Sheikh Farid apanda kizimbani Kisutu
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/sheikh-farid-apanda-kizimbani-kisutu.html
Mtuhumiwa namba moja katika kesi ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi,
Sheikh Farid Ahmed (mbele) akiwa na watuhumiwa wenzake chini ya ulinzi
wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam jana. Picha na Venance Nestory
Pia, wanakabiliwa na shitaka la kuwaingiza watu
nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha
kufanyika vitendo hivyo.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na
Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) na
mwenzake Jamal Nooridin Swalehe (38), wameunganishwa na watu wengine 18
wanaoshtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki
katika vitendo vya ugaidi.
Pia, wanakabiliwa na shitaka la kuwaingiza watu
nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha
kufanyika vitendo hivyo.
Mawakili wa Serikali, Peter Njike, Bernard Kongola
na George Barasa wakiwasomea hati ya mashtaka hayo yanayowakabili
washtakiwa hao walidai kuwa Sheikh Farid ambaye ni mfanyabiashara na
mkazi wa Mbuyuni, Zanzibar na Fundi Ujenzi, mkazi wa Koani Zanzibar,
Swalehe walijihusisha na makosa hayo ya ugaidi kinyume na Kifungu cha
27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya 2002.
Mbali na Farid na Jamal, washtakiwa wengine
wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari
Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala,
Said Kassim, Hamis Amour, Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour,
Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe.
Walidai kuwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka
huu washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya
kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Njike alidai kuwa katika kipindi hicho na maeneo
tofauti nchini, Sheikh Farid aliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary
nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Pia Sheikh Farid anadaiwa kuwa kwa makusudi na
akijua, alitoa msaada kwa watu hao wa kutenda vitendo vya kigaidi
kinyume cha sheria. Pia anadaiwa kuwa katika kipindi hicho akiwa anajua
kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao
hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya
kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine.
Hakimu Hellen Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi
Agosti 20, mwaka huu na kuamuru washtakiwa kupelekwa rumande kwa sababu
mashtaka yanayowakabili ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, Sheikh
Farid alidai mahakamani hapo kuwa anashangazwa na kitendo cha wao
kukamatwa Zanzibar na kushtakiwa Tanzania Bara wakati hawana ndugu, baba
wala mama katika upande huo wa Jamhuri ya Muungano.
“Tunashangaa kushtakiwa huku Tanganyika wakati
Zanzibar ni nchi yenye Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu na askari watiifu tu
na kila kitu,” alisema na kuongeza kuwa wamekamatwa Aprili lakini hadi
sasa upelelezi bado haujakamilika na kuhoji ni upelelezi gani huo.
BOFYA HAPA
BOFYA HAPA