Flatnews

KAMA HAYA YATAFANYIKA, TAIFA STARS YA MART NOOIJ ITAITANDIKA ZIMBABWE TAIFA


DSC_4575
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa stars chini ya kocha mkuu, Mholanzi, Mart Nooij inatarajia kucheza mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) jumapili mei 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taifa Stars wataingia katika mechi hii baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili za kirafiki. 
Aprili 26 mwaka huu walicheza na Burundi ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kufungwa mabao 3-0. Lakiki kikosi cha stars kilisheheni wachezaji kutoka katika mpango wa maboresho ya Taifa Stars. 
Mei 4 mwaka huu kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Stars ilicheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya Malawi na kulazimisha suluhu pacha ya bila kufungana.
Mechi dhidi ya Burundi, tatizo kubwa kwa Taifa stars lililkuwa kukosa uzoefu kwa wachezaji wapya.  Vijana waliotokea katika mpango wa maboresho walikuwa waoga, hawakujiamini hata kidogo na hawakuwa na nidhamu ya mchezo.
Burundi walikuwa na kazi ndogo ya kuwafunga Stars, huku wachezaji wazoefu na mechi za kimataifa kama  Deo Munish, Saimon Msuva, Frank Domayo, Ramadhan Singano `Messi`  wakijaribu kuokoa jahazi bila mafanikio.
Akina Omari Nyenye kutoka maboresho ya Stars walichezea nafasi za wazi na kuwaruhusu Burundi kuwaliza watanzania siku muhimu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo jana zilienea taarifa kuwa wachezaji watano wa Taifa stars akiwemo Nyenye, wametemwa. Wengine wanaosemekana kuachwa na kocha Nooij ni mshambuliaji Hussein Javu, beki Hassan Mwasapili, wengine ni Ammanuel Namwando na Michael Pius.
Bila shaka sababu ya kuwaacha wachezaji hawa ni ya kimpira na mwalimu Nooij ndiye mtaalam anayefahamu vizuri kwanini amewatema.
Katika mchezo dhidi ya Malawi, Taifa stars iliwatumia wachezaji waliozoeleka na wenye uzoefu kama Deogratius Munish `Dida`, Erasto Nyoni, Oscar Joshua, Nadir Haroub `Canavaro`, Agrey Morris, Frank Domayo, Jonas Mkude, Saimon Msuva, Ramadhan Singano, Harun Chanongo, Amri Kiemba, John Bocco na wengineo.
Lengo la Nooij lilikuwa ni kutafuta wachezaji wa kuwatumia katika michezo ya kimataifa ya mashindano kuanzia wa jumapili dhidi ya Zimbabwe.
Katika mechi hii, Stars ilicheza vizuri hasa safu ya ulinzi chini ya maaskari wawili wa kati, Nadir Haroub ` Canavaro` na Agrey  Morris.
Wanaume hawa kwa kushirikiana na mabeki wao wa pembeni, Erasto Nyoni na Oscar Joshua, waliifanya ngome ya Stars kuwa ngumu kupitika.
Hata hivyo bado kulikuwa na makosa ya kimchezo ambayo mwalimu atakuwa ameyafanyia kazi.
Pia katika safu ya Kiungo vijana walicheza vizuri na kupeleka mipira mingi mbele, lakini tatizo kubwa lilibaki katika safu ya ushambuliaji.
John Raphael Bocco na wenzake walikosa nafasi nyingi za kufunga na hata baada ya mechi Kocha Nooij aliwalaumu washambuliaji wake kwa kukosa umakini, na akaahidi kufanyia kazi tatizo hilo.
 
Sasa Stars inakutana na Zimbabwe iliyopiga hatua katika soka. Nadhani kila mtu anaikumbuka Zimbabwe iliyoshiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN mwezi februari mwaka huu nchini Afrika kusini.
Zimbabwe walikuwa hatari mno  na kuidhihirishia dunia kuwa mpira umeanza kuhamia  katika ardhi yao. Zimbabwe wanacheza kwa kujituma na kwa asilimia kubwa wachezaji wao wanajitolea kwa ajili ya timu.
Moja kati ya matatizo ya wachezaji wa Tanzania ni kushindwa kujitolea kwa moyo wote.
 Mpira una kanuni  kuwa kama timu yako imezidiwa, na mchezaji unafahamu kuwa kwa jitihada zako binafsi unaweza kuokoa jahazi, basi cheza kwa faida ya timu na jitolea kwa nguvu zote.
Lakini kwa wachezaji wetu wanaonekana kucheza kawaida tu bila kutambua wapo wakati gani na timu inahitaji nini.
Mechi ya jumapili ni ngumu kwa Taifa stars kutokana na maendeleo makubwa waliyopata Zimbabwe.
Wana watu kule mbele  kama Knowledge Musoma, Kingston Nkhatha. Hawa jamaa kama watakuwepo jumapili, ni shughuli pevu kwa mabeki wa Stars.
Hata hivyo masikitiko makubwa kwa Taifa stars ni kuwakosa wachezaji wawili wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kwa vyovyote vile, wachezaji hawa walikuwa muhimu katika mchezo wa jumapili kutokana na uzoefu wao na kiwango walichonacho kwa sasa, lakini kwa kuwa yameshatokea haya, basi ni kuwaangalia waliopo sasa.
 

