Catalonia kupiga kura ya maoni ya uhuru
Catalonia imetangaza rasmi kura ya maoni kuamua uhuru wake, ikiwa ni hatua ya karibuni kabisa miongoni mwa majimbo yanayotaka kujitenga ...
http://samchardtz.blogspot.com/2014/09/catalonia-kupiga-kura-ya-maoni-ya-uhuru.html
Catalonia imetangaza rasmi kura ya maoni kuamua uhuru wake, ikiwa ni
hatua ya karibuni kabisa miongoni mwa majimbo yanayotaka kujitenga
barani Ulaya na changamoto kubwa kwa serikali ya Uhispania.
Tangazo hilo lililotolewa Jumamosi (tarehe 27 Septemba) lilikuja wiki
moja baada ya Scotland kupinga kura ya kupinga kujitenga na Uingereza.Kiongozi wa Catalonia, Artur Mas, alisaini sheria ya rais inayotoa wito wa kufanyika kwa kura ya maoni katika sherehe zilizofanyika kwenye makao makuu ya serikali ya jimbo hilo mjini Barcelona, akiwa amezungukwa na viongozi wa kisiasa wa eneo hilo wanaouunga mkono kura ya uhuru.
"Kama yalivyo mataifa yote ulimwengeni, Catalonia pia ina haki ya kuamua mustakabali wake wa kisiasa," alisema Mas.
Hisia za uhuru kwenye mkoa huo ulio imara kiuchumi na ambako lugha ya Catalan hutumika sambamba na Kihispania zimekuwa zikipanda sana katika miaka ya hivi karibuni, zikichochewa na imani kwamba mkoa huo unastahili kuwa na nafasi zaidi ya kifedha na kisiasa kutoka serikali kuu mjini Madrid.
Uhispania yapinga
Serikali ya Waziri Mkuu Mariano Rajoy inasisitiza kwamba kura hiyo iliyopangwa kupigwa tarehe 9 Novemba 2014 ni kinyume cha sheria na haitafanyika.
Rajoy, ambaye alikuwa akirejea nchini kutokea China siku ya Jumamosi, alitazamiwa kuitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri kujadiliana suala hilo. Serikali yake inapanga kupeleka zuio kwenye Mahakama ya Katiba kupinga sheria iliyopitishwa hivi karibuni jimboni Catalonia ikiruhusu kura ya maoni ya uhuru, ikitarajia kuwa mahakama hiyo itaisitisha sheria hiyo na hivyo kuisimamisha kura hiyo ya maoni.
Katiba ya Uhispania hairuhusu kura za maoni kwenye suala la mamlaka ambayo haijumuishi Wahispania wote na wataalamu wanasema Mahakama hiyo ya Katiba itaamua kuwa kura hiyo ni kinyume cha sheria, lakini Mas amesema kwamba ikiwa kura ya maoni haiwezi kufanyika, basi ataitisha uchaguzi wa mapema, ambao unaweza kugeuka kuwa kauli ya ndio au hapana kwa uhuru.
"Tuko tayari kufikia makubaliano juu ya masharti ya kura ya maoni hadi dakika ya mwisho," alisema Mas.
Wakaazi wa Catalonia waunga mkono uhuru
Huku Mas akitoa wito wa kufanyika kwa kura hiyo ya maoni, maelfu ya wananchi wanaounga uhuru wa Catalonia walikusanyika kwenye uwanja mkubwa mbele ya jengo la serikali ya Catalonia katikati ya Barcelona, huku wengi wakiwa wamevaa na kupeperusha bendera za uhuru na huku wakipiga mayowe ya kuunga mkono kujitenga.
Mamia ya watu walikuwa wakisherehekea huku saa ikihisabu siku zilizobakia hadi kufanyika kwa kura ya maoni. "Leo ni siku ya kushangiria. Tumefurahi na tumeridhika kwamba Rais Mas ameitisha kura ya maoni," alisema Carme Forcadell, kiongozi wa kundi linalounga mkono uhuru ambalo limepigania kura hiyo ya maoni na kuandaa maandamano ndani ya kipindi cha miaka mitatu sasa.
Kinyume na ilivyokuwa kwa kura ya Scotland, matokeo yatakayounga mkono kujitenga kwa Catalonia hayatamaanisha moja kwa moja uhuru wa jimbo hilo tajiri, lakini Mas anasema yatampa nguvu ya kisiasa kuingia kwenye mazungumzo ya uhuru kamili na serikali kuu mjini Madrid.