Flatnews

MAMBO SITA YATAKAYOKUSAIDIA KUJINASUA KWENYE JARIBU, TATIZO, CHANGAMOTO AU GUMU UNALOPITIA.

Mwalimu Dickson Kabigumila. Nakusalimu kwa jina kuu la Yesu Kristo, Namshukuru Mungu kunipa nafasi na muda huu kukuletea ujumbe h...


Mwalimu Dickson Kabigumila.

Nakusalimu kwa jina kuu la Yesu Kristo,

Namshukuru Mungu kunipa nafasi na muda huu kukuletea ujumbe huu wa muhimu sana, ambao amekusudia wakati na majira haya uje kwako ili ukusaidie kukuvusha na kukutoa pale ulipokwama na kukupaleka kule unakotakiwa kuwa.

KUSUDI LA SOMO
Kumuandaa Mwana wa Mungu ambaye hajaingia bado kwenye jaribu, changamoto, ugumu au tatizo
ili yatakapojitokeza hayo awe na silaha ya kumsaidia kupata ushindi na kumsaidia asikwame au kupoteza muda mwingi katika hilo.
Kumsaidia Mwana wa Mungu ambaye tayari yuko ndani ya jaribu, tatizo, changamoto au ugumu fulani na hajui namna ya kujinasua/ amekwamia hapo, na pengine kukata tamaa au kuanza kumlaumu Mungu.
Kuleta ujumbe wa matumaini uliojaa kweli za Neno la Mungu zitakazomsaidia mtu kujua kwamba Biblia yake ina majibu ya shida zake na magumu yake.
Kumuonesha mtu anayepita kwenye jaribu, changamoto, tatizo au ugumu kwamba yeye si wa kwanza walikuwepo wengine waliopita huko na kuvushwa na Mungu na hivyo hata yeye atavushwa na nguvu hizohizo za Neno la Mungu na Roho Mtakatifu.
Kila Fundisho na mbinu iliyotumika katika somo hili imethibitishwa kwa Neno la kweli la Mungu. Hivyo unaposoma ujumbe huu ujue kwa hakika yote kwamba , "MUNGU ANAONGEA NA WEWE BINAFSI" Na ni "MAELEKEZO MAALUMU KWAKO BINAFSI" Kama vile ambavyo Yesu angekuja kwako saa hii na kuongea na wewe.
Hivyo kama vile ambavyo UNGEYATENDEA KAZI KAZI MAELEKEZO YA YESU, Nakusihi kwa Jina la Yesu ukimaliza kusoma hiki kilichoko humu ndani na kupata siri hizi, anza mara moja kuzitendea kazi.
Nakukaribisha sasa tuyapitie mambo hayo sita kwa ukaribu na utaratibu, na mwisho wa siku lazima uvuke kwa Jina la Yesu;

JAMBO LA KWANZA

"Mwambie Mungu"
Hakikisha Mungu "ana taarifa", Kwa lugha nyepesi usijaribu kukaa na hilo jambo moyoni au kulitatua kwa akili zako na hekima yako binafsi. Ni rahisi kuchoka na kukata tamaa.

Biblia inatueleza kwamba tusijaribu kufanya chochote kwa akili, maarifa na nguvu zetu bali tumshirikishe Mungu mambo yetu ili NGUVU YA MUNGU iingilie kutusaidia maana VYANZO VYA MATATIZO, MAJARIBU, CHANGAMOTO NA MAGUMU MENGI hapa duniani ni vya KIROHO, Yaani vina mzizi kwenye ULIMWENGU WA ROHO. Na sisi kama "wanadamu" tuna uwezo mdogo kuyakibili mambo ya "rohoni" hivyo njia rahisi ya kuyakabili hayo mambo ni kwa "KUMWAMBIA MUNGU" Maana "ANAONA NA ANAJUA KWA UWAZI KINACHOENDELEA ROHONI"

Ninachokiongelea hapa kwa hili neno "mwambie Mungu" namaanisha, "Mweleze Mungu Kupitia Maombi" kwa uwazi na bila kuficha chochote;

Hebu tuyapitie maandiko:

"Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba na pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote itawahifadhi mioyo na nia zenu katika Kristo Yesu" (Fil. 4:6-7).

