AUA MKE WAKE MJAMZITO KISA MVIVU KWENDA SHAMBANI
https://samchardtz.blogspot.com/2014/05/aua-mke-wake-mjamzito-kisa-mvivu-kwenda.html
Agatha Isack (19) amekufa kwa kipigo kutoka
kwa mumewe akisaidiwa na mwanamke anayeaminika kuwa hawara yake,
akimtuhumu kuwa mvivu wa kulima shambani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi,
Dhahiri Kidavashari alithibitisha kifo hicho na kuongeza kuwa mama huyo
mjamzito ambaye ni mkazi wa kijiji cha Manga, Kata ya Kasokola wilayani
Mlele alifikwa na umauti akikimbizwa katika zahanati kijijini hapo kwa
matibabu na mumewe huyo Vitus Mlengo (23).
Akielezea mkasa huo unaodaiwa kutokea juzi
saa sita mchana nyumbani kwa wanandoa hao kijijini humo, Kamanda
Kidavashari alisema awali baada ya kipigo mwanamke huyo alikwenda katika
zahanati iliyopo kijijini humo kwa uchunguzi zaidi na matibabu.
Kabla ya kufika hospitalini alikwenda kwa
mama yake mdogo aitwae Anastazia Charles na kumsimulia jinsi alivyopigwa
na mumewe akishirikiana na Faustina Matheo (31) ambaye anadaiwa kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na Mlengo.
“Baada ya kutibiwa Agatha alipitia nyumbani
kwa bibi yake kijijini humo na kumweleza jinsi alivyopigwa na mumewe
pia alimfahamisha bibi yake kuwa mumewe alimuonya asirudi nyumbani bila
mboga hivyo bibi yake huyo alimpatia mboga naye akarejea kwake,“
alibainisha Kamanda Kidavashari.
Inadaiwa alipofika nyumbani kwa mumewe,
Mlengo alimfukuza ndipo alirudi kwa bibi yake na kulazimika kulala huko
hadi asubuhi alipofuatana na bibi yake ndipo mumewe akampokea.
Kidavashari alifafanua kuwa juzi, saa mbili
usiku Agatha alishindwa kula chakula alichokipika mwenyewe ndipo mumewe
alipoona hali yake imebadilika ndipo alilazimika kuomba msaada wa
pikipiki kwa rafiki yake aitwae Alfred Kasonso na kumkimbiza katika
zahanati kijijini humo kwa matibabu.
Kamanda alithibitisha kuwa mume wa marehemu huyo na Faustina wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.