TRENI YENYE SHEHENA YA KEMIKALI YAPINDUKA NA KUZUA TAHARUKI KWA WANANCHI
http://samchardtz.blogspot.com/2014/10/treni-yenye-shehena-ya-kemikali.html

Shehena
ya kemikali ya salfa iliyoachwa Kijiji cha Kifuru, wilayani Kisararwe
na Mamlaka ya Reli ya Tazara na Zambia (Tazara) baada ya treni yake ya
mizigo kupata ajali, huenda ikawa tatizo kubwa kwa taifa kama itachelewa
kuondolewa.
Tayari moshi uliotokana na moto uliozuka baada ya mabehewa hayo kupinduka umeshaanza kuleta matatizo kwa wakazi wa eneo hilo.
Baadhi
ya wananchi ambao walizungumza na gazeti hili kijijini hapo walisema
kuwa kuungua kwa shehena hiyo kumewatia hofu kubwa kutokana na kutambua
kuwa kemikali hizo zina madhara makubwa kwa binadamu hasa zinapoingia
kwenye maji na kusambaa kwenye hewa. Kijiji hicho kina watu 571.
Aidha
katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha, wananchi hao
wanahofu kwamba kemikali hiyo itaingia Mto Mpiji, ambayo maji yake
yanakutana na maji ya Mto Msimbazi ambayo yanatumiwa na wakazi wa Dar es
Salaam.
Baadhi
yao walidai kupata madhara ya kiafya na kwenda kupata matibabu katika
Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe na kuelezwa kuwa hewa chafu ya kemikali
hiyo ndio iliyowasababishia madhara hayo na hivyo wakashauriwa kunywa
maji mengi pamoja na maziwa ili kuondoa sumu ya kemikali hiyo mwilini.
“Baada
ya moshi wa kemikali hiyo kutapakaa kijijini hapa, nilijisikia vibaya
mbavu zikaniuma, nilienda pale Kisarawe nikalazwa siku moja, lakini
madaktari waliniambia , tatizo langu limetokana na kuvuta hewa chafu,”
alisema Latifa Ramadhani.
Naye
Mtendaji wa Kijiji cha Kifuru, Mohammed Kaudunde alisema baada ya treni
hiyo ya mizigo kuanguka wiki moja iliyopita alisema kijijini hapo
wananchi wengi walilalamika afya zao jambo ambalo liliwalazimu kumuita
daktari wa wilaya.
“Alikuja
daktari wa wilaya hapa na timu yake wakatutangazia tu kwamba tusisogee
eneo la tukio na kwamba wananchi wanywe maji mengi pamoja na maziwa,”
alisema Kaudunde.
Alisema
pia Katibu Tawala wa Wilaya na viongozi wengine wa halmashauri ya
wilaya walifika kijiji hapo na wananchi zaidi ya 20 wakalalamika
kuathirika na moshi huo kiafya.
Mkuu
wa Usalama wa Tazara, Elisha Mhoka alisema tayari Tazara
imeshawasiliana na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) ili kusafisha
eneo hilo.
Mhoka
alisema NEMC walikuwa wanasubiri mafundi wa Tazara wamalize kazi ya
kutengeneza reli iliyokuwaimeharibika katika eneo hilo, kazi ambayo
wameikamilisha Ijumaa usiku ili waanze kazi hiyo ya kuondoa shehena hiyo
ya salfa.
“Wametuambia
wakishaiondoa shehena hiyo na kwenda kuiteketeza, pia udongo wa sehemu
hii utachimbwa wote kuhakikisha udongo wote ambao umemwagikiwa na
kemikali hiyo unaondolewa eneo hili ili kulinda mazingira ya sehemu
hii,” alisema.
Alisema
ajali hiyo imetokea eneo la mto na akaongeza kuwa kuna haja ya kufanya
usafishaji huo haraka kuhakikisha kuwa mvua zitakaponyesha zisije
zikasafirisha kemikali hiyo na kuipeleka kwenye visima vya asili vya
wananchi.
Daktari
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Paschal Nkii alipoulizwa
na gazeti hili kama kuna wagonjwa ambao wamepelekwa hospitalini hapo
kutokana na tatizo hilo la kemikali, alikiri kulifahamu tatizo hilo
lakini akagoma kuzungumza kwa kuwa si Mganga Mkuu wa Wilaya.