Usijisumbue kwa lolote... kuomba kutaachilia amani ya Mungu itakayohifadhi moyo wako [ili usiumizwe, kujeruhiwa, na kupata matatizo ndani yako] na pia atahifadhi nafsi yako [akili, hisia zako na maamuzi yako] hivyo utakuwa umekaa pahali pa ushindi.

"Huku mkimtwika Yeye [Yesu] fadhaa zenu [kinachowaumiza, kinachowaliza, kinachowatesa, kinachowaondolea furaha, kinachowaondolea amani, kinachowaondolea ujasiri] kwa maana Yeye [Yesu] hujishughulisha sana na mambo yenu" (1Petro 5:7).

Litakuwa ni jambo la ajabu usipomwambia Yesu "Mambo yako" au "kumtwika fadhaa" zako wakati Yeye yuko busy sana "akihangaika na kujishughulisha na mambo yako ya kila siku"... Hata kama ulikuwa umekata tamaa kuzungumza na Mungu kuhusu hilo; Rudi kwenye maombi sasa. Imekupasa kumwomba Mungu siku zote wala usikate tamaa (Luka 18:1).

"Umtwike BWANA Mzigo wako, naye ATAKUTEGEMEZA [Atakusaidia kuubeba, na atakupa nafuu]; Hatamwacha Mwenye haki [Aliyenunuliwa kwa damu ya Yesu] aondoshwe milele" (Zaburi 55:22).

Usikae na huo mzigo, usikae na hilo tatizo, usikae kimya ndani ya hilo jaribu, usinyamaze na hiyo changamoto, usikubali kufa na tai shingoni; mtwike Yesu mzigo wako kupitia maombi ya imani, naye atakutegemeza!

JAMBO L PILI

"Zungumza na nafsi yako"

Mtu ni roho, ana nafsi na anakaa ndani ya mwili.

Roho ndiye mtu halisi anayemtia uhai mtu ili awe mtu. Roho ikizima na uhai umeishia hapo. Ndiyo inayobeba thamani ya mtu na utu wa mtu.

Nafsi ni kiwanda chenye vitu vitatu; AKILI, HISIA NA MAAMUZI. Eneo hili linatawaliwa na ripoti ya MILANGO MITANO YA FAHAMU [Macho, Masikio, Ngozi, Pua na Ulimi].

Mwili ni nyumba na makao ya Roho na nafsi. Ni sehemu ya nje ya mwanadamu.

Turudi kwenye nafsi:

Nafsi ndiyo inabeba akili na hisia na maamuzi. Ni sehemu inayoathiriwa na changamoto, jaribu, tatizo au gumu unalopitia kuliko sehemu nyingine ya mtu. Akili inachoka au kukata tamaa, maamuzi yasiyo sahihi yanafanyika, na Hisia kama huzuni, maumivu vinatokea huko.


Kwenye vita dhidi ya jaribu, tatizo, changamoto au gumu unalokuwa unapitia, adui yako wa kwanza ni NAFSI YAKO; Halafu hilo unalpotia ni la pili. Hii ni kwa sababu JARIBU AU GUMU, AU CHNGAMOTO AU TATIZO Liko "nje yako" lakini "Nafsi yako" ni adui yako "ALIYE NDANI YAKO" Na mara zote kupigana na adui aliye ndani yako, anayekujua ni vita kubwa kuliko kupigana na adui wa nje.

Lengo la kipengele hiki cha pili ni kukusaidia "kumfanya adui yako nafsi" awe "upande wako" wakati wa vita badala ya kuungana na adui yako wa nje " jaribu, changamoto, gumu au tatizo unalopitia"

Na njia iliyowekwa Kibiblia ni "KUISEMESHA NAFSI YAKO" Na kuibadilishia taarifa "mbaya" ilizopokea kutoka nje kupitia "macho, masikio, ulimi, pua, ngozi"

Hapa unachokisema kinapaswa kiwe ni "habari njema" yaani "NENO LA MUNGU NA AHADI ZAKE" Ili kupangua shambulizi lililotoka nje kwenye jaribu, tatizo au changamoto yako.

