Flatnews

FCC yakamata shehena ya vipuri bandia vya magari na pikipiki


Ofisa Ukaguzi wa Tume ya Ushindani (FCC), Diana Augustino akihesabu sehemu ya vipuri vya kughushi vya pikipiki vilivyokamatwa katika duka lililopo Mtaa wa Mahiwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita. Aliyeshikilia mfuko ni muhudumu wa duka hilo, Daudi Lucas. Picha na Nuzulack Dausen 

Kazi hiyo ya ukamataji ilifanyika baada ya kuwapo kwa taarifa za uingizaji wa vipuri vya kuiga kutoka nchini China vilivyowekwa nembo ya ‘SP Original Piston Ring.’ Vipuri halisi vya nembo hiyo huingizwa hapa nchini na kampuni ya Saba General Enterprises pekee.


Dar es Salaam. Tume ya Ushindani (FCC) imekamata vipuri vya kughushi vya pikipiki vyenye thamani ya zaidi ya Sh23 milioni, katika operesheni ya kushtukiza iliyofanyika katika soko la Kariakoo jijini hapa.
Kazi hiyo ya ukamataji ilifanyika baada ya kuwapo kwa taarifa za uingizaji wa vipuri vya kuiga kutoka nchini China vilivyowekwa nembo ya ‘SP Original Piston Ring.’ Vipuri halisi vya nembo hiyo huingizwa hapa nchini na kampuni ya Saba General Enterprises pekee.
Akizungumza baada ya kumaliza operesheni hiyo, ofisa udhibiti na ukaguzi wa FCC, Emmanuel Ndyetabula alisema walikamata maboksi 7,912 ya bidhaa hizo katika duka na ghala linalomilikiwa na Anania Tweve. Kila boksi moja la vipuri hivyo huuzwa kwa bei ya jumla ya Sh3,000.
Maofisa wa FCC na polisi wa Kituo cha Msimbazi walikamata pia sehemu ya vipuri hivyo ndani ya duka lijulikanalo kwa jina la Jezetwe Motorcyle and Spare Parts lililopo Mtaa wa Nyamwezi na Mafia.
Sehemu nyingine kubwa ya vipuri ilikamatwa katika ghala la duka hilo lililopo Mtaa wa Mahiwa.
Ndyetabula alisema licha ya kuwapo na ongezeko la kubwa la uuzaji wa vipuri vya kughushi vya magari na pikipiki nchini, hii ni mara ya kwanza kwao kukamata vipuri vingi kiasi hicho kwa wakati mmoja.
“Hawa jamaa ni wajanja sana.dukani kwao wameweka bidhaa za nembo nyingine zinazofanana na SP na iwapo mteja akiulizia nembo hiyo basi hupanda juu ya dali kwenda kumchukulia. Baada ya uchunguzi na maofisa wa Saba General, tulibaini wana ghala kubwa ambalo huzihifadhi na kuziuza kwa kificho,” alisema Ndyetabula. Ofisa wa Saba General alisema mauzo ya vipuri hivyo yamekuwa yakishuka licha ya mahitaji kuongezeka.
“Baada ya kushuka kwa mauzo ilibidi timu yetu ianze kuchunguza chanzo ni nini, ndipo tukabaini kuna wafanyabiashara wanaingiza bidhaa feki kutoka China na kuziuza kwa bei ndogo,” alisema.
Alisema ili kuzitofautisha na bidhaa halisi za Sp piston ring, feki hazijaandikwa namba ya uzalishaji kwenye boksi na ndani vina rangi nyeusi badala ya rangi ya fedha. “Hivi vipuri bandia ukitumia siku tatu tu vinaanza kuvujisha moshi,” alisema.
Ofisa huyo alisema wao huuza vipuri hivyo kwa bei ya jumla ya Sh3,500 kwa boksi lakini wauzaji wanaouza bandia huuza kwa maelewano huku bei mara nyingi ikiwa kati ya Sh2,000 na Sh3,000.
Muuzaji wa duka hilo, Fadhili Tweve alisema hafahamu vipuri hivyo vilikonunuliwa bali bosi wake ndiye anayejua mchakato mzima.
Ndyetabula aliwataka Watanzania na Kampuni zinazozalisha au kufanya uwakala wa bidhaa mbalimbali nchini kushirikiana na FCC ili kutokomeza bidhaa bandia.

Post a Comment

emo-but-icon

item