Tanzania yagonga miaka 50
https://samchardtz.blogspot.com/2014/04/tanzania-yagonga-miaka-50.html
Dar/ Mikoani.
Wakati leo ni maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar uliozaa taifa la Tanzania, wasomi, viongozi wa dini, watendaji
wa Serikali na wananchi wa kawaida wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu
uhai wa Muungano huo.Wakizungumza
na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi walitaka Muungano huo
uvunjike kwa madai ya kutokuwa na manufaa yoyote, au uwe wa Serikali
moja, huku wengine wakitaka uenziwe kwa sababu ndiyo chachu ya amani,
umoja na mshikamano uliopo sasa.
Alisema
wadhifa wa Rais wa Zanzibar na makamu wake viondolewe na pande zote
zikubali baadhi ya vitu kutoa sadaka kwa kuvipoteza.
“Nakerwa
zaidi na Zanzibar kuwa na Katiba yao , wakati Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inasema Zanzibar ni sehemu ya nchi yake pia. Wakati
wa Sherehe za Muungano, Rais wa Zanzibar ndiye anaonekana mwenye nguvu,
kitu ambacho siyo sahihi. Rais wa Tanzania ndiye apewe hadhi kubwa,”
alisema.
Diwani wa
Kata ya Kilema Kusini, Kawawa Lubega alipendekeza Serikali mbili na
alitoa sababu kuwa hata Serikali mbili za sasa bado wananchi
hawajazifahamu vizuri. Lubega alisema kwamba shirikisho la serikali tatu
litasababisha Rais atakayekuwapo madarakani akose nguvu kiuchumi na
kiutawala.
Ofisa
Elimu wa Shule za Sekondari za Wilaya ya Moshi, George Jidamva
alipendekeza kuwapo kwa serikali mbili, lakini akashauri Katiba zote
mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, ziwekwe
mezani ili dosari zilizopo zirekebishwe akitaja kipengele cha madaraka
ya Rais.
Mwanasheria
wa Serikali, Wilaya ya Moshi, Glorian Issagya alipendekeza pia serikali
mbili ziendelee, lakini akasema wabunge waliojitoa bungeni, warudi ili
changamoto zinazojitokeza ziweze kufanyiwa kazi zisije zikaleta athari
hapo mbeleni.
Kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya, mwanasheria huyo alipendekeza ungepitia kwenye
Halmashari za Wilaya na hali hiyo ingekuwa rahisi kwa kila mtu kutoa
maoni yake kwani atakuwa amepata elimu kupitia vitongoji, vijiji hadi
kata.
Songea
Naye
mwanasiasa, Asha Kitambuli mkazi wa Wilaya ya Tunduru alisema kuwa
binafsi anapenda Muungano uendelee kuwapo akieleza kuwa una faida nyingi
na kwamba wanaopenda uvunjike ni waroho wa madaraka na wabinafsi,
akataka waache kuvuruga Muungano.
Aliongeza
kuwa, Muungano uendelee kwani ndiyo umetufikisha tulipo na kwamba
hapendi uvunjike bali kero zilizopo zirekebishwe ikiwa ni pamoja na
Watanzania Bara wawapo Zanzibar kupewa uhuru wa kufanya biashara kama
ilivyo kwa Wazanzibari.
Naye
Anispheta Malingali, mkazi wa Songea alisema Muungano uvunjwe akidai
kuwa hauna faida kwa Watanzania Bara, aliosema wamekuwa wakinyenyekea
Wazanzibar bila mafanikio na wenzao bado hawatambui mchango wa Muungano
huo zaidi ya kulalamika kila kukicha.
“Mimi
binafsi naona bora tuuvunje huo Muungano, sioni faida yake kwani wenzetu
ndiyo wanafaidi kutoka kwetu. Sisi hatuna hata raha ya Muungano, kila
kukicha wenzetu wanadai huduma muhimu kama afya, maji na umeme na
wanatekelezewa, lakini bado hawaoni faida, wamepewa hadi Bunge lao bado
hawajaridhika, wamepewa Serikali bado hawaridhiki. Binafsi sioni haja ya
kuendelea kuungana na watu walalamishi wanaopenda machafuko,”alisema
Malingali.
Mtwara
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo cha Stella Maris, mkoani Mtwara, Dk Aidan Msafiri,
alisema kuwa dhana ya Muungano ni nzuri kwani umoja ni nguvu na Muungano
ni kama mwili wa binadamu. Kikubwa ni kuzingatia maadili ya kuungana ni
lazima wote walioungana kushirikiana, kuwe na uwazi, haki na usawa.
Yaani
walioungana wawe kama wanandoa, pia kuwe na faida kwa wote walioungana
na tujifunze kwa wenzetu walioungana mfano Marekani.
Alisema
kwamba kusiwe na ubabe wa kulazimisha serikali mbili au tatu, lakini ni
vyema tukarudi kwenye serikali moja. Kuwa na serikali mbili au tatu
kutakuwa na changamoto kubwa, tuwe kitu kimoja.