Kwenye Biblia, Daudi ni mfano mzuri wa watu waliokuwa na "Ufunuo wa kuisemesha nafsi yake" , Ebu tuone baadhi ya kauli zake:

"Ee NAFSI YANGU, umhimidi BWANA. Naam vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu... Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote...." (Zaburi 103).

Hapa Daudi "ANAISEMESHA NAFSI YAKE" kuhusu matendo makuu ya Mungu wake, kwake yeye na kwa wengine alioona wametendewa hasa taifa la Israeli. Kusudi lake kubwa likiwa ni kuinua IMANI NA KUBADILI TAARIFA MBAYA kwenye nafsi yake.

Ndivyo unavyopaswa kufanya pia. Isemeshe akili yako, iambie ikubaliane na ripoti ya neno. Zisemeshe hisia zako, ziambie nini neno limesema na si kile milango mitano ya fahamu imesema.

"NAFSI YANGU yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu watoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana" (Zaburi 62)..

Hapa tunamwona Daudi ambaye "ameisemesha nafsi yake tayari" kiasi kwamba "nafsi yake imekubali kumwamini na kumtumainia Mungu" kuwa wokovu na ngome yake.

Huu ni msimamo aliotumia muda mrefu kuujenga; kadri alivyoisemesha mara kwa mara, mwishowe akafanikiwa kuitiisha na kuifanya ikubali ripoti ya Neno la Mungu kuliko ripoti ya jaribu, tatizo, changamoto au ugumu aliokuwa anaupitia.

Na wewe ukiwa kwenye jaribu, na wewe usiye kwenye tatizo au gumu, hii ndiyo kanuni... Isemeshe nafsi yako kila siku kwa ahadi na kweli za Neno la Mungu mpaka ifikie hatua ya kutii na kutoyumbishwa "kutotikiswa" na mashambulizi ya nje!!

Daudi alipoiweka nafsi yake vizuri; Alisema, "Sitatikisika sana" maana yake sitayubishwayumbishwa na kinachotoka nje, namwangalia Mungu na ahadi yake.

Mambo ya kuiambia au kuisemesha nafsi yako;
Iambie Ukuu wa Mungu wako; "Aliyemo ndani yako ni mkuu kuliko kila kitu" (1Yoh. 4:4).
Iambie (Ikumbushe) yale aliyowahi kukutendea Mungu huko nyuma [Ishuhudie nafsi yako] ; Shuhuda ni za thamani sana, kuikumbusha nafsi yako yale uliyokwishatendewa inainua imani na kuipa tumaini nafsi yako... Daudi alifanya hivyo Kwenye 1Samweli 17:32-37. Wakati anamkabili Adui wa nje [aliyeko kwenye mazingira] aitwaye Goliati. Aliikumbusha nafsi yake namna alivyomuua dubu na alivyomuua simba, nafsi yake ikakubaliana naye na kumuunga mkono kwenye vita dhidi ya Goliati. Maandiko ya ziada : Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo na kwa NENO LA USHUHUDA WAO" pia soma Zaburi 119:14, "Nimeifurahia njia ya SHUHUDA ZAKO kana kwamba ni mali mengi" ... Shuhuda ni utajiri. Shuhuda ni mali ya ajabu kwa MWAMINI zinainua nafsi yako siku ya vita. Pia soma Zaburi 119:24, "SHUHUDA ZAKO ndizo furaha yangu, na washauri wangu"... Shuhuda zina nguvu ya kurejeza furaha yako iliyopotea moyoni mwako kwa sababu ya jaribu au changamoto au tatizo ulilonalo, lakini pia zinaweza kukupa hekima ya ziada [Ushauri] wa namna ya kujikwamua kwenye hilo unalopitia.

