EDWARD CHRISTOPHER SI KIPAJI KINACHOPOTEA, SIMBA SC IMPE RUHUSA SASA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/edward-christopher-si-kipaji.html
Mwaka 2004 nilikuwa sehemu ya wachezaji wa timu ya vijana ya Mkoa wa Morogoro chini ya miaka 17. Katika timu ya vijana chini ya miaka 12 kulikuwa na vijana wengine kibao ambao kwa sasa wanacheza ligi kuu ya Tanzania Bara. Katika kikosi hicho alikuwepo kijana Edward Christopher. Sijui ni kitu gani ambacho kinaendelea katika uchezaji wa kijana huyo mwenye kipaji kikubwa cha kufunga mabao na kumiliki mpira.
Kitu ambacho ninakikumbuka hadi hivi sasa ni namna nilivyokuwa nikiwahi katika mazoezi ya timu yangu wakati huo katika uwanja wa Morogoro sekondari ili tu kuwaona wachezaji vijana wenye vipaji ambao wakati huo walikuwa chini ya Mwalimu, Yahya Berlin ( ambaye sasa ni marehemu). Vijana hao walikuwa wakianza mazoezi yao saa nane na nusu-hadi saa tisa kwa sababu uwanja huo ulikuwa ukitumiwa na timu tatu tofauti, zikiwemo Polisi Morogoro na Jamaica FC.

Christopher alikuwa akicheza kama shambulizi wa kati lakini uwezo wake wa kukokota mpira huku akitazama sehemu anayokwenda ulikuwa ni wa kiwango cha juu mno. Nilipenda kumita ‘ Henrry’ nikimfananisha kiuchezaji na mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Thierry Henrry. Edo ana kipaji kikubwa sana cha kumiliki mpira, kukokota, kufunga mabao na kutengeneza nafasi za kufunga lakini tangu alipopandishwa katika kikosi cha kwanza cha Simba SC, katikati ya mwaka 2012 mchezaji huyo ameshindwa kutulia kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Aliporudi uwanjani msimu uliopita chini ya mwalimu Abdallah King Kibadeni na Jamhutri Kiwelo mchezaji huyo aliuonekana kupungua kiwango chake cha uchezaji huku akiingia katika mizozo ya mara kwa mara na walimu wake jambo ambalo lilimfanya kuadhibiwa mara kwa mara kwa utovu wa nidhamu. Alipokuja, Zdravko Logarusic, Christopher alipewa nafasi lakini akaendelea kucheza kwa kiwango cha chini jambo ambalo lilimfanya Logarisic kumuweka mchezaji huyo katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa kuachwa.
Christppher si kipaji kinachopotea . Kama atakamilisha usajili wake wa kujoiunga na Mtibwa Sugar mchezaji huyo anaweza kurejea kama mshambuliaji wa kutisha nchini Tanzania, ni uongozi wa Simba Tu unaotakiwa kumpatia barua yake ya kumtema ili awe huru kusajiliwa kwani baadhi ya timu zinashindwa kufanya hivyo kutokana na mchezaji huyo kisheria kuwa bado na mkataba na Simba.
Edward Christopher (kulia) akifanya vitu vyake
Kwa asiyemfahamu Christopher anaweza asigundue kipaji cha mchezaji huyo, lakini upande wangu naamini moja ya makosa makubwa ambayo Logarusic ameyafanya ni kumuacha mchezaji huyo kijana ambaye alihitaji utulivu na kujengwa kisaikolojia kutokana na matatizo ambayo amekutana nayo katika klabu ya Simba. Edo anataka kuwa huru hivyo ni vyema Simba wakampatia ruhusa ya kujiunga na timu nyingine kabla ya msimu wa usajili kufungwa ili kipaji hiki kisipotee.
Christopher alifunga ‘ hat-trick’ katika mchezo wa fainali dhidi ya Mtibwa Sugar katika michuano ya Ujirani Mwema, Agosti, 2012 wakati Simba ilipoishinda kwa mabao 5-3 katika uwanja wa Taifa. Kabla ya mchezo huo, Edo alimuahidi mlinda mlango, Shaaban Kado kuwa atamfunga mabao matatu na kweliakafanya hivyo tena akiongeza bao moja na kufanya kufunga mabao manne peke yake siku hiyo. Alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu na Simba lakini kiwango chake cha chini kiuwajibikaji kimemfanya mwalimu Logarusic kumuondoa katika mipango yake na hivyo kumruhusu aondoke.
Kwa sasa anafanya mazoezi katika klabu ya Mtibwa Sugar huku akisubiri barua ya kuvunjiwa mkataba wake na Simba kitu ambacho hakijafanyika hadi sasa hivyo kumuongezea ugumu wa kusainiwa na timu nyingine ambazo zinamtolea macho mfungaji huyo kijana. Simba inaendelea kusajili ila wanatakiwa kuwaacha kiungwana wachezaji wao na si hivi wanavyomfanyia Christopher.
0714 08 43 08