Ili Taifa Stars washinde mechi ya jumapili, haya ni baadhi ya mambo machache kati ya mengi wanayotakiwa kufanya;
Mosi; watulize akili kujiandaa na mchezo huo. Kwa muda sasa wamekuwepo eneo tulivu la Tukuyu kwa maandalizi yao. Wamebakiza siku chache kufikia jumapili, hivyo lazima akili yao ielekee katika mechi hii na kuachana na mambo mengine.
Pili; watambue kuwa wapo uwanja wa nyumbani. Siku hizi mpira umebadilika sana, hata ukiwa nyumbani unachezea kichapo. Lakini kuna faida ya kucheza nyumbani. Unakuwa na faida ya uwanja wako, mashabiki wako, hivyo unakuwa na sapoti ya kila kitu hata mazingira pia.
Hata ulaya, timu nyingi huwa zinamaliza biashara nyumbani. Kwahiyo stars watambue kuwa watakuwa nyumbani, lazima wacheze kwa malengo ya kutafuta ushindi.
Kuwafunga Zimbabwe zaidi ya mabao matatu itakuwa faida kubwa kwasababu kuwafunga Harare itakuwa ngumu sana. Vijana watumie vizuri nafasi ya nyumbani.
Tatu; wasicheze na majukwaa. Taifa stars siku za karibuni imekuwa na hali mbaya kwa mashabiki. Mara kadhaa huwa wanaizomea inapocheza. Hivyo wachezaji wasijali kama itatokea hali hii, waingie kufanya kazi yao na kutafuta kushangiliwa kwa soka zuri. Kama watafunga hakuna atakayewazomea. Na kwakuwa wanajua watanzania wanawazomea, basi watafute namna ya kuwafanya wawashangilie.
Uzelendo kwa mashabiki wa kibongo bado sana, hivyo vijana wawalazimishe kuwapa sapoiti kwa kucheza vizuri.
Nne;Wapunguze makosa sehemu ya kiungo na ulinzi. Safu ya Canavaro, Morris ilikuwa imara dhidi ya Malawi. Hawakupitisha mipira ya hatari kirahisi, lakini kulikuwa na makosa madogo madogo ambayo kama Malawi wangekuwa na watu makini basi wangeifunga Stars. Kikubwa watambue kuwa kuna Musoma ambaye hafanyi makosa anapota nafasi. 
Viungo wajipange kuziba eneo la kati vizuri ili kuwasaidia mabeki kucheza kwa kutulia. Kama Zimbabwe watashambulia kutokea pembeni, basi akina Oscar na Nyoni wajiandae kukabiliana kwa nguvu ili kuwarahisishia kazi mabeki wa kati.
Tano; Safu ya ushambuliaji ya Taifa stars itatakiwa kutumia vizuri nafasi watakazopata. Kama watazichezea nafasi kama kule Mbeya dhidi ya Malawi, basi kusonga mbele itakuwa ndoto. Bocco na wenzake lazima watambue kuwa wapo nyumbani na timu inahitaji magoli ili kujiweka nafasi nzuri.
Timu itatakiwa kushambulia kwa kasi na kwa muda wote. Lakini kujilinda itakuwa muhimu pia. Stars waje kwa mtazamo wa kumiliki mpira na kucheza pasi murua,lakini kulinda eneo la iyakuwa muhimu zaidi na kushambulia kwa kasi kubwa. 
Sita; mashabiki wanatakiwa kujitokeza na kuwashangilia wachezaji wa Taifa stars. Katika mpira mashabiki ni muhimu. Ni sawa na mchezaji wa 12. Hivyo watanzania kwa moyo mmoja wajitokezea na kuwashangilia stars. Wachezaji wanajiona wana thamani kubwa wanaposikia amsha amsha za mashabiki uwanjani.
Zipo sababu nyingi za kuifanya Taifa stars ipate matokeo jumapili ya mei 18, lakini hizo ni chache miongoni mwa sababu nyingi. Mtandao huu utaendelea kukupatia sababu nyingine kadri tunavyokaribia siku ya mechi. 
Taifa Stars watanzania tupo nyuma yenu. Fanyeni kazi yenu kwa faida ya Taifa. 
Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini mkoani Mbeya itarejea Dar es Salaam kesho (Mei 14 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo.

Post a Comment

emo-but-icon

item