WAATHIRIKA WA MAFURIKO KYELA WALILIA MISAADA
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/waathirika-wa-mafuriko-kyela-walilia.html
.Mkuu wa
Wilaya Kyela Margareth Esther Malenga(kulia)akipokea msaada wa
vyandarua kupitia chama cha Msalaba Mwekundu"Redcross"kwa niaba ya
wahanga wa mafuriko wa wilaya hiyo toka kwa Mkuu wa Vodacom Tanzania
nyanda za juu kusini Bw.Macfyden Minja,anaeshuhudia kushoto ni Mkuu wa
Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule. Jumla ya shilingi Milioni 10
zimetumika kwa misaada mbalimbali kwa wahanga wa mafuriko wilayani humo.

Mkuu wa
Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule,akizungumza na baadhi ya
wanafunzi wa shule ya Msingi Kajunjumele iliyopo wilayani Kyela
iliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni,alipotembelea shule
hiyo mara baada ya kukabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya
shilingi Milioni 10 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo(hayupo pichani)kwa niaba ya
wahanga wa mafuriko wilayani humo.
Mkuu wa
Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule,akiingia kwenye moja ya darasa
lililoathirika na mafuriko hivi karibuni katika shule ya Msingi
Kajunjumele iliyopo wilaya ya Kyela,alipotembelea shule hiyo mara baada
ya kukabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya shilingi Milioni 10 kwa
Mkuu wa Wilaya hiyo(hayupo pichani)kwa niaba ya wahanga wa mafuriko
wilayani humo.
Mkuu wa
Wilaya Kyela Margareth Esther Malenga(katika)akiongozana na Mkuu wa
Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule na Mwenyekiti wa chama cha
Msalaba Mwekundu"Red Cross"Mkoa wa Mbeya Bw.Ulimboka Mwakilili,wakikagua
maeneo yaliyoathirika na Mafuriko wakati walipokwenda kukabidhi msaada
wenye thamani ya Shilingi Milion 10 kwa wahanga wa mafuriko wilayani
humo.
---
Na Mwandishi Wetu, Kyela.
Mkuu wa
Wilaya ya Kyela Bi. Margareth Esther Malenga, amesema kuwa Waathirika wa
Mafuriko wilayani kyela bado wanahitaji misaada na huduma nyingine za
kijamii kutokana na athari kubwa waliyoipata kutokana na mafuriko
yaliyotokea wilayani humo siku chache zilizopita.
Mkuu huyo
wa Wilaya ametoa wito kwa jamii ya Watanzania kujitolea kuwachangia
wahanga hao ambao bado wako katika mazingira magu,u licha ya jitihada
zilizofanywa na Serikali na kushirikiana na wadau wengine, kama Msalaba
Mwekundu "Red Cross" katika kuwasaidia wahanga hao.
Akizungumza
wakati wa kupokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka Vodacom Foundation
yenye thamani ya Shilingi Milioni 10, iliyotolewa na kampuni hiyo kwa
Shirika la Msalaba Mwekundu na kukabidhiwa kwake kwa niaba ya wahanga
hao.
"Tumefarijika
kupokea misaada hii, kutoka kwa Vodacom lakini bado, tunahitaji misaada
zaidi wahanga hawa walipoteza kila kitu pamoja na mazao yao kuharibika
hivyo misaada ya kijamii bado inahitajika, hata wengi mnaweza kuangalia
hata mazingira ya shule yetu ya Kajunjumele ilivyo katika hali mbaya
kwa sasa" alisema Bi. Malenga.
Wilaya ya
Kyela ni moja ya maeneo yaliyoathirika na mvua nyingi zinazoendelea
kunyesha kwa mwaka huu na kusababisha maafa makubwa kwa kusababisha vifo
vya watu saba na kuathiri kaya 3,983 zenye zaidi ya watu 18,976 idadi
ambayo imetajwa kuwa ni kubwa.
Kutokana
na athari hizo familia nyingi zimeachwa bila ya mahitaji muhimu ya
binadamu kama vile chakula na malazi hali ambayo inahitaji msaada wa
haraka kutoka kwa serikali na jamii kwa ujumla ili kunusuru maisha ya
waathirika na kuwafanya waishi maisha yao kama awali.
