AZAM FC YATOKA 0-0 NA RAYON SPORT KOMBE LA KAGAME, KMKM NAYO YATOKA 1-1, KCC YAICHAPA GOR MAHIA 2-1
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/azam-fc-yatoka-0-0-na-rayon-sport-kombe.html
MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc wamelazimisha suluhu tasa ya bila kufungana na wenyeji Rayon Sport katika mchezo wa pili wa kundi A kombe la Kagame lililoanza kutimua vumbi leo viwanja viwili tafouti nchini Rwanda.
Katika mechi nyingine, KMKM imetoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Atlabara ya Sudan kusini katika mchezo wa ufunguzi uliopigwa mapema katika uwanja wa Amahoro.
Wawakilishi hao wa Zanzibar walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 29 kupitia kwa Mudrik Abdullah akiunganisha kwa kichwa krosi ya Moka Msafiri, lakini beki Makame Mngwali wa KMKM alijifunga katika jitihada za kuokoa dakika chache baadaye.
Mchezo mwingine uliopigwa leo umewakutanisha KCC ya Uganda dhidi ya Gor Mahia ya Kenya na kushudia wawakilishi hao wa Uganda wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kesho Agosti 9 mwaka huu katika dimba la Amahoro mechi mbili za kundi C na moja ya kundi B zitapigwa.
Mapema itaanza mechi ya mabingwa Vital’O ya Burundi dhidi ya Benadir ya Somalia ikifuatiwa na mechi ya jioni baina ya Police ya Rwanda na El Merreikh ya Sudan.
Baadaye usiku maafande wa jeshi, APR ya Rwanda watachuana na Flambeau ya Burundi.
Azam fc watashuka dimbani tena Agosti 10 mchana kuchuana na KMKM ya Zanzibar, mchezo wa kundi A.
