Wanamgambo waiteka miji mingine miwili Iraq
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/wanamgambo-waiteka-miji-mingine-miwili.html
Wanamgambo wa Kisunni wamefaulu usiku wa kuamkia leo (13.06.2014) kuingia katika miji miwili ya mkoa wa mashariki wa Diyala, huku rais wa Marekani, Barack Obama, akitishia kutumia mashambulizi ya angani dhidi yao.
Wanamgambo wa kundi hilo waliuteka mji wa Mosul mapema wiki hii na tangu wakati huo wamekuwa wakisonga mbele upande wa kusini kuelekea mji mkuu Baghdad, katika harakati dhidi ya serikali inayoongozwa na Washia.
Wakurdi, ambao wana eneo lao kaskazini mwa Iraq lenye utawala wa ndani wametumia machafuko hayo kutanua himaya yao, kwa kuudhibiti mji wa mafuta wa Tikrit na maeneo mengine nje ya mpaka rasmi wa eneo lao. Vikosi vya Kikurdi vimewatuma maafisa wake wa usalama kuzilinda ofisi za chama cha siasa mjini Jalawla kabla wanamgambo kuwasili mjini humo. Hakuna makabiliano yoyote yaliyoripotiwa.
Duru za usalama zinasema jeshi la Iraq limefyetua risasi na makombora katika miji ya Saadiya na Jalawla kutoka mji ulio karibu wa Muqdadiya, na kuzilazimu familia kadhaa kuukimbilia mji jirani wa Khaniqin, karibu na mpaka na Iran.
Iraq itahitaji msaada
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq, Hoshiyar Zebari amekiri kwamba vikosi vya usalama ambavyo Marekani iliwekeza mabilioni ya dola kuwapa mafunzo na silaha, kabla kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo mnamo mwaka 2011 vimesambaratika.
Rais Barack Obama, kulia, na waziri mkuu wa Iraq, Nuri al MalikiAkizungumzia machafuko mapya nchini Iraq, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema, "Tuna wasiwasi mkubwa sana kuhusu yanayoendelea nchini Iraq na hatukai tu kuikodolea macho hali ilivyo bali tunatoa msaada. Tuna mawasiliano ya moja kwa moja na waziri mkuu Nuri al Maliki na viongozi wengine wa ngazi ya juu. Nimekamilisha mazungumzo kwa njia ya simu na watu wa Iraq na nafahamu rais wa Marekani yuko tayari kupitisha maamuzi muhimu katika kipindi kifupi. Kama alivyoweka wazi hapo awali, kuna masuala yanayozingatiwa na kwa wakati muafaka nina hakika rais atatangaza uamuzi wake."
Wamarekani wahamishwa
Afisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, amesema kampuni za Marekani zinawaondoa mamia ya Wamarekani wanaofanya kazi na serikali ya Iraq katika kambi ya jeshi la angani ya Balad, yapata kilometa 70 kaskazini mwa mji mkuu, Baghdad. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Jen Psaki, amesema kampuni zinawahamisha wafanyakazi wake katika maeneo mengine kwa sababu ya hali mbaya ya usalama katika eneo hilo.
Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema ufanisi wa wanamgambo kuyadhibiti maeneo ya Iraq kunadhihirisha uvamizi dhidi ya Iraq mwaka 2003 ulioongozwa na Marekani kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001, katika miji ya Washington na New York nchini Marekani, haukuwa na maana yoyote.
Lavrov aidha amesema kusambaratika kabisa kwa jeshi la Iraq lililopewa mafunzo na nchi za magharibi kunadhihirisha dhahiri shahiri kushindwa kabisa kwa juhudi zilizozijumuisha Marekani na Uingereza nchini Iraq.
Wapinzani wa Obama wa chama cha Republican katika bunge la Marekani walikuwa haraka kumkosoa rais huyo kwa kuiacha mkono Iraq kwa kuwaondoa wanajeshi wake mwaka 2011. Seneta Lindsey Graham ameonya iwapo wapiganaji wa Jihad huenda watachukua usukani nchini Iraq na taifa jirani la Syria, patazuka machafuko makubwa na ametaka nguvu za jeshi la angal la Marekani zitumike kubadili mkondo wa mambo katika uwanja wa vita.
