Lissu aiumbua serikali kwa uongo
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/lissu-aiumbua-serikali-kwa-uongo.html
Na Hudugu Ng'amilo
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amelitaka Bunge la Tanzania kuiwajibisha serikali kutokana na kuwadanganya wananchi.
Akichangia
bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 bungeni jana, Lissu
aliituhumu serikali kutoa takwimu za uongo ambazo hazionyeshi hali
halisi ya mambo yakiwamo mapato ya serikali huku akilisisitiza Bunge
kutimiza wajibu wake kwa kuiwajibisha.
Lissu
aliituhumu Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati na Madini kwa kutoa
takwimu za uongo bungeni kuhusu fedha za zilizotokana na fidia ya
ununuzi wa rada (chenji ya rada) na mapato yatokanayo na mauzo ya
madini.
"Jukumu
la wabunge si kuisifia Serikali, bali kuisimamia. Na katika kutekeleza
wajibu wao huo, wabunge wanapaswa kuihoji Serikali, huo ndiyo wajibu wao
kikatiba. Kuna ishara ambazo kwa maoni yangu, zinaenda kinyume kabisa
cha wajibu wetu tuliopewa na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania," alisema Lissu.
"Governments
lie and our government lies' (Serikali huwa zinadanganya na Serikali
yetu huwa inadanganya). Mheshimiwa Spika, leo (jana) asubuhi Bunge lako
tukufu limeambiwa kuwa madawati ya pesa za chenji ya rada yamegawanywa.
Madawati ya platiski ngumu 30,240 kwa halmshauri mbalimbali nchini na
madawati ya chuma 63,500," alisema.
Akijibu
swali la Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa, Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu, (TAMISEMI – Elimu), Kassim Majaliwa, alisema kuwa 2010-13
Serikali ilitenga Sh. bilioni 12.4 zilizotokana na na chenji ya rada
kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi
nchini.
Lakini
Lissu alipinga takwimu za Serikali kuhusu idadi ya madawati
yaliyosambazwa katika halmashauri mbalimbali kutokana na fedha hizo,
akisema ni za uongo.
"Tumeambiwa
jumla ya madawati 93,740 yaliyogawanywa kutokana na chenji ya rada,
imeandikiwa na ipo kwenye takwimu za Waziri Mkuu, za Serikali, halafu
anakuja waziri mdogo, anasema kwamba hatujagawa yote," alisema Lissu.
"Kama
hamjagawa yote, kwa nini mnaandika kwamba mmegawanya yote. Kwa hiyo,
mnatudanganya. Kwa nini mnadanganya wabunge, mnadanganya Watanzania?
Kwani ni ngumu kiasi gani kusema kwamba tutayagawa?" alihoji.
Aliendelea
kueleza kuwa katika mgawo huo wa madawati aliouita 'mgawo hewa', mkoa
wa Singida anaotoka haujapewa madawati 3,048 ya chuma na plastiki ngumu
kama ilivyoelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
"Katika
huo mgawo hewa, tumeambiwa kila halmashauri ya mkoa wangu wa Singida
ikiwamo halmashauri yangu ya wilaya ya Ikungi imepewa madawati 508. Jana
(juzi) sikuwa hapa bungeni, nilikwenda kwenye halmashauri yangu, hakuna
hata dawati moja lililopelekwa," alisema.
"Na
mchungaji hapa Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini-Chadema) anasema
Manispaa ya Iringa hakuna hata dawati moja lililopelekwa wakati
imeandikwa madawati 508 yamepelekwa. Mnatudanganya ili iweje?
"Tunataka
tuambiwe ukweli mheshimiwa Spika. Na waheshimiwa wabunge kweli mko hapa
kutimiza wajibu wenu au kutimiza maslahi yenu tu. Hebu hojini
halmashauri zenu zimepelekewa hayo madawati tisini na tatu elfu
yanayozungumzwa humu au ni maneno tu mnapigapiga makofi. Serikali
inatangaza, tunatakiwa tuisimamie, tunatakiwa tuihoji, tunatakiwa
tuiwajibishe," alisema Lissu.
AMVAA MUHONGO
Pia, Lissu aliituhumu Wizara ya Nishati na Madini kutoeleza ukweli juu ya mapato halisi ambayo Taifa linayapata kutokana na madini.
Pia, Lissu aliituhumu Wizara ya Nishati na Madini kutoeleza ukweli juu ya mapato halisi ambayo Taifa linayapata kutokana na madini.
Alisema
kuwa katika hotuba ya bajeti iliyowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salumu, kuna takwimu nyingi zinaonyesha kuwa nchi
haina matatizo yoyote ya kiuchumi ilhali Watanzania walio wengi wana
hali mbaya kiuchumi.
