BAADA YA UKIMYA WA MUDA SASA HAYA NDIO MAPYA KUHUSU NDEGE YA MALAYSIA ILIYOTOWEKA ANGANI
http://samchardtz.blogspot.com/2014/05/baada-ya-ukimya-wa-muda-sasa-haya-ndio.html
Waziri
Mkuu wa zamani wa Malaysia amesema Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani
CIA linaficha maelezo muhimu kuhusu hatima ya ndege ya Malaysia
iliyotoweka. Katika taarifa aliyochapisha katika weblogu yake siku ya
Jumapili, Mahathir Mohammad amesema CIA na shirika la utengenezaji ndege
la Marekani, Boeing, kwa pamoja zinaficha maelezo kuhusu ndege
iliyotoweka. Aidha amesema ni jambo la kushangaza kuona vyombo vikubwa
vya habari duniani havifuatlii kwa kina kadhia ya ndege hiyo ya
Malaysia. Mahathir amesema yamkini CIA iliongoza ndege hiyo kwa mbali na
kuiweka katika mfumo wa kujiendesha yenyewe kisha ikatua eneo la siri
na alama zake za Malaysian Airlines kuondolewa. Ndege
hiyo ya Shirika la Ndege la Malaysia iliyotoweka tarehe 8 mwezi wa
Machi mwaka huu ikiwa na mamia ya abiria ilipokuwa inaelekea Beijing,
China kutoka Kuala Lumpur Malaysia. Pamoja na kuwa nchi kadhaa
zinashirikiana katika juhudi za kuitafuta ndege hiyo kwa kutumia
teknolojia ya kisasa lakini bado hakuna athari zozote za ndege hiyo ya
kisasa aina ya Boeing 777-200ER iliyotengenezwa Marekani. Waziri Mkuu wa
Malaysia Najib Razak naye pia alinukuliwa akisema ndege ya abiria ya
nchi hiyo iliyotoweka ilipotoshwa mkondo wake kwa makusudi na kuendelea
kuruka angani masaa kadhaa hata baada ya kutoweka kwenye rada.
