DPP azidi kumbana Ponda
http://samchardtz.blogspot.com/2014/08/dpp-azidi-kumbana-ponda.html

UPANDE wa Jamhuri umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitupe ombi la Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda la kuitaka itoe amri ya kusimamisha usikilizwaji wa kesi ya msingi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, kwa sababu lina dosari kisheria.
Maombi hayo yaliwasilishwa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bernad Kongora, mbele ya Jaji Lawrence Kaduri, wakati ombi hilo lilipokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Hata hivyo, ombi hilo la msingi lilishindwa kuanza kusikilizwa kwa sababu upande wa jamhuri ulikuwa umewasilisha pingamizi la awali la kutaka litupwe, ambapo jana mahakama hiyo ilianza kusikiliza pingamizi hilo.
Ponda anaiomba mahakama itoe amri ya kusimamishwa usikilizwaji wa kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro hadi rufaa yake iliyokatwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapomalizika.
Wakili Kongora alisema kuwa wanaomba ombi hilo litupwe kwa kuwa hati ya kiapo na chemba samansi zina dosari kisheria ambazo hazirekebishiki.
Alidai kuwa mwaka 2012-2013 Ponda alishitakiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja nje na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, hakuwepo katika Mahakama ya Kisutu na sheria Na.3 ya mwaka 2011, inaelekeza wazi jinsi utaratibu wa kuandika hati za viapo.
Alidai kuwa aya ya tano na sita ya ombi hilo la Ponda anayetetewa na Wakili Nassor Juma, zina maombi ambayo hawatakiwi kuweka kwenye hati ya kiapo.
“Kwa mtazamo wa upande wa jamhuri, tunaona ombi hilo linaomba mahakama hii ifanyie mapitio kesi inayomkabili Ponda mkoani Morogoro… sasa sisi tunasema mahakama hii imefungwa mkono, yaani haina mamlaka ya kufanyia mapitio kwa sababu ya Kifungu cha 44(1)a cha Sheria ya Mahakimu na Mahakama (MCA), kwani kifungu hicho kinatoa mamlaka ya mahakama kuitisha jalada na kilikatazwa kutoka Mahakama za Hakimu Mkazi na si kama alivyofanya Ponda kulileta ombi hilo mwenyewe mahakamani,” alidai.
Hata hivyo, Kongora alidai mahakama hiyo inafungwa mkono kusikiliza ombi hilo kwa sababu tayari ombi lilishasilishwa mahakamani hapo mbele ya majaji wawili tofauti (Jaji Itemba na Augustine Mwarija), maombi ambayo yalitupwa.
“Mtukufu Jaji maombi hayo sasa tunaona Ponda ameamua kurudisha ombi hilo kwa mtindo tofauti… tunaomba litupwe,” alidai Wakili Kongora.
Kuhusu hoja ya pili, wakili huyo wa serikali alidai mahakama hiyo imefungwa mkono kutoa amri ya kusimamisha usikilizwaji wa kesi Morogoro, kwa sababu Kifungu hicho cha 44(1)a cha Sheria ya Mahakimu na Mahakama, hakitoi haki kwa mahakama kutoa amri hiyo inayoombwa na Ponda.
Kifungu hicho kinatoa haki kwa mahakama kuitisha jalada la kesi husika iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kilifanya uchunguzi na si mlalamikaji apeleke ombi mahakamani.
“Ni rai ya upande wa jamhuri kuwa mahakama itupilie mbali ombi la Ponda kwa sababu lina dosari za kisheria na mahakama haina mamlaka ya kutoa amri ya kuzuia usikilizwaji wa kesi inayomkabili Ponda, mkoani Morogoro,” alidai.
Hata hivyo, Wakili wa Ponda, Nassor Juma, aliiomba mahakama iahirishe shauri hilo ili aweze kupata muda wa kujiandaa kujibu hoja hizo.
Jaji Kaduri aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba Mosi mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya Wakili wa Ponda kujibu hoja za upande wa jamhuri.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa pingamizi hilo jana, Wakili Kongora alidai baada ya uchunguzi wamebaini hakuna rufaa yoyote iliyokatwa na Ponda katika mahakama hiyo, kwa sababu hakuwasilisha kwanza hati ya nia ya kukata rufaa mahakamani hapo, hivyo kisheria inachukuliwa hakuna rufaa iliyokatwa.
Hata hivyo, Jaji Kaduri alisema ameisikiliza pia hoja hiyo kuhusu rufaa ya Ponda, ila hataweza kuitolea uamuzi kwa sababu hawezi kusikiliza kesi mbili zilizofunguliwa na mtu mmoja.
Alisema alirejesha jalada la rufaa ya Ponda kwa jaji mfawidhi wa mahakama hiyo, ili aweze kumpangia jaji mwingine wa kuisikiliza.
Ponda aliwasilisha mahakamani hapo ombi la kuiomba mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia usikilizwaji wa kesi ya uchochezi inayomkabili mkoani Morogoro hadi pale rufaa yake aliyoikata mapema mwaka jana ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu Mei 9 mwaka jana iliyomtia hatiani kwa kosa la kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Markaz Chang’ombe, itakaposikilizwa.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA