Flatnews

TEMBO WA IVORY COAST WALIVYO NA DENI KUBWA KATIKA FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA 2014

  Laurent Pokou Prudent


Foot_Laurent_Pokou_5da73.jpg
 Laurent Pokou Prudent



Pamoja na nyakati za akina  Laurent Pokou, Youssouf Fofana na Joel Tieh kuwa maarufu katika historia ya usakataji kabumbu katika soka ya ndani ya bara la afrika enzi hizo, mpaka wanastaafu soka wachezaji hao wala hawakuiwezesha timu yao ya Taifa kucheza fainali za kombe la dunia.

Ndiyo maana mpaka leo hii wachezaji hao wala hawajulikani na wapenzi wa soka wa nje ya Ivory Coast nadhani kutokana na ukweli huu wa kutoifikisha timu yao hiyo katika Mashindano makubwa yenye kushindanisha mataifa mbalimbali.(FS)


Ni wazi kuwa umaarufu wa wachezaji hao kamwe hauwezi kuuzidi umaarufu wa kikosi cha sasa cha Ivory Coast. Jina la nahodha wa sasa wa kikosi hicho Didier Drogba pamoja na wachezaji wengine kama akina Yaya Toure, Kolo Toure, Didier Zokora, Gervinho, Solomon Kalou ni miongoni mwa majina machache kati ya mengi yanayokipamba kikosi cha sasa cha Tembo hao wa Afrika.

Lakini Je, Umaarufu huu wa akina Drogba katika Ivory Coast ya leo una tija yoyote kwa Taifa hilo? Ni wazi kuwa swali hili linawaumiza wachezaji wengi wa nchi hiyo huku wengi wao wakionekana kuwa na deni kubwa, deni la kuwapa raha mashabiki wa nchi yao kwa kufika mbali katika fainali za mwaka huu 2014 na ikiwezekana kuutwaa ubingwa huo.

Ivory Coast ya akina Drogba imefanikiwa kucheza fainali mbili za Mataifa ya Afrika yaani mwaka 2006 na 2012 lakini kwa bahati mbaya haikufanikiwa kutwaa ubingwa huo, vivyo hivyo katika fainali za kombe la dunia imeshiriki mara mbili katika miaka ya 2006 na 2012 lakini iliishia katika hatua za makundi.

Hii ni kumbukizi yenye kuumiza moyo kwa kizazi cha sasa cha Taifa hilo linaloonekana kuwa na nyota ya kupendwa sana na mashabiki wa soka wa ndani ya bara la Afrika, hii inatokana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi kazi hicho.

Leo hii kama utaambiwa uitaje timu kutoka bara la Afrika ambayo ina kila sababu ya kufika mbali katika fainali hizi za kombe la dunia, hapana shaka wadau wengi wa soka wataitaja timu ya Taifa ya Ivory Coast.

Lakini Kikosi kazi hicho kinachonolewa na Kocha Sabri Lamouchi kutoka nchini Ufaransa, mbali na kupewa nafasi kubwa katika fainali hizi kimeonekana kutokuwa na bahati katika mashindano ya miaka ya karibuni kitu kinachowapa wasiwasi mkubwa mashabiki wengi wa timu hiyo.

Kitendo cha kutolewa katika hatua za makundi za fainali zilizopita kinaonekana kuwapa hasira zaidi wachezaji wanaounda kikosi hicho kinachoongozwa na nahodha wao Didier Drogba ambapo tangu aanze kukitumikia kikosi hicho cha Taifa amekwisha ingia nyavuni mara 63 na kuwa kinara wa ufumaniaji nyavu kwa sasa.

Ni wazi kuwa kikosi hicho chenye nyota wengi akiwemo mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi Didier Zokora (mechi 118) kinakwenda nchini Brazili kikiwa na kumbukizi yenye kuhuzunisha sasa, kumbukumbu ya kutokuwa na bahati katika mashindano hayo makubwa na maarufu duniani kote.

Ivory Coast yenye mchezaji bora wa Afrika Yaya Toure inakwenda nchini Brazili huku ikiwa katika nafasi nafasi ya 21 katika ubora wa viwango vya FIFA vya sasa huku ikiwa na shehena ya wachezaji wenye heshima kubwa katika pande zote za dunia.

Historia inaonesha kuwa Tembo hawa wamekuwa hawafanyi vizuri katika fainali hizi kwa sababu ya makundi ambayo wamekuwa wakipangwa yaani makundi ya kifo na hivyo kujikuta wakiishia katika hatua ya makundi.

Ikumbukwe kuwa Mwaka 2006 kwenye fainali zilizopigwa nchini Ujerumani, Ivory Coast ilipangwa na nchi za Argentina, Uholanzi, Serbia na Montenegro na kumaliza kwenye nafasi ya tatu kama walivyofanya hivyo kwenye fainali za mwaka 2010 nchini Afrika Kusini ambapo walipangiwa timu za Brazil, Ureno na Jamhuri ya Korea.
 
Katika fainali za mwaka huu, Ivory Coast ipo katika kundi C pamoja na timu ya taifa ya Colombia, Ugiriki na Japan huku wachambuzi wengi wa soka wakiweka bayana kuwa bado kundi hili ni gumu kwa timu ya Ivory Coast na huenda kwa mara nyingine tena wakajikuta wakiishia kwenye hatua ya makundi.

Mtazamo huu kwa kiasi fulani unaonekana kupingwa kinaganaga na wadau wengine wa soka wanaoamini kuwa kundi la mwaka huu (2014) litakuwa jepesi zaidi kwa Tembo hawa ukilinganisha na makundi ya fainali zilizopita.

Uimara wa kikosi hiki cha Sabri Lamouchi unatokana na kusheheni wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya, mfano ni washambuliaji wake mahiri Didier Drogba na Solomon Kalou ambao wanaunda ‘kombinesheni’ nzuri pale mbele, viungo kama Didier Zokora na Yaya Toure ni wachezaji muhimu pia kwa timu hii.

Ina washambuliaji wa pembeni wenye majina makubwa wakiongozwa na Gervinho huku himaya ya ulinzi ikiwa na akina Emmanuel Eboue na Kolo Toure ambao ni miongoni mwa wachezaji tegemezi katika kikosi cha Mfaransa huyu.

Kwa kikosi hiki chenye mafundi wa kila idara, ni wazi kuwa akina Drogba na wenzake wana deni kubwa kwa nchi yao ya Ivory Coast lakini pia kwa bara nzima la Afrika.

Jina la timu hiyo ‘Tembo wa Afrika’ linazidi kuchagiza zaidi ari ya kuliwakilisha vema bara hili ambapo tangu kuanza kwa Mashindano haya ya dunia mwaka 1930 hakuna nchi ya Afrika iliyowahi kuchukua ubingwa huo.

Hapana shaka fainali hizi huenda zikawa za mwisho kwa nahodha Didier Drogba mwenye umri wa miaka 36 kwa sasa, lakini pia chochote kinaweza kikatokea kwa akina Yaya Toure (miaka 31), Kolo Toure (miaka 33) na Didier Zokora (miaka 34) ambao umri wao unawalazimisha kuifanyia makubwa nchi yao katika fainali za mwaka huu 2014. MUNGU IBARIKI AFRIKA……

Post a Comment

emo-but-icon

item