Naye
Katibu Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Faidika Wote Pamoja (Fawopa) la
mkoani Mtwara, Komba Baltazary alisema: “Muungano una faida kubwa kwani
tumechanganya nguvu za Wabara na Wazanzibari, hivyo kuwe na mfumo bora
wa uchumi.”
Aliongeza katika muundo kwa maana ya kubakia kwa Tanganyika na Zanzibar kuwe na utambulisho kwa kila nchi kati ya nchi hizo.
“Tuwe na muundo unaoweza kujadiliwa na wananchi wote kama yalivyotolewa maoni kwenye Tume ya Katiba,”alisema.
Bukoba
Makamu
Mwenyekiti wa Chama cha Saidia Wazee Karagwe (Sawaka) Clement
Nsherenguzi, alisema: “Ni muhimu kuonyesha kuwa tumeungana kweli kwa
kuwa na taifa moja la Watanzania na kuondoa ubaguzi unaojionyesha katika
masuala mbalimbali ikiwamo matukio yanayohusisha viongozi wa kitaifa.”
Naye
Katibu wa Chama cha Walemavu, Manispaa ya Bukoba, Sweetbert Mshanga
alisema: “Muungano kati ya nchi hizo umesaidia kujenga amani na
mshikamano pamoja na kuwa ni wananchi wanaofahamu matunda ya moja kwa
moja yanayotokana na Muungano huo.”
Alibainisha
kuwa faida za kuungana ni kubwa ikilinganishwa na hasara ambayo
ingepatikana kwa kutoungana, huku akitaka wananchi waelezwe wazi faida
na matunda ya Muungano.
Akitoa
maoni yake kuhusu miaka hamsini ya Muungano, Mwenyekiti wa Serikali ya
Kitongoji cha Kajure katika Kisiwa cha Bumbire, wilayani Muleba,
Deogratias Mutebwa alisema kuwa ni makosa kutaka kuua Muungano kwa
visingizio vya kero zilizopo alizosema zinaweza kufanyiwa kazi bila
kuvunja Muungano na kuwa muundo unaofaa ni serikali mbili.
Mara
Damiani
Thobias ambaye ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Sederec,
wilayani Serengeti alisema kwamba Muungano haufai kuendelea kukumbatiwa
kwa kuwa hauna tija kwa wananchi.
“Kuna
upungufu katika muundo wa serikali mbili, ndiyo maana wananchi wakatoa
maoni ya muundo wa serikali tatu unaolenga kutatua kero hizo, kama
unajengwa na nchi mbili, iweje nchi moja isionekane?”alihoji.
Nashoni
Mkondya Mwenyekiti wa Mtaa wa Bomani mjini Mugumu (CUF)alisema: “Wajumbe
wa Bunge la Katiba wanahoji uhalali wa maoni ya waliotaka serikali
tatu, mbona hawahoji uhalali wa Rais Kikwete aliyechaguliwa na watu
wachache kuwa Rais kati ya Watanzania waliopo na wao mbona ni wachache
kuliko walioko nje lakini wanajiona halali.
Aidha,
aliomba wajumbe watambue kuwa kujadili sera ya chama ya serikali mbili
wakaacha maoni ya wananchi ni kutokujua nini wanafanya kwa kuwa Katiba
ni juu ya vyama na ndiyo inaweka vyama lakini sera ya vyama haviweki
katiba.
Iringa
Mhadhiri
Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), mkoani Iringa, Gotrib Mgaya,
alieleza kushangazwa na mjadala wa Bunge la Katiba unaoendelea kwa sasa
na kusema wanaopendekeza serikali mbili wanapaswa kuja na hoja ya
kuitaka Zanzibar ibadilishe Katiba yake ya mwaka 2010.
“Kwa
maoni yangu Rasimu ya Pili ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph
Warioba imebeba maoni ya wananchi na ushahidi upo wa kutosha licha ya
wabunge kuupinga. Mimi nadhani muundo huo unatibu matatizo ya muda mrefu
ya Muungano,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Muundo
huu ulizingatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya 2010 ambayo imetamka
kuwa Zanzibar ni nchi na kumpa mamlaka Rais wake kuwa na uwezo wa
kuunda vikosi vya ulinzi, hatua hiyo imepunguza nguvu kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Pwani
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Mariam Halfani, Bosco Mfundo, Amina Hussein,
Mwantumu Shaaban, Jesca Laizer, George Bundi na Machapula Donard
walisema katika miaka 50 ya Muungano udhaifu uliojitokeza ufanyiwe kazi.
Walisema
endapo pande zote zitaridhiana na kukubali kufanyika marekebisho
itawezesha kupata suluhisho la kudumu na kuondoa manung’uniko ya
wananchi wa nchi washirika za Tanganyika na Zanzibar.
Naye
George Bundi alisema: “Mimi nafurahi miaka 50 sote tunasherehekea
Muungano, lakini zipo changamoto kila siku zinaelezwa kuhusu huu
Muungano, sasa basi wakati huu zifanyiwe marekebisho ili upande mmoja
usiwe na manung’uniko. Sasa kwa nini wanakataa wazi Tanganyika siyo
nchi? Wakisema hivyo basi hata huo Muungano uliopo ambao ni wa pande
mbili za nchi ya Tanganyika na Zanzibar nao haupo.”