Akizungumza
punde baada ya kukabidhi msaada huo kutoka kwa Vodacom Foundation,
Mwenyekiti wa chama cha Msalaba Mwekundu"Red Cross"Mkoa wa Mbeya
Bw.Ulimboka Mwakilili,, amepongeza hatua hiyo kwani ni mara ya pili kwa
kampuni hiyo kufanya hivyo ambapo awali walisaidia shirika hilo kwa
waathirika wa mafuriko mkoani Morogoro.
"Kwa mara
nyingine tena tunashukuru kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania
kwa msaada huu kwani walishafanya hivyo kwa waathirika wa mafuriko
mkoani Morogoro. Leo tumepokea msaada wa vifaa kama mablanketi, magodoro
pamoja na vyandarua vya kujikinga na mbu, msaada huu unagharimu
shilingi milioni kumi, " alisema Ulimboka, na kuongeza kuwa, "Msaada huu
utatumika kama ulivyokusudiwa na si vinginevyo, kwa kweli ni matumaini
mapya kwa familia zilizoathirika wilayani Kyela."
Ulimboka
alisisitiza kuwa tofauti na miaka iliyopita mvua za mwaka huu zimenyesha
kwa wingi na kuacha maafa makubwa, hivyo wao kama msalaba mwekundu
wanaowajibu wa kutoa msaada wa haraka. Shirika peke yake haliwezi lakini
linaamini kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali nchini watafikia lengo.
"Napenda
kutoa wito kwa makampuni, mashirika na taasisi nyingine kutoa msaada kwa
watanzania wenzetu waliokumbwa na maafa haya. Familia hizi ambazo
baadhi zimeondokewa na wapendwa wao, makazi, vyakula na mali nyingi,
yatupasa tufikirie wenzetu hawa wanaoshindwa kujihusisha na shughuli za
uchumi kwa kutokuwa na makazi pamoja na malazi maalum." Alihitimisha
Ulimboka.
Aidha,
Mkuu wa Vodacom Foundation, Yesaya Mwakifulefule amesema kuwa msaada
wanaoukabidhi ni jitihada za wafanyakazi na kampuni kwa ujumla katika
kuhakikisha kidogo walichokuwa nacho wanashirikiana na watanzania wenzao
walio katika hali ngumu hivi sasa.
"Msaada
huu unajumuisha mablanketi 200 ambapo kila familia itapatiwa mawili ili
kuwalinda dhidi ya hali mbaya ya hewa iliyochochewa na makazi yao au
kutokuwa na makazi kabisa. Pia tunakabidhi magodoro 200, kila familia
itapatiwa moja, magodoro haya yatasaidia malazi kwa familia ambazo zina
mazingira magumu. Mbali na hapo pia vyandarua 100 vitagawiwa kwa
waathirika hawa kuwakinga na mbu na hatimaye kujikinga na maambukizi ya
malaria." Alisema Mwakifulefule
Mwakifulefule
alihitimisha kuwa kwa niaba ya Vodacom angependa kutoa pole kwa
waathika wa mafuriko hayo na kuwataka wasife moja watanzania wenzao wapo
bega kwa bega nao kuhakikisha wanasaidiwa kuikabili hali inayowakumba.
Pia ametoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano wa Shirika la Msalaba
Mwekundu kwa kuwa mstari wa mbele kujitolea kusaidia kila watanzania
wanapopatwa na matatizo. Wao kama kampuni wapo tayari muda wote
kushirikiana nao na wasisite kuwafuata pindi wanapohitaji msaada.
Mafuriko
hayo katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya yalitokea mwezi wa Aprili mwaka
huu na kulingana na takwimu zilizofanyika watu saba walipoteza maisha
huku watu 1,087 ambao ni sawa na kaya 235 walipelekwa katika kambi 14
zilizokuwepo shuleni na makanisani.
Familia
hizo zinahitaji msaada wa haraka wa chakula, malazi pamoja na msaada wa
huduma za kiafya ambazo ni muhimu kulingana na mazingira magumu
wanayoishi.