Iambie Nafsi yako kuhusu AHADI ZA NENO LA MUNGU; "Mungu ameikuza ahadi yake [Neno lake] kuliko jina lake" (Zaburi 138:2), Lakini pia, "Mungu si mtu aseme uongo; wala si mwanadamu ajute; iwapo amesema ATALITENDA. Ikiwa amenena ATALIFIKILIZA" (Hesabu 23:19), Kumbuka, "Neno la Mungu LI HAI,tena LINA NGUVU, tena LINA MAKALI KULIKO UPANGA WOWOTE UKATAO KUWILI..." (Waebrania 4:12). Kadri unavyoiambia nafsi yako kuhusu Ahadi za Neno la Mungu, unafuta na kugeuza "taarifa mbaya" za kushindwa na kupanda "habari njema" za ushindi na kuwekezekana na mwisho wa siku, "MTEGO WA ADUI [Jaribu, changamoto, tatizo au ugumu] Utavunjika na NAFSI YAKO itaokoka" (Zaburi 124:6-7).

JAMBO LA TATU

"Zungumza na hilo jaribu, changamoto, ugumu au tatizo unalopitia"

Jambo la kwanza la msingi la kukunasua ni "Kumwambia Mungu" la pili linalofuata baada ya kumwambia Mungu ni "Kuisemesha/ kuiambia nafsi yako" na jambo la tatu la muhimu ni "Kuzungumza na hiyo hali unayoipitia"

Unapozungumza na hiyo changamoto, jaribu, tatizo au gumu unalopitia kusudi kubwa ni "KURUDISHA MASHAMBULIZI" dhidi yake kupitia "SILAHA YA MDOMO WAKO NA MANENO YAKO YA IMANI" Maana kwenye "KINYWA CHAKO NA ULIMI WAKO KUNA NGUVU YA KULETA MAGEUZI" Kama utautumia sawasawa na NENO LA MUNGU.

Tuone wenzetu walivyofanya kwenye Biblia;

BWANA YESU:

Alizungumza na MTINI USIOZAA na kuulaani ya kwamba usizae tena wala mtu asile matunda yake milele (Marko 11:12-22). Na hakika walipopita pale kesho yake [masaa 24 baadaye] walikuta "umekauka toka shinani" sawasawa na "maneno yake" ya imani. Mdomo wako una mamlaka na nguvu ya "ROHO MTAKATIFU" ya kusababisha "vyenye utasa vizae" au kila "kizaacho uharibifu" kwako na watu wako "kiwe tasa". Yatumie maneno yako yanaweza kukupa matokeo unayoyataka kugeuza hali unayopitia.

Yesu alisema, "KAZI ZOTE ALIZOTENDA TUTAZITENDA KAMA TUTAMWAMINI NA KUAMINI KWAMBA TUNAWEZA KUZITENDA" (Yohana 14:12).

Alizungumza na UPEPO NA DHORUBA iliyotishia kuzamisha chombo chao (mashua) na ikatii na kunyamaza kimya (Marko 4:35-41, Luka 8:22-25).

Nawe UKIAMINI unaweza kabisa KUISEMESHA NA KUIAMURU Kila DHORUBA NA UPEPO unaotishia ndoa yako. Unaweza KUAMURU NA KUNYAMAZISHA kila UPEPO NA MAWIMBI yanayotishia hatma na kesho ya wanao. Unaweza KUNYAMAZISHA KILA UPEPO unaotishia maisha yako. Usikubali kukaa kimya, Fungua mdomo na yatumie maneno yako kama silaha ya vita kurudisha mashambulizi dhidi ya "hiyo hali" iliyokushambulia. Usikubali KUZAMA HUKU UNAJIANGALIA. Kama Yesu angelikaa kimya, Angelizama huku akiwa na UPAKO wa kumsaidia. Una ROHO MTAKATIFU NDANI YAKO; Una upako wa kukufanya uwe mshinda na zaidi ya mshindi (Warumi 8:37), Maana, "Kama Alivyo Yesu ndivyo ulivyo wewe katika ulimwengu huu wa sasa" (1Yohana 4:17b).

Alizungumza na MAITI IITWAYO LAZARO iliyokuwa kaburini kwa SIKU NNE, INANUKA, IMEOZA mpaka IKAFUFUKA, IKATIWA NGUVU, IKATAKASIKA NA KUTOKA KABURINI NA KUISHI TENA (Yohana 11).

