Homa ya Dengue Yaibua Tafrani Jijini Dar
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/homa-ya-dengue-yaibua-tafrani-jijini-dar.html
TAARIFA
isiyo sahihi ya maambukizi ya homa ya dengue inayoenezwa na mbu aina ya
aedes, imesababisha baadhi ya madereva teksi jijini Dar es Salaam,
kujilinda kwa kuvaa glovu za mikononi, soksi ndefu miguuni na kujifungia
muda wote katika magari yao hata ambayo hayana viyoyozi.
Uchunguzi wa gazeti hili wiki hii, umebaini
madereva hao wamekuwa wakivaa soksi miguuni hata kama wamevaa
kandambili, huku wakiwa na glovu viganjani kwa madai kuwa wanaogopa
kuumwa na mbu mwenye virusi hivyo.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya
madereva wa kituo cha mtaa wa Mindu Upanga, walikiri kuvaa mavazi hayo
kujikinga na ugonjwa huo ambao hauna tiba.
“Kwa kweli ugonjwa huu ni hatari kama
hauna
tiba , unafikiri tutapona kweli, ni heri tuvae hivi, au tujifungie
ndani ya gari wakati tunasubiri wateja,” alisema Juma Hassan mmoja wa
madereva teksi hao.
Hassan alimruhusu mwandishi kuzungumza naye
akiwa amejifungia ndani ya gari huku jasho likimtoka na kulowanisha
shati lake, kwa hofu kwamba akifungua madirisha, mbu wataingia na
kumwambukiza ugonjwa huo.
Baraka Joseph dereva teksi wa kituo
hicho, yeye alikuwa amevaa koti na miguuni amevaa soksi pamoja na
kandambili, na alisema taarifa alizonazo zinaonesha ugonjwa huo unatisha
kwani unaua muda mfupi na hauna tiba, hivyo sio ugonjwa wa kuudharau
hata kidogo.
“Ugonjwa huu unatisha na tumesikia
hapa mjini watu wengi wameupata, sasa kazi yetu hii tuko vijiweni tangu
alfajiri hadi muda huu (saa mbili usiku), ni lazima tujikinge vinginevyo
tutautapa na hatujui kama tutapona,” alisema Joseph.
Hali kwenye kituo cha kona ya
Muhimbili, ambako taksi huwa zinapaki hapo, ilikuwa tofauti ambapo
kulikuwa na dereva mmoja tu, ambaye naye alisema wenzake wameondoka kwa
kuwa maeneo hayo kuna mbu wengi wanahofu ya kuumwa na kupata homa ya
dengue.
“Nimebaki mimi ,lakini hata hivyo
naondoka, nimejipaka dawa ya kuzuia mbu ila bado nina wasiwasi huenda
mbu mwenye virusi hivyo akaniuma nikaupata, sasa itakuwa shida, kwa
kweli ugonjwa huo unatutisha,” alisema Rashid Muhammed, ambaye ni dereva
wa teksi eneo la Kona ya Muhimbili.
Wakati huo huo, Mkoa wa Shinyanga
ulijikuta ukilazimika kukanusha uvumi ulioenea kuhusu kulipuka kwa
ugonjwa wa dengue, baada ya kulazwa kwa mgonjwa mmoja mwenye viashiria
vya ugonjwa huo katika hospitali ya mkoa.
Akizungumza na gazeti hili ofisini
kwake mjini hapa jana Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk
Ntuli Kapologwe, alikanusha kulipuka kwa ugonjwa huo mkoani hapa, baada
ya vipimo vya mgonjwa huyo vilivyopelekwa Dar es Salaam, kubaini hana
ugonjwa huo.
“Ni kweli mtoto aliyelazwa katika
hospitali ya mkoa alikuwa na viashiria vya kuambukizwa ugonjwa huo vya
uchovu, kuishiwa nguvu, kutokwa na damu puani na homa kali, lakini
hakuwa na ugonjwa wa dengue kwa kuwa vipimo vyake kuonesha anasumbuliwa
na ugonjwa mwingine ambao unatibika kwa tiba sahihi,” alisema Dk
Kapologwe.
Uvumi kuhusu kuibuka kwa ugonjwa huo,
ulisababisha mkanganyiko uliowakumba baadhi ya wagonjwa waliofikia
hatua ya kutaka kukimbia wadini ili kunusuru maisha yao wakihofia
kuambukizwa ugonjwa huo.
Dk Kapologwe alisema, ili
kuthibitisha kuwa mgonjwa aliyefika hospitali kupatiwa matibabu
anasumbuliwa na maradhi ya dengue, ni lazima vipimo vyake vipelekwe
kwenye Maabara Kuu jijini Dar es Salaam na majibu ya vipimo yathibitishe
kuwa kweli mgonjwa huyo ameambukizwa ugonjwa huo.
Akizungumzia kinga ya ugonjwa huo, Dk
Kapologwe aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuchoma na
kuangamiza mazingira yanayoweza kuwa chanzo cha mazalia ya mbu ambao
husababisha ugonjwa huo
