RASMI! MICHAEL WAMBURA RUFANI YAKE YAPIGWA CHINI TFF, KAMPENI KABLA YA MUDA ZAMPONZA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/rasmi-michael-wambura-rufani-yake.html
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya Michael Wambura kupinga kuenguliwa
kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye
mwezi huu.
Wambura aliwasilisha rufani yake mbele ya Kamati hiyo
iliyokutana leo (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini ya Kaimu
Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa kumwengua katika kinyang’anyiro
hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa kufanya kampeni kabla ya
muda uliopangwa.
Baada ya kupitia vielelezo, kanuni na sheria, Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya
kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l)
pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
Kwa mujibu wa ibara hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba
inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify) mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka
maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati
zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata kanuni za uchaguzi kama
zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani za mara kwa mara.
Uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF
umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na pia Katiba ya Simba.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)