Kila alichofanya Yesu unaweza kukifanya endapo unamwamini na unaamini ahadi yake kwamba tutafanya yote aliyofanya na zaidi (Yohana 14:12).

Iambie kila hali ya maisha yako inayoelekea kufa au iliyokufa kwa mamlaka na imani nayo ITAKUWA HAI TENA. Ndoa yako inaweza kuinuka na kuishi tena. Watoto wako wanaweza kurekebishika tena. Mmeo/ Mkeo anaweza kuwa "mtamu na mwema" kama siku zile mlipooana. Biashara yako inaweza kuishi tena. Kila kilichokufa maishani mwako kinaweza kuwa hai endapo utayatumia maneno yako "ya ushindi" na "ya imani", Amka, amka, amka! Vita haijaisha mpaka tu pale utakaponyamaza bila kugeuza mambo kwa mdomo wako na ulimi wako uliopakwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU.

Kumbuka HAKUNA LISILOWEZEKANA KWA MUNGU (Luka 1:37, Yeremia 32:27), Lakini pia, "MAMBO YOTE YANAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE" (Marko 9:23), Ukiamini tu, "UTAUONA UTUKUFU WA MUNGU". Na kama UNAAMINI, Onesha hiyo imani yako "KWENYE MANENO YAKO" Usikubali kukalia mdomo wako; Ufungue na kuisemesha hiyo hali yako.

DAUDI ALIMSEMESHA GOLIATI (1Samweli 17):

"Wewe unanijia kw upanga, na mkuki na fumo, bali mimi ninakujia kwa JINA LA BWANA WA MAJESHI, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana... Na leo hii BWANA atakutia mikononi mwangu, nami nitakupiga na kukuua na nyama yako nitawapa ndege wa angani. Nitakuua kwa mikono yangu hii ili upate kujua ya kwamba BWANA haokoi kwa panga wala mkuki wala fumo... Nawe utajua ya kwamba VITA NI YA BWANA"

Haya ni baadhi ya maneno ALIYOSEMA DAUDI DHIDI YA JARIBU, CHANGAMOTO, TATIZO, GUMU LAKE Liitwalo GOLIATI.

Washindi wote kwenye BIBLIA yako walishinda UPINZANI ulioinuka kinyume chao kwa NGUVU YA ULIMI WAO.

Ukikaa kimya, adui yako anakuwa mkubwa na atameza imani yako. Imani ikimezwa, tayari mashaka na hofu vitazaliwa. Na hivi vikitokea, VITA ITAKUSHINDA!!

EZEKIELI ALIZUNGUMZA NA MIFUPA MIKAVU IKAWA HAI NA KUWA JESHI KUBWA KWA NENO LA BWANA (Ezekieli 37).

"Enyi mifupa mikavu kusanyikeni [Ikawa].... Enyi mifupa mikavu mfunikwe na nyama na misuli na mishipa [Ikawa]... Enyi miili iliyo na nyama na mishipa na misuli mfunikwe na ngozi [Ikawa]... Enyi miili iliyokufa na isiyo na uhai, natabiri PUMZI YA UHAI Iingie ndani yenu na mpate kuishi tena [Ikawa]..."

Haya ni baadhi ya yaliyotokea kwenye Ezekieli 37. Mwanzoni Ezekieli hakujua kwamba "ANAO UWEZO NDANI YAKE" wa "KUYAUMBA MAMBO KWA NENO LA BWANA" Lakini alipojua kwamba "HALI YOYOTE INAWEZA KULISIKIA NA KULITII NENO LA BWANA" Hapo ndipo alipolitumia KUTABIRI NA KUFANYA VITU VITOKEE.

Inawezekana nawe hujui kwamba UNAYO NGUVU ITENDAYO KAZI NDANI YAKO (Waefeso 3:20). Nikupe taarifa tu kwamba unayo NGUVU NA NEEMA JUU YAKO ya kukufanya UFANYE VITU VITOKEE. Hivyo inuka na "ITABIRIE MIFUPA MIKAVU" kwenye maisha yako, "HATUA KWA HATUA" Kama Ezekieli mpaka itakapokuwa HAI na kuwa JESHI KUBWA.

