Kesi ya Liz yaanza kusikilizwa Kenya
http://samchardtz.blogspot.com/2014/06/kesi-ya-liz-yaanza-kusikilizwa-kenya.html
Kesi dhidi ya mshukiwa mmoja wa
ubakaji aliyekuwa miongoni mwa genge la watu waliombaka msichana mmoja
kwa Jina Liz mwaka jana ,na kumtupa ndani ya shimo, inaanza kusikilizwa
leo.
Mshukiwa huyo alikuwa mmoja wa watuhumiwa ambao
polisi waliwapa adhabu ya kukata nyasi kwa kitendo cha ubakaji na kisha
kuachiliwa.Mnamo Jumatatu mamia ya wanawake waliandamana mjini Busia ambako kesi hiyo inafanyika wakiunga mkono haki kwa Liz huku kesi hiyo ikianza kusikilizwa.
Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopinga dhuluma dhidi ya wanawake, uliongoza waandamanaji ambao baadaye walikusanyika katika kituo cha mkuu wa jimbo, Isaiah Nakoru.
Walimkabidhi mkuu huyo nyaraka zilizotiwa saini kutaka Liz atendewe haki.

Wanaharakati waliandamana wakitaka Liz kutendewa haki
Viongozi wa maandamano wanasema kuwa idadi kubwa ya wasichana waliobakwa tangu kusikika kwa kisa cha Liz wamekuwa wakienda kuwashitaki watuhumiwa kwa polisi.
Liz alibakwa na wanaume sita ambao walimuwacha na majeraha mabaya kwenye mwili wake kiasi cha kulazwa hospitalini kwa miezi kadhaa.
Mamake Liz alikuwa miongoni mwa waandamanaji.
