MASHINDANO YA NGALAWA YANOGESHA TAMASHA LA 17 LA ZIFF 2014 VISIWANI ZANZIBAR
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/mashindano-ya-ngalawa-yanogesha-tamasha.html
Baadhi ya washiriki wa mashindano ya
resi za Ngalawa wakijiandaa tayari kwa kuanza mashindano hayo katika
shamra shamra za tamasha la 17 la ZIFF 2014 linaloendelea visiwani
Zanzibar.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
NGALAWA zote 11 zilizoingia majini
kukamilisha mzunguko wa saa mbili wa resi za ngalawa mjini Zanzibar
zilimarisha mashamshamu hayo bila najali na timu tatu zilipewa zawadi za
ushindi.
Resi za Ngalawa kama zinavyojulikana ni
utamaduni halisi wa visiwa vya pemba na Unguja na ni sehemu ya tamasha
kubwa la filamu la kimataifa la Zanzibar ambalo linaendelea visiwani
hapa.
Kwa wale waliozaliwa maeneo ya bara, resi
hizi zilikuwa kivutio kikubwa kwao kutokana na maandalizi yanayofanywa
kabla ya kuingia majini na dau kunyanuliwa.
Wakati dau limenyanyuliwa, maji yamekuwa
yakichotwa ama ndani ya Ngalawa au nje katika bahari kumwagia tanga
katika hali inayoelezwa kuliimarisha katika ukinzani wa upepo.
“mbio za Ngalawa ni kipimo kikubwa cha
Uzanzibari wetu na kila mwaka ZIFF huhitimisha utashi wake wa kuwa na
tamasha la nchi za jahazi kwa kuwa na mbio za ngalawa” alisema
mshehereshaji Muslim Nassoro Abdalla katika shamrashamra zilizofanyika
ufukweni kandoani mwa hoteli ya Tembo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia
ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo
(mwenye t-shirt ya njano) akupiliza Kipenga kuashiria kuanza kwa
mashindano hayo yaliyofanyika kwenye fukwe za Hoteli ya Tembo visiwani
Zanzibar.
Muslim ambaye alisema kwamba mwaka huu
walitaka kuwa na mbio za timu 20 (ngalawa) walishindwa kuhitimisha
ndoto hiyo kutokana na masuala nje ya uwezo wa ZIFF.
Ili kukamilisha vyema mbio hizo kunatakiwa kuwa na boti za kutosha za uokozi kama kutatokea ajali.
Mwaka juzi kulitokea ajali ambayo hata
boti ilipofanya uokozi nayo ikazidiwa na kulazimisha watu kukwama mpaka
jioni walipopata boti nyingine kutoka Bandarini.
Wakati wa mbio za resi ambazo washindi wa
kwanza ni timu iliyokuwa ikiongozwa na Hatibu Suleiman waliokuwa ndani
ya ngalawa Ipo Siku, ngoma mbalimbali za asili zilipigwa ufukoni kama
hamasa huku watu wakisubiri marejeo ya ngalawa hizo.
Baadhi ya Ngalawa zinazoshiriki mashindano hayo zikianza kukata mawimbi.
Mbio hizo ambazo zilianzishwa na mbunge
wa Kiembesamaki na Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Mahmoud Thabiti Kombo
mshindi wake wa pili alikuwa ni timu ya haji Hassan (kama nadhodha)
ndani ya ngalawa Kipanga. Aidha Hassan Simai na wenzake waliokuwa katika
ngalawa iliyoitwa peace of Love walikuwa washindi wa tatu.
Timu ya ngalawa ambayo inahitaji ujuzi
katika utekaji tanga , kulirekebisha na kubalansi ngalawa inahitaji watu
wapatao watano na si chini ya watatu.
Tamasha la filamu linaendelea mjini hapa
kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za mafunzo ya utunzi, utengenezaji wa
filamu na uhakiki wake.
Pichani juu na chini ni Sehemu ya wakazi wa Zanzibar wakishuhudia mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ( wa pili
kulia) akiwa meza kuu na mmoja wa wadhamini wa mashindano hayo Mohammed
Burudani ya Ngoma kutoka Nungwi ikitumbuiza wakati wa mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo
akionyesha moja ya zawadi t-shirt kwa watoa burudani waliokuwa
wakishindana kucheza ngoma za asili.
Mkazi wa Nungwi na Stone town (mwenye
kaptura) wakishindana kutoa burudani ya ngoma za asili za visiwani humo
wakati wa mashindano hayo.
Mshehereshaji wa tamasha la ZIFF 2014,
Muslim Nassor akimuonyesha moja ya zawadi (haipo pichani) mkazi wa Stone
town aliyekuwa akisherehesha wakati wa mashindano ya Ngalawa kwenye
fukwe za hoteli ya Tembo visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo
akikabidhi zawadi kwa mshindi wa tatu nahodha wa resi za Ngalawa iliyopewa jina la " Peace of life" M, Bw. Hassan Simai.
Mshindi wa tatu nahodha wa resi za
Ngalawa, "Peace of life" Bw. Hassan Simai katika picha ya pamoja na
mdhamini wa Ngalawa yao iliyopewa jina la " Peace of life" Mkurugenzi
mtendaji wa Zanlink, Bw. Sanjay Raja.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni
Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo
akikabidhi zawadi kwa mshindi wa pili nahodha wa resi za Ngalawa
iliyopewa jina la "Kipanga" Haji Hassan. Katikati ni mdhamini wa Ngalawa
ya Kipanga, Bi. Latifa Mohamed Omar kutoka Zan Air.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Mh. Mahmoud
Thabit Kombo akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa nahodha
mashindano ya resi za Ngalawa, Bw. Khatib Suleiman katika shamra shamra
za tamasha la 17 la ZIFF linaloendelea kutimua vumbi visiwani Zanzibar.
mshindi wa kwanza wa mashindano ya resi za Ngalawa, Bw. Khatib Suleiman (kushoto) akipongezwa na mdhamini wake mwakilishi wa Com-Net Zanzibar Bw. Mohammed (katikati). Kulia ni Mwenyekiti wa bodi ya ZIFF, Mh. Mahmoud Thabit Kombo.