Tafadhali USIUKALIE MDOMO WAKO umebeba miujiza ya kukuvusha na kukupa matokeo. Zungumza na hiyo "hali unayopitia" kama alivyofanya BWANA YESU, DAUDI au EZEKIELI, Na NGUVU YA MUNGU itaachiliwa KUYAFANYA YATOKEE KWENYE UHALISI.

Mungu aliye hai, Baba yako wa mbinguni, ameahidi kwamba, "ATAYAUMBA MATUNDA YA KINYWA CHAKO [MANENO YAKO]" (Isaya 57:19). Usikae kimya, jiwekee mkakati wa kuisemesha hiyo "hali unayopitia" mpaka ife au ibadilike. Tumia maneno yako yana nguvu ya kukutoa kwenye mateso uliyomo!

JAMBO LA NNE

"Linda amani yako"

Utulivu wa moyo wako na nafsi yako ni wa muhimu sana katika kushinda jaribu au pito ulilonalo. Jaribu au shetani akifanikiwa kuvuruga amani yako, tayari atakushinda.

Hivyo hakikisha unaitunza amani yako kwa gharama zote ulizonazo. Usikubali kuipoteza amani yako.

Ebu tuyapitie maneno ya Mungu katika eneo hili:

"KATIKA AMANI nitajilaza na kupata usingizi wangu mara; kwa maana wewe BWANA ndiwe unijaliaye kuwa salama" (Zaburi 4:8).

Ukivurugwa na kuipoteza amani yako, HATA USINGIZI HAUTAPATIKANA maana ili mtu alale na kupata usingizi lazima awe na amani moyoni na kwenye nafsi yake [akili yake].

"Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa KWA AMANI; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi" (Isaya 55:12).

Amani ni kiongozi sahihi na wa lazima wa mwanadamu. Pale amani ilipo, akili inafanya kazi sawasawa na kuamua vema na kusababisha maendeleo na matokeo vitokee.

Mtu anayeongozwa na amani hata kama kuna majaribu [milima na vilima] maishani mwake; kwa sababu ya silaha ya amani aliyonayo, atailazimisha na kuitiisha hiyo milima na vilima VIIMBE NYIMBO KWAKE badala ya VITISHO. Mtu anayetembea na kuongozwa na amani, mwisho wake utakuwa ni kuwafanya watu [miti ya kondeni] wampigie makofi maana lazima atashinda na kumaliza kwa ushindi. Iruhusu amani ikuongoze kama unataka kushinda mwana wa Mungu.

Usiipoteze amani yako, ilinde kwa gharama zote.

"Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba na pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na AMANI YA MUNGU, ipitayo akili zote itawahifadhi mioyo na nia zenu katika Kristo Yesu" (Fil. 4:6-7).

Kama utaitunza na kuihifadhi IMANI YA MUNGU ndani yako; Hiyo amani ya Mungu ITAUHIFADHI MOYO WAKO NA NAFSI YAKO [akili yako, hisia zako na maamuzi yako] visiathiriwe na kuzuiwa kufanya kazi na hilo jaribu, changamoto, tatizo au gumu unalopitia.

Hakikisha unailinda AMANI YAKO kama kweli unataka kupata ushindi kwenye "hiyo hali mbaya" unayopitia.

MTAJI WA AMANI:

Biblia inasema Mungu, Baba yako wa mbinguni ndiye CHANZO CHA AMANI. Maadamu anakaa ndani yako, tayari unayo amani ndani yako. Ni swala la kuitunza na kuihifadhi ili adui asiibe au kuivuruga.

"MUNGU WA AMANI mwenyewe..." (1Thesalonike 5:23).

"Naye MUNGU WA AMANI atamseta Ibilisi chini ya miguu yenu upesi" (Warumi 16:20).

"Kwa maana sisi [mimi na wewe] tumepewa mtoto mwanaume; na jina lake ataitwa Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, MFALME WA AMANI..." (Isaya 9:6-7).

