Balozi Sefue afunguka Katiba Mpya
Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue.
http://samchardtz.blogspot.com/2014/09/balozi-sefue-afunguka-katiba-mpya.html
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema hakuna uwezekano wa kubadili
muundo wa muungano kutoka Serikali mbili kwenda Serikali tatu
katika mchakato wa Katiba.
Kauli ya Balozi Sefue imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa
Kituo cha Demokrasia (TCD) na kutoa uamuzi wa kuahirisha mchakato wa Katiba hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. (FS)
Suala
la muundo wa muungano lilichukua mjadala mkali ndani ya Bunge Maalumu
la Katiba huku wajumbe wanaounda kundi la Ukawa wakiunga
mkono mapendekezo ya Rasimu ya Katiba ya muundo wa Serikali tatu na wajumbe wa CCM wakisisitiza muundo wa Serikali mbili.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Balozi Sefue alisema mchakato
wa Katiba unahitaji maridhiano, lakini suala la muundo wa
muungano halina maridhiano katika jamii hivyo litachelewesha upatikanaji wa Katiba:
"Katika
historia ya nchi yoyote, wakati unafika wananchi wakawa na maridhiano
fulani, wakaamua kuyaingiza ndani ya Katiba. Tatizo linajitokeza pale
watu au makundi fulani yanapong'ang'ania kuingiza
ndani ya Katiba mambo ambayo ni dhahiri hayana maridhiano ndani ya jamii. Mfano ni suala la muundo
wa Muungano," alisema na kuongeza:
"Uzoefu
wa Bunge Maalumu hadi sasa ni kuwa hakuna uwezekano wa kupata
maridhiano ya kubadili muundo wa Muungano kutoka Serikali mbili kwenda
tatu. Hutapata maridhiano hayo ndani ya Bunge Maalumu na hutapata maridhiano ukienda kwa wananchi," alisema.
Alisema
anaamini wajumbe wa Bunge Maalumu walifanya uamuzi wa busara kuliweka
kando jambo hilo linalotugawa, na kuendelea kujadili Rasimu ya
Katiba kwa msingi wa mfumo uliopo wa Serikali mbili," alisema.
Balozi Sefue aliongeza kuwa tangu suala hilo liwekwe kando kumekuwa na kasi na matumaini ya kupata Katiba Mpya.
Alisema jambo hilo ni kubwa na uzoefu unaonyesha lina uwezo mkubwa wa kutugawa na kuchelewesha
kupatikana kwa Katiba Mpya.
Balozi
Sefue alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliamini yatapatikana
maridhiano kuhusu kubadili muundo wa Muungano, ilivyo sasa, ni wazi
kuwa maridhiano kuhusu mabadiliko hayo hayapo na
hayatapatikana. "Hakuna idadi ya makongamano na maandamano
yatakayobadili hali hiyo sasa," alisema.
Licha
ya kusema kuwa kuna matumaini ya kupata Katiba Mpya, Balozi Sefue
alisema ikishindikana Katiba iliyopo itafanyiwa marekebisho ili ituvushe
hadi mchakato utakaporejeshwa tena.
(MWANANCHI)
