Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano, Majaliwa Kassim Majaliwa.
SERIKALI imewasimamisha kazi watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ambao jana iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani.
Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw.
Robert Nyoni. Uamuzi huo umetolewa Jumamosi, Novemba 28, 2015 na Waziri
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma
zinazowakabili. Kama ilivyo kwa wenzao sita waliosimamishwa kazi jana
(akiwemo aliyekuwa Kamishna Mkuu), nao pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda
nje ya nchi hadi uchunguzi utakapokamilika. “Kazi ya kuwachunguza
ilianza jana ileile na sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya
utumishi ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi,” alisema Waziri
Mkuu. Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt.
Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi
hao. Jana mchana, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushtukiza kwenye
bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua namna shughuli
zinavyoendelea kwenye bandari hiyo hasa kwenye maeneo ya kupokelea
mizigo kutoka nje ya nchi. Katika kikao kilichofanyika bandarini hapo na
kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Waziri Mkuu aliamua
kuwasimamisha kazi maafisa watano na TRA kutokana na ‘upotevu’ wa
makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-. Waziri Mkuu
alisema upotevu huo unasababishwa na mchezo unaofanyika baina ya
wafanyabiashara na watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena kupita
bila kulipiwa ushuru na hivyo kuikosesha Serikali mapato.