Flatnews

TANZANIA KUONGEZA USHIRIKI WAKE KATIKA OPERESHENI ZA ULINZI WA AMANI-MHE. MEMBE



Waziri wa  Mambo ya Nje na  Ushirikiwano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe  akizungumza wakati wa mkutano wa Kilele wa ngazi ya Mawaziri uliozungumzia  Uimarishaji wa Operesheni za Kulinda Amani. Mkutano huo uliandaliwa na  Marekani ambapo Makamu wa Rais wa nchi hiyo Bw. Joe Biden ndiye aliyeongoza mkutano.  Waziri  Membe ametoa ahadi ya ushiriki zaidi wa Tanzania  katika operesheni  za kulinda amani chini ya Umoja wa Maifa

 Sehemu ya washiriki wa mkutano wa  uimarishaji wa  Operesheni za Kulinda Amani uliokuwa umeandaliwa na Marekani na kufanyika hapa Umoja wa  Mataifa sambaba na  majadiliano ya jumla ya   Baraza Kuu la 69 la Umoja wa Mataifa ( UNGA) zaidi ya  nchi therethini zimetoa ahadi zao wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki  Moon
 Mhe. Waziri akiteta jambo na  Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo ambao uliongozwa na  Makamu wa Rais wa Marekani Bw. Joe Biden.


Na Mwandishi Maalum

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuongeza kiwango cha ushiriki wake katika Operesheni za Ulinzi wa Amani kupitia Umoja wa Mataifa, ambapo imebainisha kusudio lake thabiti la kuongeza vikosi vitatu ili kusaidia kurejesha Amani palipo na migogoro ndani ya Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe ( Mb) ametoa ahadi hiyo siku ya Ijumaa, hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa kilele wa ngazi ya Mawaziri Uimarishaji wa Operesheni za Ulinzi wa Amani ulioandaliwa na Marekani na kuongozwa na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Bw.Joe Biden.

Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Rais wa Rwanda, Mawaziri Wakuu wa Japan, Bangladesh na Pakistan. Ulikuwa na lengo la kukusanya ahadi mpya za kuimarisha operesheni za ulinzi wa Amani ambapo Joe Biden alitangaza kuwa nchi yake imetenga dola 110 milioni zitakazotumika katika kuimarisha uwezo wa nchi za kiafrika kushiriki kwa ufanisi katika ulinzi wa Amani. Fedha hizo zitatolewa kwa kipindi cha kati ya miaka mitatu na mitano.

Mhe. Membe yuko hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa akishiriki mikutano mbalimbali inayokwenda sambamba na majadiliano ya Jumla ya Baraza Kuu la 69 ( UNGA) ambalo Mhe. Rais Jakaya Kikwete alilihutubia siku ya Alhamis.

Waziri amesisitiza kuwa Tanzania haichukuli wajibu wa operesheni za kulinda Amani kwa kubahatisha au kiurahisi, bali inauchukua wajibu huo kwa uzito na kwa dhamana kubwa.

Ameongeza kuwa, ni kwa kutambua uzito na umuhimu wa dhamana hiyo ndiyo maana Tanzania hivi sasa ni nchi ya 12 kati ya 122 zinazoongoza kutoa walinzi wa Amani duniani ikiwa na wanajeshi zaidi 2,300 kati ya 96,535 wanaohudumia Misheni 16 za Umoja wa Mataifa zilizopo sasa.

“Tunaamini katika msemo wa Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba, nyumba ya jirani yako ikiwaka moto, basi jua kijiji kizima kiko hatarini”. Akasisitiza Mhe. Waziri.

Na kuongezaa ni msingi huo unaoendelea kutoa mwongozo wa ushiriki wa Tanzania katika Operesheni za Ulinzi wa Amani kwa kupeleka wanajeshi wake huko Lebanon,(UNIFIL), Darfur ( UNAMID) na DRC ( MONUSCO).

Pamoja na Tanzania nchi nyingine zaidi ya thelathini zimetoa ahadi zao katika mkutano huo. 

Post a Comment

emo-but-icon

item