Utata kuhusu Heroine iliyonaswa Kenya
https://samchardtz.blogspot.com/2014/04/utata-kuhusu-heroine-iliyonaswa-kenya.html
Hiki ni kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kunaswa Afrika
Serikali
ya Kenya imelalamika kuwa haikupewa taarifa zozote kuhusu dawa za
kulevya zilizonaswa na wanajeshi wa Australia wanaoshika doria katika
ufuo wa bahari Hindi , ufukweni mwa Kenya.
Hii
ilijitoza katika mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina
Mohammed na balozi wa Australia nchini humo Bwana Geof Tooth aliyetakiwa
na serikali kuelezea kuhusu tukio la kunaswa kwa dawa hizo.
Zilinaswa
Ijumaa zikiwa zimepakiwa katika mifuko 46 ambayo ilikuwa imefichwa
kwenye mifuko ya SimitiDawa hizo zenye uzani wa kilo 1,023 ambazo ni
kiwango kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kunaswa katika pwani ya
Afrika, ni za thamani ya dola milioni 289.
Ubalozi
wa Australia umekanusha madai kuwa, manowari yake ya kijeshi iliingia
katika eneo la bahari inayomilikiwa na Kenya na kunasa shehena ya dawa
hizo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, ubalozi huo umesema
kuwa madawa hayo ya kulevya yalinaswa katika eneo la bahari
inayomilikiwa na jamii ya kimataifa na kuwa hakuna manowari yake
iliyoingia Kenya.
Pia
yalinaswa katika operesheni dhidi ya biashara ya kimataifa ya dawa za
kulevya. Taarifa zilisema kuwa dawa hizo ziliharibiwa kwa kumwagwa
baharini.
Taarifa
hiyo imesema kuwa tukio hilo halina uhusiano wowote na Kenya na kuwa
habari zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini Australia kuwa madawa
hayo yalinaswa karibu na kenya ilikuwa kutoa taswira tu ya eneo la
tukio.
Shehena kubwa kuwahi kunaswa
Wiki
iliyopita wanajeshi wa Australia walinasa mashua moja iliyokuwa
imesheheni zaidi ya tani moja ya madawa ya Heroine katika bahari ya
hindi na taarifa hiyo inasema kuwa mashua iliyonaswa haikuwa na usajili
wowote.
Ubalozi
huo umekariri kuwa haukuhusika na operesheni hiyo ambayo ilifanywa na
wanajeshi wa majini wa Australia wanaoshika doria katika bahari ya hindi
chini ya mkataba wa kimataifa wa kupambana na uharamia na uhalifu
katika bahari ya hindi.
Hata
hivyo ubalozi huo umesema kuwa shirika la kimataifa la kupambana na
uharamia na uhalifu CMF litaendelea kushirikiana na serikali ya Kenya
hasa katika kuelezea zaidi operesheni yake.
Tangu
shehena hiyo kukamatwa kumekuwa na shauku miongoni mwa maafisa wa ulinzi
na wale wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni nchini Kenya kuhusiana na
tukio hilo na madai kuwa kenya haikuhusishwa katika operesheni hiyo
licha ya kutendeka katika eneo linalosemekana kuwa lake.
NA BBC SWAHILI