu tu ambavyo vipo Ukawa ndivyo
vitakavyounda hili baraza jipya la mawaziri kivuli,” alifafanua Mbowe.
Kuhusu muda wa kuunda baraza hilo,
Mbowe, alisema, yeye ndiye mwenye kuliunda na kwamba baada ya kulivunja
la sasa, atatangaza wakati wa kupatikana kwa baraza jipya kwa kuwa la
sasa bado lipo.
Kabla ya Mbowe ambaye ni mjumbe wa
Bunge la Katiba na Mbunge wa Jimbo la Hai kutangaza maamuzi ya kufanya
mabadiliko hayo, awali baraza hilo lilikuwa likiundwa na wabunge wa
Chadema pekee. Baraza hilo liliundwa mwaka 2011 baada ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2010 na kuwashirikisha Chadema peke yao.
Mbowe alipounda baraza hilo alisema
kuwa asingevihusisha vyama vingine vya upinzani kwa kuwa wakati huo
havikuwa na mwafaka wala maslahi yanayofanana.
Hata hivyo, aliahidi kuwa angewateua
wabunge wa vyama vingine baada ya kuridhika kwamba kambi ya upinzani ina
mwafaka na msimamo wa pamoja katika masuala mbalimbali muhimu kwa nchi.
Mbowe alitangaza uamuzi wa kuundwa
baraza jipya kivuli litakalovishirikisha vyama vingine Aprili 30, mwaka
huu baada ya yeye pamoja na wajumbe wenzake wanaounda Ukawa, kufanya
mkutano wa pamoja kwa lengo la kusisitiza msimamo wa muundo wa serikali
tatu na kupinga wa serikali mbili unaoungwa mkono na Chama cha Mapinduzi
(CCM).
Viongozi wote wa kitaifa wa vyama
hivyo vinavyounda Ukawa walihudhuria Mbowe alisema katika mkutano huo
kuwa kulivunja baraza la sasa la mawaziri kivuli ili kuwaingiza pia
wajumbe kutoka vyama vingine vya upinzani na kwamba ushirika uliopo
baina vyama vyao hivyo hautaishia tu katika kudai katiba ya wananchi,
bali utaendelea hadi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kutokana na hilo, Mbowe, aliongeza
kuwa wiki hii anatarajia kuvunja baraza la mawaziri kivuli na kuliunda
upya ili kuhakikisha Ukawa inasambaa siyo katika Bunge Maalum la Katiba
tu, bali katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika
Uchaguzi Mkuu mwakani.
MREMA AZUNGUMZA
Alipoulizwa jana na NIPASHE kuhusiana
na kauli ya Mbowe, Mrema alihoji kwamba wanaposema yeye ni CCM kwa nini
hawazungumzii ndoa ya CCM na CUF ambao waliunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar.
“Mbona hiyo ndoa hawaisemi, badala
yake wananisema mimi. Upinzani wa kusaliti nchi, sitaufanya na yale ya
kubomoa nchi sitayakubali,” alisema.
“Nimewahi kushika Uwaziri wa Mambo ya
Ndani, Kazi na Vijana pamoja na unaibu Waziri Mkuu hivyo kuwa waziri
kivuli ni maigizo,” alisema Mrema.
Mrema pia alihoji ni kwanini baadhi
ya viongozi wa vyama vya siasa wanamuita kuwa ni CCM wakati wao
wanapoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM
hawakatai uteuzi huo.
Cheyo alipotafutwa jana simu yake ilikuwa inaita bila majibu.
Mrema ni Mbunge pekee anayetoka Tanzania Labour (TLP) na Cheyo ni Mbunge pekee kutoka United Democratic (UDP).