UKAWA WATOA MASHARTI MAGUMU KUSHIRIKI UCHAGUZI 2015
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/ukawa-watoa-masharti-magumu-kushiriki.html
Serikali
imetakiwa kuandaa taratibu za mpito za kushughulikia Uchaguzi Mkuu ujao
ili kunusuru nchi kuingia katika mtanziko unaoweza kuwa chanzo cha
machafuko ya kisiasa, endapo utafanyika bila kupatikana kwa Katiba Mpya
la sivyo Kambi Rasmi ya haitashiriki.
Hayo
yalielezwa jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe alipokuwa akitoa hotuba ya kambi hiyo bungeni kuhusu Makadirio ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Hatuwezi
kuingia uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa kwa utaratibu uliopo
leo, hatuwezi kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani na Tume ya Uchaguzi
kama ilivyo leo, hatuwezi tena kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani
wakati matokeo ya uchaguzi wa Rais hayawezi kuhojiwa mahakamani.”
Aliongeza:
“Hatuwezi kuingia kabla na hoja ya mgombea huru haijapatiwa majibu,
tukiwa na daftari la wapigakura lililopo leo na hatuwezi kulikubali
daftari jipya litakalotengenezwa kama wadau wote hatutashirikishwa
kikamilifu.”
Kauli
hiyo ya Mbowe imekuja siku moja tu baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kuwasilisha bungeni, Bajeti ya ofisi yake ambayo imetenga Sh5 bilioni
kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika baadaye
mwaka huu.
Mbowe
alisema kama ilivyo kawaida, Serikali na CCM inaweza kupuuza tahadhari
hizo na kulazimisha kwenda katika chaguzi hizo katika mazingira ambayo
hayana mwafaka kama inavyoonekana sasa katika Mchakato wa Katiba Mpya.
Ukawa haitarejea bungeni
Katika
hotuba hiyo iliyobezwa na wachangiaji wa CCM kuwa imezungumzia Katiba
badala ya Bajeti, Mbowe alisema wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), hawatarejea katika Bunge la Katiba mpaka watakapohakikisha kuwa
maana halisi ya uwepo wa Bunge hilo unafuatwa.
Alisema
kama lengo ni kutumia mwavuli wa Bunge Maalumu la Katiba ili kuendeleza
mfumo wa kikatiba na muundo wa muungano uliopo sasa, wajumbe wa Ukawa
hawatakuwa sehemu ya usaliti huo kwa Watanzania.
“Kama
kitakachojadiliwa katika Bunge la Katiba kitalenga kuboresha matakwa ya
wananchi kama yalivyodhihirishwa katika Rasimu ya Katiba na taarifa za
tume, wanachama wa Ukawa watakuwa tayari kurudi kwenye Bunge Maalumu la
Katiba ili kuendelea na mjadala wa rasimu,” alisema Mbowe.
Ofisi ya Rais
Mbowe
alisema kati ya wajumbe 201 wa Bunge la Katiba walioteuliwa na Rais
Jakaya Kikwete, zaidi ya wajumbe 160 ni wanachama wa CCM.
Alisema
hofu ya Kambi ya Upinzani kwamba CCM ingetumia mamlaka ya Rais katika
uteuzi wa wajumbe wa bunge hilo, sasa imedhihirika wazi.
Alisema
wajumbe hao walichomekwa kwenye Bunge Maalumu kwa kutumia kivuli cha
waganga wa jadi, taasisi za kidini, asasi za kiraia, taasisi za
kitaaluma na watu wenye malengo yanayofanana.
“Hatua hii imechangia kujenga mazingira ya kutokuaminiana na hivyo kuweka msingi mbaya wa mchakato husika,” alisema.
Alisema
hata lilipoanza Bunge la Katiba, CCM iliendelea kufanya hila za
kuchakachua kanuni za Bunge la Katiba ili kupitisha hoja zao kirahisi.
“Walipoona
wamekwama walimtumia Mwenyekiti wao Taifa (Rais Kikwete) ambaye
alitumia kivuli cha urais kusisitiza msimamo wa CCM na kutisha wajumbe
wa Bunge la Katiba kwamba kama ukipita muundo wa serikali tatu jeshi
litapindua Serikali,” alisema Mbowe.
Alisema
Rais Kikwete ndiye aliyebariki uandikaji wa Katiba Mpya Desemba 2010,
lakini hivi sasa anaongoza mawaziri wake, viongozi waandamizi, wabunge
na wajumbe wa CCM kujadili Rasimu ya Katiba kwa kutukana, kudharau,
kubeza, kuzomea na kushutumiana.
Alisema
kitendo hicho kinathibitisha kauli zilizowahi kutolewa na aliyekuwa
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kwamba Serikali ya CCM haioni haja
ya kuwa na Katiba Mpya kwani iliyopo sasa inatosha.
MWANANCHI
