Wanaharakati wamuomba Dk Shein atete na wanaCUF
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/wanaharakati-wamuomba-dk-shein-atete-na.html
Pia, wamesisitiza umuhimu wa wananchi kufuatilia Bunge Maalumu la Katiba, licha ya baadhi ya wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususa Bunge hilo.
TGNP Jana Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, alisema ni vyema wananchi wakaendelea kusikiliza kinachojadiliwa bungeni kwa kuwa hayo ni maoni yao.
Liundi alisema mjadala wa masuala ya Katiba, utaendelea kujadiliwa kwa lengo la kuhakikisha maoni ya wananchi yanasikika na kuingizwa kwenye Katiba ili kujenga Katiba, inayomthamini mwananchi na sio kikundi kidogo cha watu.
“Ni jukumu letu kufuatilia kinachojiri bungeni, licha ya Ukawa kutoka, kwani kinachojadiliwa ni maoni yetu na tunawajibu wa kusikia na kupima kama ndio tuliyopendekeza kwa lengo la kupata Katiba yenye mrengo wa kijinsia,” alisema Liundi.
ZIROP
Taasisi ya Sera na Utafiti ya Zanzibar (ZIROP) ilimshauri Dk Shein, kuingilia kati na kuzungumza na wajumbe wa CUF, kurudi katika vikao vya bunge hilo, vinavyoendea Dodoma.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Mohamed Yussuf akizungumza na waandishi wa habari, alisema Dk Shein akiwa Rais wa Zanzibar, anao ushawishi mkubwa wa kuzikutanisha pande mbili zinazotofautiana.
Akifafanua, alisema ushawishi wa Dk Shein ni mkubwa kwa sababu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa ni ya Umoja wa Kitaifa na inajumuisha mawaziri kutoka vyama vya CCM na CUF.
Alisema kitendo cha upande wa CUF kugomea Bunge Maalumu, kitasababisha Zanzibar kushindwa kupata Katiba nzuri yenye maslahi ya Wazanzibari.
“Tunamuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, kuwaita CUF kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi tatizo la kususa katika Bunge Maalumu,” alisema Yussuf.
Mjumbe wa Jumuiya ya ZIROP, Enzi Talib, alisema matatizo ya Muungano, yatamalizika kwa wajumbe hao wa Bunge Maalumu kurudi bungeni.
Alisema Zanzibar ina kero nyingi katika Muungano, ikiwemo masuala ya forodha na wafanyabiashara kutoka Zanzibar, kutozwa kodi mara mbili wakati wanapoingiza bidhaa zao nchini.
“Hayo ndiyo matatizo ambayo wafanyabiashara kutoka Zanzibar yanawakabili, ambayo jibu lake litapatikana katika Bunge Maalumu na sio nje ya bunge hilo,” alisema Talib .
Imeandikwa na Ikunda Erick, Dar na Khatib Suleiman, Zanzibar
BOFYA HAPA