"Kwenye
hotuba ya bajeti ya mwaka huu, utadhani nchi hii hakuna shida, nchi hii
mambo mazuri, nchi hii maendeleo yapo, hela zipo na kila kitu sawa.
Lakini tunajua na Mungu anajua ni uongo, ni maneno tu," alisema Lissu na
kuongeza:
"Tumeambiwa
kwenye kitabu hiki cha Hali ya Uchumi kwamba mwaka huu wa 2013/14
tumeuza nchi za nje bidhaa mbalimbali na huduma zaidi ya dola milioni
3,700, Sh. bilioni 4,986 mheshimiwa Spika."
Alisema
takwimu za Serikali (kitabu cha Hali ya Uchumi 2013/14) zinakinzana na
takwimu zilizotolewa na Waziri wa Niashati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara
hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15.
"Tumeambiwa
katika kipindi hicho hicho cha mwaka 2013/14 mauzo ya madini nchi za
nje, kwa takwimu ya Serikali kwa mujibu wa Hali ya Uchumi mwaka huu ni
Sh. bilioni 1.790. Kwa hotuba ya waziri, hapo sasa, anasema ni dola
bilioni 1.861.
"Ukisikiliza
takwimu hizi mheshimiwa Spika utadhani kwamba hizo ni hela ni za kwetu.
Hizo hela ni za hawa wanaomiliki migodi na sisi hatumiliki migodi,"
alisema.
Akinukuu
takwimu za Wizara ya Nishati na Madini huku akionyesha kitabu cha hotuba
ya Prof. Muhongo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo
kwa mwaka 2014/15, Lissu alisema katika mwaka 2013/14 mapato ya Serikali
kutokana na madini yalikuwa Sh. bilioni 189.
"Ukitazama
kitabu hiki cha Muhongo, mapato ya Serikali kutokana na madini ni Sh.
bilioni 189, kodi mbalimbali au dola milioni 115 kwa wastani, mafunzo ni
dola bilioni 1.8 mapato ya Serikali ni milioni 114, haifiki hata
asilimia 10 ya mauzo," alisema Lissu na kuongeza:
"Sasa
ukitumia takwimu ambazo Serikali inatupa kuhusu mambo mazuri, madini ya
mabilioni mengi yanauzwa, utafikiri ni hela zetu, kumbuka hizo fedha si
zetu, ni za wawekezaji."
"Tumetunga
sheria za madini na tumetunga sheria za uwekezaji zinazosema kwamba
hawa ndiyo tuwakabidhi madini na sasa tunawakabidhi gesi waimiliki,"
alisema Lissu.
KAMATI YA BAJETI YALIPULIWA
Wakati Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge imetajwa kulipwa posho za kutisha kwa siku, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, ameitupia kombora jingine baada ya kuhoji sababu za wajumbe wake kutohudhuria kikao cha Bunge hilo jana asubuhi.
Wakati Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge imetajwa kulipwa posho za kutisha kwa siku, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, ameitupia kombora jingine baada ya kuhoji sababu za wajumbe wake kutohudhuria kikao cha Bunge hilo jana asubuhi.
Mbunge wa
Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali juzi alitoboa siri Bungeni
kwamba kila mjumbe wa kamati hiyo analipwa Sh. 500,000 wanapokuwa katika
kikao.
Mpina
alisema wajumbe kamati hiyo hawatendi haki kwa kutohudhuria vikao vya
Bunge la bajeti kwa vile kamati hiyo ni muhimu katika upitishaji wa
bajeti hiyo.
"Tunajadili
bajeti, lakini wajumbe wa Kamati ya Bajeti hawamo humu bungeni, wako
kwenye vikao vyao. Tunapangaje ratiba za namna hii mheshimiwa Spika?
alihoji.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, hakujibu hakusema chochote juu ya utoro wa wajumbe hao jana mchana.
Aidha,
Mpina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na
Biashara, aliitaka Serikali kuweka wazi taasisi na watu waliotumia Sh.
trilioni 9.36 zilizoongozeka katika Deni la Taifa ndani ya miezi tisa.
"Deni la
Taifa ndani ya miezi tisa tu limeongezeka kwa Sh. trilioni 9.36 na
inaelezwa kwamba sababu za kuongezeka ni mikopo mipya na kulipa madeni
mengine. Tunataka, kabla ya kuunga mkono hoja tuambie fedha hizo
zilienda kwenye wizara gani," alisema Mpina.
Mpina pia
alikosoa matumizi ya dola ili kulinda ushindani wa Shilingi ya Tanzania
akisema kuwa Serikali imeyaruhusu bila sababu za msingi.