Jaji Warioba Azidi Kushambuliwa..Afanaishwa na Maiti Iliyokufa Ikafufuka
http://samchardtz.blogspot.com/2014/09/jaji-warioba-azidi-kushambuliwaafanaish.html
Mbunge
wa Mbinga Kusini, Kapteni John Komba, kwa mara nyingine amemshambulia
aliyekuwa Mweyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba, kwa ‘kuwaingilia’ na amemuomba Rais Jakaya Kikwete, amuite na
kumkanya.
Katika
mchango wake bungeni jana, Komba alianza kwa kusema, “Ninalo moja kubwa
la kuchangia hapa, juzi nilizungumza habari hapa, jamani eh..., mtu
akishazikwa, akifufuka ni tatizo kubwa katika kijiji kile, kazi
haziendi…sasa jana (juzi) mmeona.?”
“Mimi nasema ukweli kabisa, huyu mzee ana nini, ana kitu gani na sisi, mbona anatuingilia sana,” alisema.
Komba
alisema anamwomba Rais amwite Jaji Warioba na kumweleza hakumtuma
kufanya hivyo isipokuwa kukusanya maoni basi, na inatosha hapo
alipofikia.
Alisema,
Jaji Warioba alipoteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, kitu
cha kwanza alinukuliwa akisema, “mmenichagua mimi na wenzangu sasa
naomba mtuache msituingilie, na kweli hakuingiliwa na alifanya kazi na
kumaliza vizuri bila kuingiliwa.”
“Lakini anatuingilia sisi, mkuki kwa nguruwe? Yeye amekuwa refarii?
Anatufuatilia
kila tunachofanya, sasa na yeye anasema atapambana na sisi, ataingia
mitaani, anapambana na sisi, yeye upande mwingine na sisi upande
mwingine, haya, njoo Warioba kwetu, tutaonana,” alisema.
Alisema
Jaji Warioba anafanya kinyume na alivyoagizwa, kwani wakati wa kuunda
tume yake, Rais alimwambia akusanye maoni basi, na amekusanya mengi.
Alisema
Jaji Nyalali alipokuwa anakusanya maoni kuhusu mfumo wa demokrasia ya
vyama vingi maoni yalionyesha asilimia 80 ya watu walipenda mfumo wa
chama kimoja uendelee na asilimia 20 walipenda mfumo wa vyama vingi,
jambo ambalo lilikuja kuheshimwa.
Hata hivyo, alisema anashangaa kuona kila wanachokifanya wajumbe wa BMK, Jaji Warioba kazi yake ni kuzungumzia tunu tu.
“Baba baba huyu kila kitu tunachokifanya yeye tunu tunu tunu tunu tunu tuuu basi,” alisema.
Kuhusu uhalali wa BMK, Komba alisema anashangaa kumwona Warioba ambaye ni Jaji anashindwa kuheshimu uamuzi wa majaji wenzake.
“Majaji wenzake wamesema bunge hili ni halali, sasa Warioba ni jaji gani ambaye hataki kuheshimu hata wenzake, jamani?
Shutuma
za Komba dhidi ya Jaji Warioba zinafuatia ushiriki wake katika
adhimisho la miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) jijini Da es Saam juzi.
Adhimisho
hilo pia lilitumika kumkumbuka muasisi wa LHRC, marehemu Dk. Sengondo
Mvungi ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumzia
adhimisho la juzi, Komba alisema wakati Jaji Warioba anazungumza
kulikuwa na wazungu wengi, na akaonyesha wasiwasi wake kuwa huenda (Jaji
Warioba) amepewa kitu na wazungu hao au ameahidiwa kitu hivyo akataka
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufuatilia.
Alisema jambo la ajabu ni kwamba, “baba huyu kila siku (anatuingilia) anatufuatilia kila tunachofanya.”
Alimtuhumu
Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu kuwa hana maadili lakini
Makamu Mwenyekiti wa BMK, Samia Hassan Suluhu, alimtaka Komba kufuta
maneno aliyomtuhumu (Warioba) kuwa hana maadili, naye akasema, “hana
maadili ya kujali wenzake kama wanafanya mambo mazuri, isipokuwa anayo
maadili ya mambo mengine.”
Kwa
upande wake Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, alizungumza kwa
kifupi kuwa anamshauri Jaji Warioba apumzike baada ya kufanya kazi nzuri
ya kukusanya maoni ambayo ndiyo yametumika kama msingi wa Katiba.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge alisema kuwa
anawaheshimu baadhi ya viongozi wanaoendelea kutoa maoni yao ya kuiponda
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa hivyo hapendi kabisa kulumbana nao.
Aliwataka
Watanzania kuzisoma Rasimu zote mbili (ile ya Jaji Warioba na
inayopendekezwa na BMK) ili wapime kuona ni ipi iliyo bora.
Alisisitiza
kuwa msingi wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na BMK ni Rasimu ya
Jaji Warioba hivyo madai ya kwamba maoni ya wananchi hayakuzingatiwa
hayana ukweli wowote.
Source:Nipashe