ESCROW GUMZO LA SASA MJINI
http://samchardtz.blogspot.com/2014/11/escrow-gumzo-la-sasa-mjini.html
WAKATI sakata
la kuchukuliwa kwa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta
Escrow likiendelea kuwa gumzo la sasa la mjini, sura mpya imeanza
kujitokeza kwa watu zaidi wanaohusishwa na kugawiwa salio kutajwa, licha
ya waliotajwa awali kuendelea kubakia katika orodha.
Kashfa
hiyo iliibuliwa kwa mara ya kwanza na mbunge wa Kigoma Kusini kupitia
Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila katika kikao cha Bunge
lililopita, kitu ambacho kilipingwa kwa nguvu kubwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Hata
hivyo, kadiri siku zinavyokwenda hali imeonekana kuwa ni ngumu kwa
vigogo wa serikali kwani wanaonekana kama wameshikwa pabaya na wengi
wametajwa kuhusika kwa njia moja au nyingine.
Ukiacha Werema, Muhongo
na Eliakim Maswi kutajwa kunufaika na uchotwaji wa fedha hizo zilizokuwa
Benki Kuu, wengine wanaodaiwa kupata mgao huo ni pamoja na Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka,
mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali, Andrew Chenge na Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndullu.
4Aidha
vigogo wengine wengi, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, nao
wanatajwa kuhusishwa na ukwapuaji wa fedha hizo kutokana na nyadhifa
zao.
Lakini
wakati Bunge hilo likianza vikao vyake vya wiki hii, Spika wa Bunge,
Anne Makinda, naye alitajwa bungeni na Mbunge wa Mkanyageni kwa tiketi
ya CUF, Habib Mnyaa kuwa anadaiwa kupewa mgao wa dola milioni moja za
Marekani.
Kana
kwamba haitoshi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali, katika kijarida
maalum kilichochapishwa kumchafua kilichosambazwa Dodoma, naye anatajwa
kuchukua mlungula kutoka kampuni inayohusishwa na sakata hilo ya PAP.
Akaunti
ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kutunza
fedha ambazo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) zilipaswa
kuilipa kampuni ya kufua umeme wa IPTL kwa kuiuzia nishati hiyo.
Hiyo
ilitokana na shirika hilo la umma, kushtaki katika mahakama ya
kibiashara ikilalamikia bei kubwa iliyotozwa na IPTL na kusababisha
kufunguliwa kwa akaunti hiyo ili fedha hizo ziwekwe huko hadi muafaka
baina ya pande hizo mbili utakapopatikana.
Hata hivyo, kabla ya muafaka huo kupatikana, wajanja walikwenda na kuzichukua fedha hizo ambazo sasa zinawatokea puani!


