Serikali yasikia kilio deni kubwa la MSD
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya
http://samchardtz.blogspot.com/2014/11/serikali-yasikia-kilio-deni-kubwa-la-msd.html
Jana wabunge kadhaa walisimama na kuibana Serikali wakitaka sasa suala hilo litolewe maelezo, huku baadhi wakipinga hatua ya vikao vya Bunge kuendelea kama fedha hizo hazitalipwa.
Hatua hiyo ilitosha kuifanya Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu ambaye anakaimu pia nafasi ya Kiongozi wa Shughuli za serikali bungeni, Profesa Mark Mwandosya kuahidi kuwa tamko la serikali kuhusu hali ya vifaa tiba na dawa nchini litatolewa wiki hii.
Mbunge wa kwanza kulalamikia hali mbaya ya huduma za matibabu nchini, alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) ambaye aliomba Mwongozo wa Spika, na kuelezea namna wanawake wenye saratani ya shingo ya kizazi wanavyopata mateso, kutokana na kuharibika kwa mtambo maalumu wa mionzi katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.
Alisema hali hiyo inatokana na mtambo wa pili katika hospitali hiyo kuwa mbovu kwa muda mrefu sasa bila kutengenezwa, hatua iliyofanya wagonjwa kutegemea mtambo mmoja uliokuwa umesalia, ambao nao sasa umeharibika.
Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Khasim Ahmed (CUF) yeye alipinga vikali hatua ya vikao vya Bunge kuendelea, huku deni la zaidi ya Sh bilioni 102 la MSD likishindwa kulipwa na serikali na kufanya wagonjwa kuendelea kuteseka.
Mbunge huyo ambaye alitoa hoja na kuungwa mkono na wabunge wengine, alisema hakuna sababu kwa Bunge hilo kuendelea na hivyo alitoa hoja ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea ili fedha za wabunge, zikalipe deni la MSD.
Hatua hiyo ilitosha kumfanya Mwandosya kusimama na kutoa ahadi ya Serikali ya kuwasilishwa kwa tamko maalumu la Serikali bungeni wiki hii kuhusu hali ya vifaa tiba, ikiwemo pia suala la deni la MSD.
Mbali ya suala la MSD, Waziri Mwandosya akijibu mwongozo wa Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) kuhusu wakulima kukosa masoko na kulemewa na mazao ambayo sasa yanakaribia kuoza, pia alisema Serikali kupitia kwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza itawasilisha tamko wiki hii.
Ahadi hiyo ya Waziri Mwandosya ilipokelewa kwa furaha na wabunge wengi, ambao baadaye wakichangia kwenye muendelezo wa hotuba ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2015/2016, waliipongeza Serikali kwa ahadi ya kushughulikia suala hilo la MSD.
Tangu kuanza kwa Mkutano unaoendelea wa Bunge, suala la deni la MSD limechukua sehemu kubwa ya mjadala, hatua ambayo bila shaka ndiyo iliyoifanya Serikali kuamua kulitolea tamko kwa lengo la kueleza mikakati ya kuokoa maisha ya Watanzania wanaoteseka hospitalini.
Mbunge mwingine ambaye amewahi kupendekeza Bunge kuahirishwa ili fedha wanazolipwa zikalipe deni la MSD kuiwezesha Bohari hiyo kununua dawa, ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), aliyetoa hoja hiyo wiki iliyopita.
Naibu Spika, Job Ndugai mara zote ambazo suala hilo limetajwa bungeni, amekuwa akisema ni suala zito na kubwa, lakini amekuwa akiwaomba wabunge kuvuta subira wakati Serikali ikiendelea kulifanyia kazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu na wa uhakika.