Marekani yaendeleza mashambulizi dhidi ya IS
Muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la dola la kiislamu IS umefanya mashambulizi mapya ya kutokea angani dhidi ya kundi hilo...
http://samchardtz.blogspot.com/2014/09/marekani-yaendeleza-mashambulizi-dhidi.html
Muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la dola la kiislamu IS
umefanya mashambulizi mapya ya kutokea angani dhidi ya kundi hilo nchini
Syria, yaliyolenga viwanda vya mafuta kwa siku ya pili
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria limeripoti kutokea
mashambulizi mapya katika mkoa wa mashariki mwa Syria wenye utajiri wa
mafuta, Deir Ezzor, na Hasakeh katika upande wa kaskazini mashariki,
maeneo ambayo pia yalishambuliwa siku moja kabla.Mashambulizi yote ya kutokea angani yalivilenga visima vya mafuta katika mikoa hiyo miwili, ambako wanamgambo wa IS huchukua mafuta yao kwa ajili ya biashara ya magendo.
Watalaamu wanasema kuwa mauzo ya mafuta kutoka Syria na Iraq ni miongoni mwa chanzo kikubwa cha mapato ya kundi hilo, ambalo hutengeneza karibu dola milioni moja na tatu kwa siku.
Wakati huo huo nchini Uingereza wabunge wanajiandaa kupiga kura ya kuamua kama nchi hiyo itajiunga na operesheni ya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya kundi hilo nchini Iraq, ijapokuwa hakuna uwezekano wa Uingereza kushiriki katika mashambulizi yanayofanywa nchini Syria.
Waziri Mkuu wa uingereza David Cameron akiuhutubia mkutano wa kilele mjini New York kabla ya kurejea nyumbani alisema lazima juhudi za pamoja zichukuliwe ili kuukabili ugaidi. Kama bunge la Uingereza litaidhinishisha nchi hiyo kujiunga na mashambulizi, ndege za kivita za Jeshi la Uingereza zitajiunga na ndege za Marekani, Ufaransa, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Jordan katika kuzipiga ngome za IS. Tayari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kupambana na wapiganaji wa kigeni.
Ubelgiji na Uholanzi pia zinapanga kutuma ndege za kurusha mabomu aina ya F16 ili kujiunga na operesheni ya Iraq. Uholanzi pia itatuma wanajeshi 250 pamoja na maafisa wengine 130 wa kutoa mafunzo kwa jeshi la Iraq wakati naoy Ugiriki ikisema itatuma silaha kwa wanajeshi wa Kikurdi wanaopambana na majihadi.
Hapo jana, polisi jijini London iliwakamata watu tisa wanaoshukiwa kuwa na mahusiano na wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu, akiwemo mhubiri mmoja mwenye msimamo mkali.
Nalo shirika la ujasusi la Marekani FBI limesema limemtambua mwanamgambo wa Dola la Kiislamu aliyeonekana katika video zinazoonesha wanahabari wawili wa Marekani wakichinjwa na mfanyakazi wa misaada wa Uingereza, ijapokuwa limekataa kutoa maelezo zaidi. Mashambulizi ya kutokea angani yanayofanywa na majeshi ya muungano nchini Syria yameripotiwa kuwauwa karibu wapiganaji 140 pamoja na raia 13, ijapokuwa wizara ya ulinzi ya Marekani imesema bado inachunguza ripoti za kuwepo vifo vya raia.