KUTOKA BRAZIL 2014: Ronaldo analisha walala nje wa mitaani
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/kutoka-brazil-2014-ronaldo-analisha.html
- Staa wa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima anashirikiana na Serikali ya Brazil katika mpango maalumu wa kuwalisha watu wote wanaolala nje katika mitaa ya Brazil kutokana na umaskini uliosababisha ukosefu wa makazi.
Staa wa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima
anashirikiana na Serikali ya Brazil katika mpango maalumu wa kuwalisha
watu wote wanaolala nje katika mitaa ya Brazil kutokana na umaskini
uliosababisha ukosefu wa makazi.
“Hao jamaa wanaolala nje usiwaone hivyo, wanakula
vizuri kuliko baadhi ya Watanzania waliokuja kutafuta maisha hapa. Kuna
gari maalumu linapitia kuwaletea Wali, Nyama, Chips, Matunda, Kuku na
kila aina ya chakula kizuri.” Ananiambia Mtanzania huyo wakati tukikata
mitaa huku akiomba nisimtaje jina.
“Wamewekewa hoteli yao ambayo wanaweza kwenda kula
bure, lakini wenyewe tu wamekuwa wavivu. Wakilala hawataki kuamka
kwenda kula na ndiyo maana badala yake huwa wanaletewa vyakula.”
“Kuna hoteli nyingine wanaweza kwenda kula chakula
na kulipa Rias moja tu kwa sahani. Ronaldo ndiye anashirikiana na
Serikali katika mpango huo maalumu na kuna siku nyingine yeye mwenyewe
huwa anatembea mitaani kugawa chakula hicho.” Jioni ya siku hii hii
ninayopata habari hii ndio napata bahati ya kuona wimbo mmoja wa kundi
la wanamuziki wa Brazil huku staa mwingine wa zamani wa Brazil,
Ronaldinho akiimba. Naambiwa kuwa ndio kazi yake kubwa siku hizi. Mambo
ya mpira amepunguza kwa kiasi kikubwa na badala yake mbwembwe zake
amezidisha nje ya uwanja.
Ronaldo anaonekana kuwa bize na masuala ya Jamii,
lakini inadaiwa kuwa Ronaldinho yuko bize kweli kweli na masuala ya
starehe na ndiyo maana licha ya urafiki wa muda mrefu na kocha Fillipe
Scolari, lakini alimwambia mapema kuwa hatamchukua katika fainali za
kombe la dunia.
Anachofanya Ronaldinho ni kuongeza mauzo ya
wanamuziki wa Brazil kwa kuimba vipande vya nyimbo zao huku akionekana
katika video na nyimbo nzima inapata mvuto. Kazi hiyo pia anaifanya staa
mwingine wa zamani wa Brazil, Adriano.
Kitu kinachovutia kutoka kwa mastaa wa Brazil ni
ukweli kwamba wanapomaliza maisha yao ya soka Ulaya na kwingineko wote
huwa wanarudi zao nyumbani kula raha. Ni tofauti na mastaa wa Afrika
ambao wengine wanaamua kubaki Ulaya, hasa wale ambao mataifa yao
yalitawaliwa na Wafaransa.