Yesu Kristo AMETUPA AMANI YAKE: "AMANI nawaachieni; AMANI YANGU nawapa, niwapavyo mimi ni tofauti na ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga" (Yoh. 14:27).

JAMBO LA TANO

"Tunza Furaha yako"

Biblia inatuambia waziwazi kwamba "MOYO ULIOCHANGAMKA" yaani "MOYO WENYE FURAHA" ni "DAWA BORA" bali "MOYO ULIOPONDEKA/ ULIONYONG'ONYEA UKAUSHA MIFUPA" (Mithali 17:22).

Hivyo basi, kwakuwa MOYO ULIOFURAHI NI DAWA... Ni muhimu sana mtu unapokuwa unapitia jaribu, changamoto, tatizo au gumu kuhakikisha Unatunza furaha ya moyo wako maana hiyo NI DAWA ambayo itakusaidia kupita kwenye moto "bila kuungua" na kwenye maji mengi lakini "yasikugharikishe" (Isaya 43:2).

Mungu anajua kwamba hapa duniani kuna siku za mabaya. Na ametuambia hilo kwenye Neno lake ya kuwa "Ameuumba mtu mbaya kwa ajili ya siku ya ubaya" (Isaya 54:16), Lakini anataka "TUFURAHI SIKU ZOTE" Bila kujali ni siku nzuri au mbaya!

Ebu tuyapitie maandiko:

"Furahini siku zote; tena nasema furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu" (Fil. 4:4-5).

Biblia inatutaka tuwe watu wa kufurahi siku zote [siku za mabaya au siku za mema]. Na ni kweli ni ngumu kufurahi siku ya mabaya [Kipindi cha majaribu, magumu, changamoto au matatizo] lakini NENO linatuambia inawezekana kwa kuwa "BWANA YU KARIBU" na hayuko mbali nasi.... Yuko karibu nasi kutupa furaha ya ajabu na kutupa mioyo iliyochangamka. Kwa msaada wa Bwana Yesu tunaweza kufurahi siku zote. Muombe furaha leo, naye atakupa!

"Furahini siku zote; Ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu" (1Thesalonike 5:16-18).

Mungu anapenda haya mambo matatu yawe kwenye maisha yetu daima:

-Tuwe na furaha siku zote.

Na yuko tayari kutupa furaha; ndiyo maana "aliyachukua masikitiko yetu na kujitwika huzuni zetu" (Isaya 53:4).

-Tuombe bila kukoma; Yesu anasema, "Imetupasa kuomba siku zote wala tusikate tamaa" (Luka 18:1).

-Tushukuru kwa kila jambo; Maana kila kinachotokea kwenye maisha ya MWAMINI Mungu amekikusudia kukitumia "kutupa mema" (Warumi 8:28).

Hivyo hakikisha Furaha yako haiondoki. Ilinde na kuitunza kwa gharama zote. Maana hiyo ni "dawa bora" ya kukuvusha wakati wa jaribu, ugumu, tatizo au changamoto.

JAMBO LA SITA

"Kiri Ushindi; Sawa na Neno la Mungu na si kwa kuangalia hali unayopitia"

Hii ni hatua ya ajabu sana inayokamilisha na kuuzalisha muujiza nje [kwenye macho ya nyama]. Ni hatua ya kupuuzia kile unachoona, kusikia, kuhisi, kunusa nakadhalika. Ni hatua ya kukataa ukweli, taarifa, maarifa wowote ulio kinyume na ahadi ya Neno la Mungu.

Usisahau ya kwamba, "Vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana vimeumbwa na NENO LA MUNGU na ya kuwa pasipo Neno hakuna kilichofanyika wala kitakachofanyika" (Yohana 1:1-3).

Hii ni kwa sababu, "Neno la Mungu li hai [halijafa wala si maandishi matupu au masimulizi], tena lina nguvu [kuliko kitu chochote], Lina makali kuliko upanga wowote ukatao kuwili [Ni silaha ya uhakika na ya kushinda katika vita zote]..." (Waebrania 4:12).

Hivyo hatua hii ya "kuzaa muujiza wako" inahitaji "Uenende kwa imani na si kwa kuona [milango mitano ya fahamu]" (2Kor 5:7).

