Mama Kikwete awataka Walemavu kutokumlaumu mwenyezi Mungu kwa Ulemavu wao
https://samchardtz.blogspot.com/2014/04/mama-kikwete-awataka-walemavu.html
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akimkabidhi Kiongozi wa Kituo cha walemavu cha
Raisbura Bwana Mohamed Chitawala baadhi ya vyakula alivyowaletea-
mchele, unga, mafuta ya kupikia, sukai, soda na vinginevyo wakati
alipotembelea kituo cha walemavu cha Rasibura huko Lindi siku ya Pasaka.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Watu
wenye ulemavu wa viungo wametakiwa kutosikitika kwanini Mwenyezi Mungu
aliwaumba hivyo na kujiona wanyonge bali wajione wako sawa na watu
wengine kwani katika maisha ya binadamu kila jambo lina makusudi yake.
Hayo
yamesemwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wazee
wenye mahitaji maalum wanaoishi katika kituo cha Rasbura kilichopo
wilaya ya Lindi mjini.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alifika kituoni hapo kwa ajili ya kuwajulia hali wazee hao na
kuwapatia zawadi mbalimbali za mchele, nyama, sukari, unga wa ugali,
vitunguu, mafuta ya kupikia, nyanya na soda kwa ajili ya sikukuu ya
Pasaka.
Alisema
inawezekana Mwenyezi Mungu aliwaumba hivyo walivyo ikiwa ni kwa
makusudi ili iwe njia rahisi ya kumfikia yeye na kuwataka kushukuru kwa
yote. Jambo la muhimu aliwaomba waendelee kuishi kwa amani na upendo
kama ndugu.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akimkabidhi zawadi yake ya Pasaka Ndugu Theresia
Thomas ambaye ni mlemavu wa viungo anayeishi katika kituo cha Rasibura
huko Lindi. Baadaye Mama Salma anaonekana akipiga picha naye akiwa
amelala kitandani kwani Theresia hawezi kukaa wala kusimama.
“Nilipanga
siku ya leo kusherehekea sikukuu ya Pasaka pamoja nanyi huwa nafanya
hivi katika sikukuu mbalimbali kama X-Mass na Mwaka mpya, nasherehekea
na watoto yatima na watu wazima wa dini mbalimbali nawaomba adhimisheni
siku hii katika mazingira ya upendo, amani na utulivu”, alisema
Mwenyekiti huyo wa WAMA.
Akielezea
Historia ya kituo hicho kinachomilikiwa na kanisa Katoliki Jimbo la
Lindi Mkurugenzi wa KARTAS Mzee Saimoni Mnimbo alisema miaka ya nyuma
kituo hicho kilikuwa ni Gereza la wafungwa lakini mara baada ya
kujengwa kwa gereza jipya ndipo Serikali ililipatia jengo hilo Idara ya
Ustawi wa jamii na ikaanza kulitumia kama kituo cha wazee wasiojiweza.
Mzee
Mnimbo alimshukuru Mama Kikwete kwa moyo wake wa huruma na kuamua
kwenda kuwatembelea na kuwapatia zawadi mbalimbali vikiwemo vyakula na
vinywaji na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano ingawa kanisa
linawahudumia wazee hao bali nao wanatakiwa kuwasaidia.
“Tunawashukuru
wadau mbalimbali wanaotuunga mkono na kuwahudumia wazee hawa. Hapa
kwetu hakuna tatizo la maji, kuna kipindi mji mzima wa Lindi haukuwa
na maji lakini katika kituo hiki tulikuwa na maji ya kutosha
tunaishukuru ofisi ya Mkuu wa mkoa kwa kutulipia bili ya maji kila
mwezi”, alisema Mzee Mnimbo.
Baadaye Mama Salma anaonekana akipiga picha naye akiwa amelala kitandani kwani Theresia hawezi kukaa wala kusimama.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi Mzee
Ally Mtopa alisema katika kituo hicho hakuna mambo ya udini kwani
binadamu wote ni sawa na kwa yeyote anayejijuwa kuwa yeye ni binadamu
basi akili yake ikitazame kituo hicho na kuweza kukisaidia .
Naye
Mzee Mohamed Chitawala ambaye anaishi katika kituo hicho alisema
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za afya kwani wakienda
Hospitali kupata matibabu wanapata usumbufu na katika kituo hicho
hakuna dawa za huduma ya kwanza.
Tangu
mwaka 1995 kituo hicho kinamilikiwa na kanisa Katoliki jimbo la Lindi,
wazee wanaoishi hapo wana ulemavu wa macho na viungo kutoka dini zote
ambao wametelekezwa na jamaa zao. Idadi yao ni 10 kati yao wanawake ni
sita na wanaume ni wanne kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huu.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akiongea na baadhi ya watu wenye ulemavu
wanaoishi katika Kituo cha Rasibura mara baada ya kuwakabidhi zawadi zao
za Pasaka. Picha na John Lukuwi.