Unapopuuza hilo unalopitia na "kung'ang'ana na Neno" lazima "Utarudi na Ushuhuda" Kwa maana "Neno la Mungu ni mbegu isiyoharibika" (1Petro 1:23), Hivyo lazima itoe MATOKEO.

Biblia inasema, " Maana ni heri yeye aliyesadiki; maana yatatendeka kwake yale aliyoambiwa na BWANA [Kupitia Neno la Mungu]" (Luka 1:45).

Hivyo badala ya kuzungumza kuhusu "hali ngumu au mbaya" unayopitia, zungumza kuhusu "tumaini ulilonalo" kupitia "Imani yako kwa Mungu na Neno lake"

Sema hivi:

"BWANA atafanya njia nyikani na mito jangwani... Atafanya jambo jipya sasa na nitaliona" (Isaya 43:19).

Kiri na kutabiri mabadiliko na si kuzungumza kuhusu tatizo au jaribu lako. Kiri ahadi ya Mungu kwako.

"Kwa maana MTETEZI WANGU YU HAI; Na atasimama juu ya nchi [kunitetea/ kunisaidia na kuniokoa]..." (Ayubu 19:25).

"Baada ya kupitishwa kwenye moto huu, nitatoka kama dhahabu safi" (Ayubu 23:10).

"... KUNA KUINUKA TENA. Na Mnyenyekevu Mungu atamwokoa" (Ayubu 22:29).

Ushindi hauko mbali na wewe... Lile Neno la imani liko karibu na wewe (Warumi 10:8), Kama ukilitumia na kulikiri litafanya mabadiliko yatokee!!

KWANINI KUKIRI NENO LA MUNGU:
Limeumba mbingu na nchi na vyote viijazavyo (Waebrania 11:3, Mwanzo 1), Hivyo linaweza "KUUMBA MAISHA YAKO" kwa urahisi zaidi.
Liko hai, lina nguvu kuliko "hali yoyote unayopitia" na "linajua hali unayoipitia" hivyo laweza kukunasua maana "mambo yote yako wazi kwake [Neno]" (Waebrania 4:12-13).
Ni mbegu isiyoharibika idumuyo milele (1Petro 1:23), Kila atakayethubutu "KULIPANDA" Litaota na kukua na "KUTOA MATUNDA ANAYOTAKA" maishani mwake au katika eneo anakotaka badiliko.

Ni taa ya miguu na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105)... Linaweza kukuonesha "katika ya jaribu, ugumu, changamoto" unayopitia wapi pa kupitia na wapi pa kutokea.
Ndio silaha anayoitumia ROHO MTAKATIFU Kuleta mabadiliko na matokeo tunayoyataka maishani (Waefeso 6:17).
Ndilo linalowafanya "MALAIKA WAWE HODARI [WAPATE NGUVU] YA KUTENDA MAISHANI MWETU" (Zaburi 103:20). Bila Neno la Mungu, Malaika "wanapwaya" na wanashindwa kukusaidia... Ila "WAKISIKIA SAUTI YAKO INAYOLITAMKA NENO LA MUNGU" Wanapokea nguvu kuja "Kutenda kitu maishani mwako".

HITIMISHO

Naamini Mungu amesema nawe moja kwa moja; au amekupa ujumbe unaomhusu mtu fulani unayemjua unayejua anahitaji kusikia ujumbe huu.

Hakikisha unausambaza [share] kwa wengine [marafiki] kwa wingi uwezavyo. Pamoja tunaweza kuisambaza habari njema.

MWISHO

Napatikana kwa mialiko ya kufundisha Neno la Mungu kwenye semina, makongamano, fellowship, mikesha, mashuleni, vyuoni na kila penye uhitaji.

Mungu ameniita na amewekeza ndani yangu kwa ajili ya dunia yangu.

Nitumie tuujenge Ufalme wa Mungu.

Sifungwi na Udhehebu. Ninayemtumikia ni Yesu Kristo na Mungu aliye hai aliyeniita.

Post a Comment

emo-but-icon

item